Ni swali wanalojiuliza watu wengi, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
(ZEC), kumtangaza Dk. Ali Mohamed Shein, kuwa mshindi wa nafasi ya
urais kwenye uchaguzi wa marudio uliofanyika Jumapili iliyopita kwa
kupata kura 299,982, sawa na asilimia 91.4.
Ushindi huo umeweka historia ya pekee kwa Zanzibar tangu kurejea kwa uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1995.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi huo wa marudio yaliyotangazwa na
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, anayemfuata Dk. Shein ni Hamad
Rashid Mohamed wa chama cha ADC, aliyepata kura 9,734 sawa na asilimia
tatu, huku Maalim Seif Sharf Hamad wa CUF aliyetangaza kususia uchaguzi
huo, akipata kura 6,076 sawa na asilimia 1.9.
Historia inasemaje?
Tangu mwaka 1995, CUF imekuwa mpinzani mkubwa wa CCM na karibu kila
uchaguzi, imekuwa ikitangazwa na ZEC kupata zaidi ya asilimia 40 ya kura
zilizopigwa.
Mwaka 1995, mgombea wa CCM, Dk. Salmin Amour Juma, alitangazwa kushinda
kwa kupata kura 165,271 sawa na asilimia 50.2 huku Maalim Seif wa CUF
akiwa na kura 163,706 sawa na asilimia 49.8 ya kura 328,977
zilizopigwa.
Kadhalika, mwaka 2005, Amani Abeid Karume wa CCM alishinda kwa kura
239,832 sawa na asilimia 53.2, huku Maalim Seif akifuatia kwa kura
207,733 sawa na asilimia 46.1. Kura halali zilikuwa 450,968.
Mwaka 2010, Dk. Shein wa CCM alipata kura 179,809 sawa na asilimia 50.1,
Maalim Seif kura 176,338 sawa na asilimia 49.1. Kura halali zilikuwa
358,815.
Kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka 2010, hali ya
kisiasa ya Zanzibar ilikuwa tete, hasa kutokana na viongozi wa CUF na
wanachama wake kuamini kwamba kwa miaka yote wamekuwa wakishinda, lakini
huibiwa kura.
Hali hiyo ilijitokeza dhairi Januari, 2001, baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2000, kwa kuibuka vurugu na watu kadhaa kupoteza maisha huku
wengine wakikimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya walikokaa kama
wakimbizi.
Baada ya uhasama wa muda mrefu, mwaka 2010 ilipoundwa Serikali ya Umoja
wa Kitaifa (SUK), hali ya kisiasa ya visiwa hivyo ilitulia.
Miaka mitano baadaye sasa, CUF imesusia uchaguzi wa marudio ikitaka
mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 2015 atangazwe, jambo linaloibua maswali
mengi juu ya mustakabali wa visiwa hivyo.
Hali ya Muungano
Kwa muda mrefu Wazanzibar wamekuwa wakilalamikia mfumo wa Muungano, hali
iliyofanya wakati wa mchakato wa Katiba Mpya wengi kupendekeza kuwa na
Muungano wa Mkataba.
Hata hivyo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilitokuwa chini ya Jaji Joseph
Warioba, ilipendekeza kuwa na Muungano wa Serikali Tatu ambazo
zilionekana kuungwa mkono na Wazanzibari, waliokuwa wanataka mfumo wa
mkataba. Lakini suala hilo liliota mbawa, baada ya Katiba
Inayopendekezwa kulitupilia mbali. Swali, ni je, baada ya uchaguzi huu,
hali itakuwaje?
Zanzibar yenye mamlaka kamili
Hoja ya Zanzibar yenye mamlaka kamili, imekuwa pia ikishinikizwa kwa
muda mrefu na chama hicho cha upinzani, ambacho kwa mujibu wa matokeo
hayo ya ZEC kwenye uchaguzi uliopita, yanaonyesha kimekuwa kikiungwa
mkono na zaidi ya asilimia 40 ya watu wanaopiga kura.
Chama hicho kutokuwa na mwakilishi hata mmoja kwenye baraza la
wawakilishi wala kiongozi serikalini, kunaweza pia kufanya hoja hiyo
sasa ikashika kasi, kutokana na kuamini kwamba kurudiwa kwa uchaguzi huo
kumetokana na shinikizo la Tanzania Bara.
