MFUKO wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF) unakamilisha maandalizi ya kupelekwa madaktari bingwa katika visiwa
vya Unguja na Pemba.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo,
Michael Mhando wakati akizungumza kabla
ya kumkaribisha mgeni rasmi katika hafla ya kutoa kadi za kikoa kwa wanachama
260 iliyofanyika Jang'ombe jana.
Hafla hiyo iliandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Jang’ombe
Ali Hassan King kuashiria kuanza kwa matibabu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
kwa mpango wa Kikoa ambao ni mpango wa hiari wa huduma za matibabu unaosimamiwa
na NHIF.
Alisema madaktari hao
watapelekwa katika maeneo ambayo watakubaliana na wenzao wa Zanzibar.
"Tunao mpango wa kutoa
huduma za kibingwa kwa kutumia madaktari bingwa ambao tutawapeleka maeneo
tutakayokubaliwa ili kutoa huduma hizo kwa wanachama wa mfuko na wananchi wote
kwa ujumla. Kazi hii tutaifanya hapa Unguja na tutaifanya vilevile Pemba,"
alisema.
Alisema hayo yatawezekana
baada ya kushauriana na wenzao wa Hospitali ya Mnazi Mmoja na Al-rahma namna
bora ya kufanikisha huduma hiyo.
Alisema lengo la kutoa huduma
hizo ambazo kwa upande wa Tanzania Bara, wiki ijayo wataifanya mkoani Ruvuma ni
kuwahudumia wananchi hata kama ni kwa vipindi vifupi lakini wawezeshwe nao
kupata huduma hizo ambao mara nyingi zinapatikana katika hospitali za rufaa.
Aidha katika hotuba yake hiyo
alisema kwamba wana mpango wa kuanza kutumia huduma za madaktari bingwa
waliostaafu kazi, ili waone namna bora kuweza kuwatumia katika programu za
kuhudumia katika maeneo mbalimbali yanayohitaji ujuzi wao.
Akizungumzia huduma za NHIF
katika visiwa hivyo Kaimu Mkurugenzi mkuu huyo alisema kwamba wanatoa huduma za
matibabu kwa wanufaika zaidi ya 43,056 waliopo Unguja na Pemba wengi wao wakiwa
ni watumishi wa Serikali ya Muungano na familia zao.

Post a Comment