0


Timu ya soka ya Ndanda FC ya mkoani Mtwara imeendelea kujihakikishia kubaki katika ligi kuu ya Tanzania bara, baada ya hii leo kufanikiwa kufikisha pointi 30 katika msimamo kwa kuifunga Mwadui FC ya Shinyanga kwa mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Mabao ya Ndanda yamefungwa na Bryson Raphael katika dakika 29 baada ya kuachia shuti kali la nje ya 18 lililomshinda mlinda mlango Shabani Kado na Ahmad Msumi aliyefunga bao la ushindi dakika ya 90 kwa kuunganisha krosi ya Atupele Green, huku bao la kufutia machozi la Mwadui likifungwa na Kelvin Kongwe dakika ya 61 baada ya kuwatoka walinzi wa Ndanda waliodhani kuwa ameotea.

Kocha wa Mwadui, Jamuhuri Kiwelo amesema timu zote zimecheza vizuri lakini Ndanda waliweza kutumia vizuri nafasi walizozipata na kuweza kupata ushindi huo na kudai kuwa goli la pili lilitokana na nafasi ambayo ilipotezwa na Mwadui langoni mwa Ndanda.

Naye, kocha msaidizi wa Ndanda, Mussa Mbaya, amesema pamoja na timu yake kuonekana kupata matokeo mazuri kwa baadhi ya mechi zake katika kuelekea mwisho wa ligi, lakini bado anahitaji kushinda zaidi ili ajihakikishie kubaki katika ligi, huku akiwasifu wachezaji wake kwa kucheza kwa kutokata tamaa na kuweza upata goli dakika za mwisho.
Matokeo mengine ya mechi zilizopigwa leo ni:-
Mtibwa Sugar 1 - 1 Tanzania Prisons
African Sports 1-0 Kagera Sugar

Post a Comment

 
Top