Deni la Taifa limeongezeka kwa Sh7.05 trilioni, kutoka Sh26.49 trilioni Juni 30, 2014, hadi Sh33.54 trilioni sawa na ongezeko la asilimia 27.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Assad, deni la ndani ni Sh7.99 trilioni huku deni la nje likiwa ni Sh25.55 trilioni.
Akiwasilisha ripoti hiyo jana bungeni, alisema kiwango hicho cha ongezeko la deni ni kikubwa katika kipindi cha muda mfupi.
“Uchambuzi wangu umeonyesha kuwa malipo ya kugharimia madeni ya Sh4.6 trilioni mwaka huu ni sawa na asilimia 46 ya makusanyo ya ndani ya Serikali ambayo ni Sh10.8 trilioni,” alisema.
Alisema gharama hizo zikijumuishwa na gharama nyingine kama mishahara ya wafanyakazi na malipo ya likizo, Serikali hubaki na kiasi kidogo cha fedha za kugharimia miradi ya maendeleo na huduma nyingine za kijamii.
Profesa Assad alipendekeza mambo matatu kama sehemu ya mikakati ya kukabiliana na ongezeko la deni hilo, ikiwamo Serikali kuongeza jitihada za ndani za kuhamasisha ukusanyaji mapato ili kujenga wigo mpana wa kulipa madeni.
Pia, alishauri kuwapo kwa mpango mkakati kuhusu fedha, hasa upunguzaji wa gharama na mikopo yenye masharti.
Jambo la tatu, alishauri Serikali kuwa na uratibu mzuri wa shughuli zinazohusisha miamala ya fedha za kigeni, akisema hatua hiyo inawezekana kama kutakuwapo usimamizi thabiti.
Post a Comment