Mkurugenzi
Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga akiwatambulisha watumishi wa
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) alipoitembelea ofisi
hiyo mapema leo.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki
(Mb) akisisitiza uwajibikaji kwa watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) alipoitembelea ofisi hiyo mapema leo.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki
(Mb) akiagana na viongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mara
baada ya kumaliza ziara ya kikazi aliyoifanya Makao Makuu ya TASAF
mapema leo.
WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mhe. Angella Kairuki (Mb) ameuagiza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kusaidia jitihada za
serikali za kuwaondolea wananchi kero ya umaskini.
Mhe.
Kairuki amesema TASAF inayo dhima kubwa ya kuhakikisha kuwa huduma
inazozitoa kwa wananchi zinakwenda sambamba na misingi ya uadilifu na
utawala bora ili hadhi ya mfuko huo iendelee kuwa kubwa.
Waziri
Kairuki ameyasema hayo alipotembelea Makao Makuu ya TASAF jijini Dar es
salaam ambako alizungumza na watumishi wa mfuko huo ikiwa ni mwendelezo
wa ziara za kikazi katika taasisi zilizo chini ya Ofisi ya
Rais-Utumishi na Utawala Bora ambayo amepewa dhamana ya kuisimamia baada
ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John P. Magufuli.
“Ninawasisitiza
muhakikishe kuwa, walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
wananufaika vilivyo na fedha zinazotolewa ili hatimaye waweze kuondokana
na umaskini” alisema Kairuki.
Aidha,
Mhe. Kairuki ameuagiza uongozi wa TASAF kuweka utaratibu utakaowezesha
ukaguzi wa mara kwa mara wa walengwa wa Mpango huo nchini kote ili
kuhakikisha kuwa watu wasiostahili wanaondolewa kwenye utaratibu wa
ruzuku na kupunguza malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
Mhe.
Kairuki ameonya vikali dhidi ya uwezekano wa kuweko matumizi mabaya ya
fedha kwa kutoa ruzuku kwa watu wenye uwezo jambo ambalo amesema
halipaswi kufumbiwa macho na pale itakapobainika wahusika wachukuliwe
hatua za kuwaondoa kwenye Mpango na kisha kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria.
Katika
hatua nyingine, Waziri Kairuki ameuagiza uongozi wa TASAF kutoa
mapendekezo ndani ya siku 30 ya namna ya kukabiliana na malalamiko
yanayoelekezwa kwa watendaji wa ngazi za vijiji,kata,na hata wilaya
ambao wamekiuka taratibu za kuwabaini na kuwaorodhesha walengwa wa
Mpango wa Kunusuru Kaya maskini ili hatua zichukuliwe haraka
iwezekanavyo.
Awali
akitoa maelezo kwa Waziri, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus
Mwamanga amesema Mfuko umefanikiwa kuandikisha zaidi ya walengwa Milioni
1.1 ambao wanaendelea kupata ruzuku na kuwa hadi kufikia mwezi Januari
2016 zaidi ya shilingi Bilioni 204 zimetolewa kwa walengwa ambapo
matokeo chanya yameanza kuonekana hususani katika Nyanja za elimu, afya
na makazi.
Bwana
Mwamanga amesema licha ya changamoto zilizopo hususani katika
upatikanaye wa fedha za kukidhi idadi kubwa ya walengwa ,Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF )umeendelea kufanya juhudi za kutafuta fedha
kutoka kwa wadau wa maendeleo na kuiomba serikali kuona namna inavyoweza
kuunga jitihada hizo ili hatimaye vita dhidi ya umaskini iweze
kufanikiwa .
Kuhusu
Mpango wa kunusuru kaya maskini, Bw. Mwamanga amesema walengwa wa
Mpango huu wamehamasika kwa kiwango kikubwa huku wengi wao wakionyesha
uwezo katika kufuata masharti na taratibu za Mpango hivyo suala la
upatikanaji wa fedha kwa uhakika lina umuhimu mkubwa ili kutowavunja
moyo walengwa hao.
Post a Comment