Waziri wa Fedha wa SMZ, Omary Yusuph Mzee, akizungumza na Nipashe mapama
wiki hii, ofisini kwake eneo la Vuga, Zanzibar, alisema lengo la
serikali ni kuhakikisha inaondokana na utegemezi wa wafadhili.
Mzee alisema Zanzibar inategemea asilimia 20 ya misaada kwa ajili ya
kukamilisha bajeti yake kila mwaka pamoja na mikopo kutoka taasisi za
fedha, zikiwamo benki za nje.
Pia bajeti ya Serikali ya Zanzibar inategemea asilimia 20 ya mikopo
kutoka nje, jambo ambalo litaweza kuathiri maendeleo ya visiwa hivyo,
endapo nchi wahisani zitaweka mgomo kwa sababu ya uchaguzi huo.
Kauli hiyo ya Mzee inaibua swali la kwamba baada ya wahisani kuonyesha
kutoridhishwa na uchaguzi ulivyokuwa, nini hatma ya visiwa hivyo endapo
wakisusia kuchangia bajeti yake?
Utalii
Alisema bajeti ya Zanzibar inategemea asilimia 26 hadi 28 ya mapato
yanayotokana na sekta ya utalii wa ndani na nje na kwamba bado
kunahitajika mikakati ili kupanua wigo wa kupata fedha.
Kwa mujibu wa Mzee, Zanzibar inapokea watalii kati ya 300,000 na
400,000 kwa mwaka na kwamba wanatarajia wataongezeka baada ya kufungua
ofisi za kuhamasisha utalii wa nje.
Licha ya takwimu hizo kuonekana ziko juu, hali ya sasa ya takriban
asilimia 50 ya Wazanzbiar ambao wanaunga mkono CUF kususia uchaguzi wa
marudio, je hakutaathiri sekta ya utalii haswa ikitegemeana na historia
ya miaka ya nyuma kabla ya muafaka kufikiwa?
Wasomi wachambua
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jijini Dar es Salaam, Prof.
Haji Semboja wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), alisema utawala wa
Zanzibar haukuwa halali kushikiliwa na CCM, kutokana na mwitikio mkubwa
wa ushindi ulioonyeshwa na CUF.
“Rekodi ya uchaguzi uliopita inaonyesha vyama vya upinzani vilistahili
ushindi kwa Tanzania Bara na Visiwani tofauti na awali, kwa sababu kama
vimeweza kutoka asilimia 10 za ushindi na kuingia nafasi ya
kinyang’anyiro, kisiasa vilistahili kushika madaraka kama dhamira ya
serikali ni kuwa na vyama vingi,” alisema Prof. Semboja.
Alisema ingawa mfumo wa kiuchumi hautayumba kwa serikali hizo mbili
kutokana na madaraka hayo kushikiliwa na CCM, bado mfumo wa kidemokrasia
utaathiri vyama vinavyothubutu kushiriki uchaguzi, kwa sababu wananchi
wanataka mabadiliko.
Katika hilo, alimshauri Dk. Shein, kufanya majadiliano na vyama vya upinzani ili kuwapo na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Kwa sasa washirikiane wakae meza moja na kupanga maendeleo ya serikali
yao, lakini CCM wawe wapole na CUF wawe wastaarabu kwa maridhiano ya
pamoja kwa sababu nchi yetu ni moja, tujenge umoja wetu,” alisema
Semboja.
Naye Prof. Mwesiga Baregu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT),
alisema kama jitihada za haraka hazitafanywa na viongozi wa ngazi za
juu, akiwamo Maalim Seif, kuunganisha umoja wa wananchi, hali ya mauaji
inaweza kujitokeza.
Alisema uchaguzi si tendo la kuhesabu kura na kushinda, bali ni tendo la
kisiasa ambalo ndani yake linaunganisha muungano wa wananchi, hivyo
uchaguzi ukiwagawa wananchi katika matabaka, inamaanisha uchaguzi huo ni
batili kwa sababu haujaunganisha lengo moja.
Kwa mantiki hiyo, uchaguzi unaogawa wananchi na kuweka sura ya mpasuko
si sahihi wala haujatumia haki kwa sababu hautajenga maendeleo na badala
yake utabomoa,” alisema Prof. Baregu.
Alisema uchaguzi wa marudio, uliofanywa Zanzibar Machi 20, mwaka huu, na
kwa mara nyingine Dk. Shein kushinda urais kupitia CCM, umewapa
ubumbuazi na kuwapiga ganzi Wanzanzibar wengi, kwa sababu tatizo kubwa
ni uhalali wa rais aliyeshinda kwa wananchi.
