0


Pato la taifa limeendelea kukua kwa kasi ya asilimia 6.3 katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba mwaka 2015 ukilinganisha na asilimia 5.4 mwaka 2014 katika kipindi kama hicho.

Takwimu hizo zilitolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk Albina Chuwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

“Pato la taifa katika kipindi hicho cha Julai hadi Septemba mwaka 2015 limeendelea kukua kwa kasi ya aslimia 6.3 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 5.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2014” alisema Dk Chuwa.

Aidha Dk Chuwa amesema kuwa, makadario ya pato la taifa kwa mwaka 2015 yanayotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 89.1 kwa mwaka mzima wa 2015 kama hakutakuwa na misukosuko ya kiuchumi.

Mbali na kukua kwa pato la taifa, takwimu hizo zimebainisha kuporomoka kwa uzalishaji wa bidhaa viwandani kwa asilimia 3.6 ukilinganisha na asilimia 6.3 kipindi  kama hicho kwa mwaka 2014.

Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Husein Kamote ametaja tatizo la ukosefu wa umeme kama moja ya sababu za kuporomoka kwa uzalishaji huo viwandani.

“Katika kipindi hiki hali ya upatikanaji wa umeme haikuwa nzuri na hata gharama zake zilikuwa juu, umeme ndiyo moyo wa sekta ya viwanda, kama unakuwa na shida basi uzalishaji viwandani huyumba,” alisema Kamote.

Naye Mhadhiri na Mtafiti wa Masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Semboja Haji aligusia kuporomoka kwa uzalishaji wa mazao kulikoelezwa na takwimu hizo.

“Kitaalamu ukuaji wa sekta ya kilimo hauridhishi kwa sababu tulitegemea kwamba kadri uchumi unavyokuwa na sekta hii nayo ikue hasa ukizingatia kilimo ndiyo chanzo cha kukua kwa baadhi ya sekta nyingine ya viwanda.” alisema Prof Semboja.

Post a Comment

 
Top