0

KATIBU Mkuu wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Dk Prime Nkwela na watendaji wa baraza hilo, wamepewa siku 30 kukagua vyuo vyote nchini, kujiridhisha na usajili na utoaji wa elimu katika vyuo hivyo.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako. Alilitaka baraza hilo kuhakikisha linapata mwongozo bora katika kuvipandisha vyuo hadhi, kwani sio kila chuo kinaweza kuwa chuo kikuu.

Profesa Ndalichako alisema hayo jana wakati akizungumza na watendaji wa Baraza hilo baada ya kuzungumza na watendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET). Alisema kuwa wizara itakaa kuangalia mahitaji ya Taifa, kwani bado linahitaji wasomi kutoka ngazi mbalimbali, ikiwemo astashahada na stashahada kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali.
Alisema suala la utoaji wa elimu bora, linatakiwa kuangaliwa kwa upana zaidi, kwa kuwa elimu iliyopo ipo katika makaratasi na sio katika vichwa vya wanafunzi waliohitimu.
Alisema wapo baadhi ya wahitimu wa elimu ya juu, ambao hawajulikani wanafanya nini, hivyo inapaswa kutoa elimu inayolingana na mahitaji kwa wanafunzi kuweza kufanya kitu chochote.
‘’Unapozungumzia udhibiti wa elimu unapaswa kuangalia kama elimu inayotolewa ina manufaa kwa wanafunzi au inaishia katika makaratasi. Mwanafunzi anaweza akajaza kitu katika makaratasi ya mitihani na kufaulu vizuri, lakini hana kitu alichoingiza katika kichwa chake,’’ alisema Profesa Ndalichako.
Alieleza kuwa baraza linatakiwa kutoa mwelekeo kwa Watanzania kwamba wanahitaji vyuo vya ufundi na vigezo vyake ni vipi ili watanzania wenye sifa waweze kujiunga.
Alifafanua kuwa watendaji wa NACTE, wanatakiwa wanaposajili vyuo vya elimu na vya ufundi, wawe tayari kupeleka watoto wao kujifunza katika vyuo hivyo. Alisema maofisa wasio wazalendo, wanasajili vyuo kwa kuona kuwa ni biashara, ambapo hata mtoto wake anamshauri akasome katika vyuo vizuri tofauti na alichokisajili.
‘’Sekta ya elimu imewekwa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji mali, utoaji wa elimu bora na sio soko. Nawaomba mkague vyuo vyote vilivyopo na mhakikishe kuwa hakuna chuo ambacho kina shaka yoyote ili tuweze kufikia malengo ya kuwa na elimu bora,’’ alisema.
Akizungumzia udahili wa wanafunzi, Profesa Ndalichako alisema kuwa vyuo ambavyo vipo nje ya mfumo wa NACTE katika kuhakiki taarifa zao, ndio chanzo cha kuwa na mianya ya udanganyifu. Alisema vyuo vyote vinatakiwa kuingizwa katika mfumo huo ili kupunguza udanganyifu wa vyeti vya kujiunga na vyuo.

Post a Comment

 
Top