0


Wamiliki wa nyumba zilizowekewa alama za x zilizopo pembeni mwa barabara kuu ya Tanzam jijini hapa, wamelalamikia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mbeya wakidai zoezi hilo limegubikwa upendeleo.

Nyumba zilizowekewa alama hizo zipo pande zote za barabara, hususan mitaa ya Sai, Ilomba, Mama John na Soweto huku zikisababisha hofu kwa wamiliki wa hoteli na majengo makubwa.

Wananchi waliodai ni wamiliki wa nyumba zilizowekwa alama mitaa hiyo walifika ofisi za Mwananchi mjini hapa, wakilalamikaia wawekaji alama hizo kuwa wanapendelea.

“Wenye nyumba wa upande wa kulia wakizungumza nao vizuri wanawekea alama za kijani, lakini wa upande ambao hawajazungumza wanaweka alama nyekundu hata kama awali nyumba zilikuwa nje ya barabara,’’ alisema Samuel Dickson kwa niaba ya wenzake.

Dickson alisema kabla ya kuweka alama, wahusika wanafanya mazungumzo na wenye nyumba, hivyo kugeuza zoezi zima kutawaliwa na upendeleo au rushwa.

Kaimu Meneja wa Tanroads mkoani hapa, Suleiman Lawela alisema hana muda wa kuzungumzia suala hilo mpaka kazi itakapokamilika.

Hata hivyo, baada ya kubanwa alisema kwa ufupi: “Kazi inaendelea.”
Lawela alisema nyumba zinazowekewa alama ya x nyekundu zitabomolewa bila kulipwa fidia kwa sababu wameifuata barabara, lakini walipoweka kijani wanaweza kujitetea.

Alisema zoezi la ubomoaji litaanza muda wowote baada ya kumalizika kwa zoezi la kuweka alama hizo, ili kuweka barabara pana zaidi.

Kauli hiyo inatolewa wakati Tanroads imeweka alama ya x nyekundu na kijani kwenye zaidi ya nyumba 500 zilizopo barabara kuu ya kwenda Zambia, ikiwa ni ishara ya kuwataka wamiliki wabomoe kupisha ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Uyole hadi Mbalizi.

Taarifa ya Tanroads iliyotolewa hivi karibuni kwenye kikao cha bodi ya barabara ilisema Serikali imetenga Sh500 milioni kufanya upembuzi yakinifu na usanifu kwa maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo jijini hapa.

Post a Comment

 
Top