![]() | |
|
BARAZA la
Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Monduli mkoani Arusha ambalo
linaundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), limemuunga
mkono kwa vitendo juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli za `kutumbua
majipu’, wakisema hatua hiyo inarudisha heshima na nidhamu katika
utumishi wa umma.
Aidha,
jana walichukua hatua ya kupendekeza katika mamlaka husika kusimamishwa
kazi kwa watumishi watatu wa Idara ya Ardhi wilayani hapa, kupisha
uchunguzi wa hasara ya zaidi ya Sh milioni 700 kutokana na kuuzwa kwa
viwanja 100 bila kufuata taratibu. Aidha, wametaka baada ya uchunguzi
huo wahusika wafikishwe mahakamani kushtakiwa.
Wakimzungumza
ndani ya kikao kwa nyakati tofauti, walisema wanamuunga mkono kwa dhati
Rais Magufuli aliyejipambanua kuwa anakerwa na tabia ya ufisadi, rushwa
na matumizi mabaya ya madaraka zinazofanywa na watumishi wa umma.
Akitangaza
maazimio hayo mbele ya kikao cha Baraza la Madiwani juzi baada ya kukaa
kama kamati, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Isaack Joseph maarufu kwa
jina la Kadogoo, alisema maamuzi yote hayo ni kuhakikisha wanarejesha
nidhamu ya utumishi serikalini na kuunga mkono jitihada za Rais
kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma.
“Tumefikia
uamuzi huu si kwa kukurupuka tumefanya uchunguzi tumejiridhisha kwa
kushirikisha kila aliyestahili kushirikishwa na kufikia maamuzi haya ya
kuwasimamisha kazi watumishi hawa wa idara ya Ardhi,” alisema.
Aliongeza
kuwa, “ wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi rasmi na ukikamilika
wafikishwe katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi za kisheria na
stahiki ili hatua zaidi zichukuliwe.”
Aliwataja
watumishi ambao wamekumbwa na maamuzi hayo kuwa ni Leonard Haule ambaye
ni mpimaji ardhi, Ofisa Ardhi mteule Kitundu Mkumbo na Mrasimu ramani,
Leoni Mkwavi ambapo wanadaiwa kuuza viwanja na fedha kutoziwasilisha
kwenye halmashauri na pia baadhi ya viwanja walivyouza kutoviingiza
katika ramani ya halmashauri.
Alivitaja
viwanja vilivyouzwa na watumishi hao kuwa vipo eneo la CDTI Monduli
Mjini na kutaja idadi yake kuwa ni zaidi ya viwanja 100 ambapo
halmashauri hiyo imeweza kukusanya fedha kiasi cha Sh milioni 500 pekee
mpaka Desemba mwaka jana na kupata hasara ya Sh milioni 700.
Wakizungumzia
kusimamishwa kwa watumishi hao, baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo
walipongeza uamuzi huo na kwa kusema hauna chembe ya malalamiko kwani
umefuata taratibu kutokana na malalamiko mengi yaliyopo Monduli baada ya
kuuzwa kwa viwanja hivyo.
Akizungumza
kwa niaba ya watumishi wenzake, Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hiyo,
Daudi Sabiga alisema huo ni utaratibu wa kiutumishi na kwamba utasaidia
kuleta nidhamu kwa watumishi wengine.
‘’Unajua
hivi sasa kuna hii sera ya utumbuaji majipu katika maeneo mengine
unasikia mtumishi kafukuzwa kazi kwa tuhuma ndogo ambayo haina
uthibitisho… lakini kwa hii ya hapa kwetu imefanyiwa utafiti wa kutosha
na wahusika kubainika na hatua zimechukuliwa za kuwasimamisha kama
taratibu za utumishi zinavyotaka na ikibainika bila shaka uhusika wao,
basi hatua zaidi za kinidhamu zinachukuliwa,” alisema Sebiga.
Aidha,
madiwani hao wameazimia kwa pamoja kumuomba Rais Magufuli kuutupia macho
Wakala wa Umeme na Ufundi Tanzania (TEMESA) mkoani Arusha kwa kile
walichodai nao ni `jipu’ kutokana na kutoa huduma zisizoridhisha na
zenye gharama kubwa.
Wamesema
wakati wakisubiri `jicho’ la Rais Magufuli ndani ya taasisi hiyo,
halmashauri ya Monduli haitapeleka vifaa na magari yao Temesa mkoani
hapa kwa ajili ya matengenezo.
Akifafanua,
Mwenyekiti huyo wa halmashauri hiyo alisema wameshangazwa na kupokea
hati ya madai kutoka Temesa ya matengenezo ya kuweka kioo cha gari cha
mbele cha Toyota Land Cruiser na raba zake inayowataka kulipa Sh 900,000
wakati gharama halisi katika maeneo mengine ni Sh 120,000.
“Ndugu
zangu waheshimiwa madiwani huu ni wizi na hili la Temesa Arusha ni jipu
ambalo Rais anatakiwa kulitumbua. Kutokana na huu ushahidi tulionao
tumeazimia kabisa bila woga kutopeleka vifaa vyetu vyote pale Temesa kwa
matengenezo na tutapeleka katika gereji nyingine ambazo zimeidhinishwa
Kisheria,’’ alisema.
Maamuzi
hayo mazito ya madiwani wa Halmashauri ya Monduli yamefanywa katika
kikao chao cha kwanza cha baraza la kawaida la madiwani pamoja na
maamuzi hayo kilipokea taarifa mbalimbali za kamati kwa robo mwaka ya
Oktoba hadi Desemba, mwaka jana.

Post a Comment