Rais wa Tanzania
John Magufuli amelalamikia tabia ya vijana wengi kukaa vijiweni na
kucheza pool badala ya kufanya kazi mijini na maeneo ya mashambani.
Rais Magufuli ametoa wito kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha watu wanafanya kazi hususani vijana."Haiwezekani vijana wawe wanashinda vijiweni wanacheza pool, wakati wazee na akina mama wapo mashambani wanalima. Kawahimizeni wafanye kazi, wasipofanya kwa hiari walazimisheni kufanya kazi," amesema Rais Magufuli, kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu.
Kiongozi huyo alitoa agizo hilo baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa 25 pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Jumanne.
Dkt Magufuli amewataka kwenda kufanya kazi kwa kujiamini na kujielekeza kutatua kero za wananchi.
Amewataka wakuu hao wa mikoa kusimamia ulinzi na usalama katika mikoa yao.
Aidha, Dkt Magufuli amewaagiza kusimamia udhibiti wa fedha za umma katika halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji na kumetoa siku 15 kwa halmashauri hizo pamoja na Wizara na Taasisi za Serikali kuondoa majina ya wafanyakazi hewa katika orodha za mishahara ya watumishi wa umma.
Dkt Magufuli amewasisitiza wakuu hao wa Mikoa kutosita kufanya maamuzi na kuchukua hatua haraka, huku akitaka wawasimamie ipasavyo wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu wa tarafa na watendaji wa kata na vijiji ili watekeleze wajibu wao.
Post a Comment