“Ukifuatilia uchaguzi wa Oktoba, mwaka jana, mshindi hakutangazwa, na baadaye uchaguzi huu baadhi ya vyama vimejiondoa.
Kutakuwapo na hali ya kutoelewana kwa sababu uchaguzi huo, kulisababisha
mtafaruku kwa Wazanzibari tangu awali, hivyo mgogoro ni jambo
lisilozuilika kwa sasa Zanzibar,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Mawasiliano ni jambo la busara kwa nchi yoyote yenye
kupenda amani na taifa lake. Ushauri wangu serikali ya Zanzibar itafute
njia ya kukaa na vyama vya siasa ili kuingilia kati hali ya mvutano
unaoendelea kwa sababu wakipuuza jambo dogo waelewe hali ya uvunjivu wa
amani inaweza kujitokeza na mauaji yataendelea,” alisema.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Paul Kuwenga,
alisema suala la Zanzibar linahitaji kuangaliwa upya kwa sababu liko
katika kipindi cha mpito wa vyama vingi.
Alisema kinachotakiwa ni ushirikishwaji kwa sababu jamii inayoishi humo
ni mchanganyiko na kila moja ina uhuru wa kufanya uamuzi wake katika
jambo fulani, badala ya kushinikizwa wakubaliane kwa sababu nchi iko
katika utawala wa demokrasia.
KAULI YA DK. SHEIN AKIAPISHWA
Jana Zanzibar iliweka historia nyingine kwa wananchi wake kushuhudia
Rais wa awamu ya saba, Dk. Shein akila kiapo cha kuongoza visiwa hivyo.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othuman Makungu, alimwapisha Dk. Shein saa
tano asubuhi, ikifuatiwa na tendo la kupigiwa mizinga 21.
Dk. Shein ambaye aliingia uwanjani hapo akiwa na msafara wa magari 10 na
pikipiki 13, kabla ya kula kiapo, alikagua gwaride maalum la majeshi ya
ulinzi na usalama.
Rais huyo wa Zanzibar akizungumza baada ya kuapishwa, aliahidi kuongoza kwa haki na bila kumwonea mtu yeyote.
Aliwataka Wazanzibari kudumisha amani na umoja ili kuharakisha kujiletea
maendeleo yao, huku akisisitiza kwamba uchaguzi umekwisha.
Alisema atahakikisha amani inadumishwa na kwamba atavishughulikia
vikundi vyovyote vitakavyojaribu kufanya vurugu visiwani humo.
Pia aliahidi kuunda serikali makini ambayo itawasaidia Wazanzibari
kujiletea maendeleo ya haraka, huku akisema afanya hivyo kwa kuangalia
Ilani ya CCM ya mwaka 2015.
Dk. Shein alisema Zanzibar ina matatizo mengi na kwamba serikali makini itasaidia kutatua matatizo ya wananchi wake.
Aliwapongeza wapigakura ambao walimchagua na kusema kipaumbele chake ni
kuhakikisha amani inatawala visiwani humo na kwamba serikali
haitamvumilia mtu yeyote atakayejaribu kuvunja amani.
Aliwaomba viongozi wa dini kuhubiri amani na kwamba serikali yake
itahakikisha inawaunganisha Wazanzibar wote bila itikadi za vyama vyao.
AHADI YA SHEIN KWA MAGUFULI
Dk. Shein alimwahidi Rais John Magufuli kwamba atashirikiana na Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusimamia misingi ya uwajibikaji
na kuhakiksha watumishi wa umma wanakuwa na nidhamu.
"Nitaunda serikali makini ambayo inafuata maadili na hili nitahakikisha linafanyika haraka iwezekanvyo,” alisema.
Kabla ya kula kiapo, Dk. Shein aliombewa dua na viongozi wa dini,
akiwamo Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Khamis Haji Khamisi na Askofu wa Kanisa
Katoliki Zanzibar, Augstine Shao na Askofu wa Kanisa la Anglikana,
Michael Hafidh.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo Mawaziri,
Makatibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Magufuli,
baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, Marais wastaafu na wananchi wa
kawaida.
Viongozi wa chama kikuu cha upinzani cha CUF pamoja na wafuasi wao hawakuhudhuria sherehe hizo.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment