MARAIS
wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wameanza
kuzungumza lugha moja wakisisitizana kuchapa kazi, kuondokana migogoro
ya ndani na porojo za kisiasa kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Msimamo
wa viongozi hao ulijidhihirisha jana kupitia hotuba zao kwenye hafla ya
kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara yenye kilometa 234.3 kutoka
Arusha-Holili hadi kuingia Voi, Kenya itakayogharimu dola za Marekani
milioni 353. Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na marais Yoweri Museveni
wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na James Wani Igga aliyemwakilisha
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kirk.
Wakiongozwa
na mwenyeji wao, Rais John Magufuli, anayeongozwa na falsafa ya ‘Hapa
Kazi Tu’ katika kuongoza Tanzania, marais Uhuru na Museveni
walidhihirisha utayari wao wa kuunga mkono falsafa hiyo, kuhakikisha
wanazifikisha nchi wanachama kwenye neema.
Katika
hotuba yake, Magufuli aliwataka marais wenzake kujikita katika
kushirikiana na kuacha tofauti za ndani kwa kuwa wananchi wanasubiri
maendeleo kwa kasi ya hali ya juu. Akihimiza nchi wanachama kumaliza
tofauti za ndani mwao, Magufuli alisema nchi za EAC ni tajiri ingawa kwa
sasa ni masikini wa kutupwa na ombaomba.
Alisema
hazipaswi kuwa ombaomba, bali kinachotakiwa ni kujipanga kikamilifu na
kusonga mbele na kuacha tofauti ya kiitikadi ndani ya vyama vya siasa
uchaguzi ulishapita. Alisisitiza kwamba wananchi wa EAC wana shida
nyingi. “Hatutakiwi kuwa masikini kiasi hiki. Ni lazima tufike mahali
tujiulize ni nani aliyeturoga, kama yupo mchawi lazima tumtafute
tumkemee...,” alisema.
Malizeni matatizo ndani
Magufuli
alisema kila nchi ina matatizo yake ya ndani, ambayo yanapaswa
kutatuliwa kuhakikisha rasilimali zake zinatumika kuleta maendeleo.
Alitoa mfano wa Sudan Kusini yenye madini aina zaidi ya 22, eneo la
kilimo na ng’ombe wengi, kwamba wanakabiliwa a mgogoro wa kugombania
madaraka ambao hawana budi kuumaliza na kusonga mbele.
“Hata
Tanzania tunayo matatizo yetu, hata Rwanda wana matatizo yao… Kwa sisi
tuliopewa dhamana, tushiriki kikamilifu kuondoa matatizo ya nchi zetu,”
alisisitiza. Aliendelea, ‘’Sasa umefika wakati sisi viongozi (marais)
kumaliza matatizo ya ndani ya nchi na nchi kusonga mbele kwani ni
viongozi wa wananchi wa itikadi zote,dini zote na makabila yote bila ya
kubagua’’.
Rais
Magufuli alisema yeye akiwa Mwenyekiti wa EAC, wameamua kwa pamoja
kujenga viwanda katika nchi hizo kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi zao,
kwani kwa sasa asilimia 63 ya vijana hawana ajira.
Alisema
marais wa EAC wameamua kujenga viwanda kwa lengo la kutoa ajira kwa
vijana hao, ambao wako vijiweni na hiyo itasaidia mazao ya kilimo na
biashara yanayolimwa katika nchi hizo, kupata soko na kuuzwa ndani ya
ukanda na hata nje kwa faida ya wananchi.
Rais
alieleza kusikitishwa kuona zao la biashara kama vile pamba, inalimwa
nchini lakini inasafirishwa kwenda nje na kutengenezwa nguo na baadaye
zinarudishwa nchini kama mitumba baada ya kuvaliwa. Alisema Tanzania
sasa haiwezi tena kuwa shamba la bibi kwa wachache kujinufaisha zaidi na
masikini kuwa masikini zaidi.
Utumbuaji majipu bado
Rais
alisema uamuzi anaofanya wa kuwachukulia hatua watu wanaotumia vibaya
madaraka na wala rushwa, si wa kuwaonea, bali vipo vitu vya hovyo
ambavyo vimefanyika na kuumiza mamilioni ya Watanzania. Alisisitiza
kwamba, wote waliofanya hivyo watachukuliwa hatua na kufikishwa
mahakamani, hatimaye wafungwe.
‘’Nisipochukua
hatua kwa mambo yalivyofanyika, haina haja ya mie kuwa Rais. Kuna mambo
ya hovyo hovyo jamani yamefanyika. Nitawafukuza tu. Hilo halina
msamaha,’’ alisema. Magufuli aliomba wananchi wa EAC wawe watulivu,
akisisitiza kwamba marais wameamua na ndiyo maana miongoni mwa maazimio
yao ni kufanya nchi ziwe na viwanda.
Alisema
viongozi wakiungwa mkono na wakaombewa kwa Mungu, wataweza kutekeleza
waliyodhamiria. “Mkituombea tutekeleze tunayoweza kufanya tutaweza,
msipotusaidia hatutaweza… na ndiyo maana kwa Watanzania wenzangu
tumekuwa na hatua ndogo ndogo tunazofanya kushughulikia watu
walioneemeka na mambo ya hovyo.
Alisema
kwa upande wa Tanzania, kazi ya kutumbua majipu inaendelea na hata
idadi ikifika 2,000 haoni tatizo, ilimradi Watanzania walio wengi
wanufaike. “Watuache tufanye kazi kwa ajili ya Watanzania walio
wanyonge. Tanzania ilikuwa shamba la bibi, watu walikuwa wakifanya ya
hovyo. Nimekuwa waziri kwa miaka 20 ninayajua,” alisema.
Alisisitiza
kwamba mambo ya mateso kwa wananchi hayana chama. Alisema hatua
wanazotaka kuchukua ni kwa ajili ya maslahi ya wananchi wote bila kujali
itikadi zao. Huku akikiri kwamba kazi hiyo ni ngumu na ya ajabu,
aliendelea kuomba waombewe lengo la kusaidia wananchi litimie.
“Tusipofanya,
hakuna sababu ya mimi kuwa rais, ni vyema niende nyumbani nikalale,
hakuna sababu ya mimi kuitiwa rais..kwa hiyo nawaomba ndugu zangu
Watanzania mniunge mkono tufanye haya tunayofanya….mambo ya hovyo.”
Aliendelea kusema, “ juzi tumeshindwa kuingia mambo ya roaming kwenye
EAC kwa sababu sisi hatujasafisha nyumba yetu.
Kwenye
TCRA ilibidi nifukuze baadhi ya wafanyakazi ; Pale zaidi ya Shilingi
bilioni 400 zimepotea, tungeweza kununua ndege na kutengeneza barabara.
Lakini watu wamechezea pale na bado wanajiita wasomi.
Na
ndiyo maana tumeamua kufukuza, na tutawafukuza na bado watapelekwa
mahakamani. Wafungwe wapate machungu ya wananchi waliyotengeneza miaka
mingi,” alisema akisisitiza kuwa ni lazima ifike mahali waache
kuvumiliana na kuoneana aibu.
Aonya uvyama
Magufuli
ambaye alitumia nafasi hiyo, kuwashukuru wakazi wa Arusha kwa kumchagua
kuwa Rais, aliwahakikishia kuwa yeye ni Rais wa Watanzania wote
akisisitiza kutowabagua kwa misingi ya vyama na itikadi nyingine.
“Nataka
niwahakikishie mimi ni kazi tu,” alisema. Alimpongeza Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari akisema hana makeke, anajali maisha ya watu.
“Nisipompongeza nitakuwa mnafiki.
Ni
kijana safi, hana makeke, anajali maisha ya watu…uchaguzi umeisha,
tufanye kazi tuhakikishe wananchi wanapata maendeleo,” alisema na
kutania akisema, “Ukimuona Nassari sura yake ni Chadema lakini moyo wake
ni CCM.”
Aliwaambia
marais wenzake kwamba, wananchi wote walio kwenye nchi za jumuiya
wanachohitaji si vyama, bali wanataka maisha mazuri. Alisema mambo ya
kuomba omba misaada hayana budi kuisha.
Vile
vile alisema mambo ya watu wachache kuwa matajiri na wengine wakabaki
masikini , pia yaishe. Alisema marais wa nchi wanachama wanapaswa
kujikita kubadilisha maisha ya wananchi wote wa Afrika Mashariki.
Uhuru afagilia ‘Kazi Tu’
Kwa
upande wake, Rais wa Kenya, Uhuru alisema, “Tupunguze maneno na sasa
iwe kazi tu wananchi wafurahie nchi zao. Tutengeneze kila kitu hapa hapa
EAC na siyo kununua kutoka nje ya nchi hii ni aibu.”
“Tunapaswa
kuanza rasmi safari ya kwenda Kanani (matumaini) na safari hii ndefu
sana, lakini ina manufaa kwa wananchi wa nchi za EAC kwani safari hiyo
ikikamilika na kufika kunakohitajika, vijana wengi watapata ajira,”
alisema.
Aidha,
alisema anatambua historia ya Rais Magufuli akiwa Waziri jinsi
alivyowezesha ujenzi wa barabara nchini. Alimwomba aendelee na ujenzi wa
barabara ziungane na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Akihimiza
uchapa kazi, Uhuru alisema serikali za nchi za EAC zimelala na siyo
wananchi kwani wanashirikiana kwa kila hali ikiwemo kufanya biashara kwa
pamoja bila ya kubaguana. Rais Uhuru alisema wananchi wa EAC wanafanya
biashara kila mara na kila kona lakini viongozi wa nchi hizo wako katika
usingizi mzito kwa kuweka vikwazo vya hapa na pale.
Alisisitiza
marais kuondoa vikwazo hususan mipaka na vizingiti , badala yake
waruhusu wananchi wafanye biashara ya wazi bila ya kificho kwa maslahi
ya nchi hizo za ukanda. Alisema viwanda vingi vya nguo vimekufa katika
nchi za jumuiya bila sababu za msingi.
“Na
sasa tunaamua kuvaa mitumba. Hilo lazima libadilike,” alisema.
Aliendelea kusisitiza, “mmejaliwa kuwa na gesi na gesi iwanufaishe kwa
asilimia kubwa na pia gesi hiyo ije nchini kwangu kwa kuuzwa kwa bei
nafuu.”
Museveni
‘akubali’ Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema Afrika imelala,
inashtuka kutaka maendeleo wakati kumekucha, jambo alilosema kwa sasa
halitakiwi kwa watu wa EAC, kwani wanapaswa kuamka na kufanya kazi ya
kuinua uchumi bila ya woga.
Rais
Museveni alisema serikali ya Tanzania imejitahidi kujenga barabara zake
za ndani, tofauti na zamani hivyo nguvu hiyo inapaswa kuunganishwa
katika nchi za jumuiya. Alisema zamani alikuwa akitumia gari aina ya
Land Rover ya kizamani kusafiri katika baadhi ya mikoa lakini kote huko
kulikuwa hakuna lami bali kulikuwa na vumbi.
Alisema
lakini sasa anaweza kuja nchini na usafiri huo hadi jijini Dar es
Salaam kwa kuwa kila kona kuna lami. Aliomba viongozi wenzake
kushirikiana kwa dhati kujenga barabara katika nchi za EAC akisisitiza
kuwa hizo ni sehemu ya shughuli za kimaendeleo na kiuchumi
zitakazowezesha nchi kusonga mbele bila vikwazo.
Barabara
iliyozinduliwa Mradi huo wa ujenzi wa barabara unagharimiwa na Shirika
la Jica la Japan, Benki ya Afrika (ADB) pamoja na fedha za Serikali ya
Tanzania. Rais Magufuli alisema, kwa mara ya kwanza Arusha itakuwa na
barabara yenye njia nne.
Licha
ya marais Museveni, Kenyatta wakiwa na mwenyeji wao Rais Magufuli,
viongozi wengine waliohudhuriwa sherehe hizo za kuweka jiwe la msingi,
ni pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na viongozi wa EAC
akiwemo Katibu Mkuu wa Jumuiya aliyemaliza muda wake, Dk Richard
Sezibera.
|
Post a Comment