0
Al-ShababMajeshi ya Kenya yamekuwa yakikabiliana na wanamgambo wa al-Shabab Somalia tangu 2011
Rais Uhuru Kenyatta amesema majeshi ya Kenya yatawinda wapiganaji walioshambulia kambi ya majeshi ya Muungano wa Afrika nchini Somalia na kuua wanajeshi.
“Tutawawinda wahalifu waliohusika katika matukio ya leo. Damu ya wanajeshi wetu haikumwagwa bure,” amesema kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
Rais Kenyatta amethibitisha kwamba kambi ya wanajeshi wa Muungano wa Afrika (Amisom) katika eneo ambalo linasimamiwa na majeshi ya Kenya ilishambuliwa asubuhi.
Hata hivyo, hakueleza waziwazi kuhusu iwapo ilikuwa kambi ya majeshi ya Kenya.
Wapiganaji wa Al-Shabab wamesema waliua wanajeshi wengi wa Kenya baada ya kuvamia kambi ya majeshi ya AU Somalia.
Kundi hilo la Kiislamu limesema liliteka na kudhibiti kambi hiyo mjini el-Ade na kuua wanajeshi 63 wa Kenya.
Wakazi wameambia BBC kwamba wapiganaji hao wa al-Shabab wamepandisha bendera yao katika kambi hiyo na kwamba walionyesha miili ya wanajeshi waliouawa katika barabara za mji huo.
  Kenyatta
Rais Kenyatta amekiri wanajeshi wa Kenya waliuawa Somalia
Lakini msemaji wa majeshi ya Kenya Kanali David Obonyo alikuwa awali amesema kambi iliyoshambuliwa si ya majeshi ya Kenya.
Badala yake, alisema kambi iliyo karibu ya wanajeshi wa Somalia ndiyo iliyovamiwa na majeshi ya Kenya yalijibu shambulio hilo.
Idadi ya waliofariki kutoka pande zote mbili bado haijabainika, Kanali Obonyo amesema kupitia taarifa.
Ameambia BBC kwamba ripoti kuwa wanajeshi wengi wameuawa ni “propaganda ya kawaida kutoka kwa al-Shabab”.
Kambi iliyoshambuliwa inapatikana eneo la El-Ade, kusini magharibi mwa Somalia.
"El Adde inasimamiwa na Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF) yanayohudumu chini ya Amisom. Wanajeshi wetu walichukua hatua upesi kulinda kambi yao; kulinda amani na uthabiti ambao wamo Somalia kudumisha; na kulinda taifa letu dhidi ya maadui na washirika wao," amesema Rais Kenyatta kupitia taarifa.
“Inahuzunisha kwamba baadhi ya wanajeshi wetu waliuawa. Inavunja moyo.”
Baada ya kutokea kwa habari za shambulio hilo, Wakenya mtandaoni wameanza kutumia kitambulisha mada #IStandWithKDF kuomboleza wanajeshi waliouawa na kuonyesha uungaji mkono wao wa juhudi za jeshi Somalia.
  AU
Wanajeshi wa AU husaidia serikali ya Somalia
Kenya ina majeshi 4,000 kwenye kikosi cha AU nchini Somalia ambacho kina wanajeshi 22,000.
Kikosi hicho, ambacho hujulikana kama Amisom, huungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Mkazi wa el-Ade ameambia BBC kwa njia ya simu kwamba alisikia mlipuko mkubwa mwendo wa saa kumi na moja unusu alfajiri na baadaye akasikia ufyatuaji mkali wa risasi.
"Tuliona mpiganaji wa al-Shabab mjini. Na pia tuliwaona wanajeshi wa Kenya waliokuwa wanatoroka kambi.
"Kwa sasa kambi imo mikononi mwa al-Shabab. Tunaona magari ya kijeshi yakiteketea na maiti za wanajeshi zimetapakaa. Hakuna raia aliyeuawa lakini lakini watu wengi wameutoroka mji.”
  Al-Shabab
Al-Shabab wamekuwa wakitekeleza mashambulio ya mara kwa mara Somalia
Afisa mmoja wa al-Shabab ameambia BBC kwamba wapiganaji hao walishambulia kambi hiyo baada ya sala ya asubuhi, walilipua lango la kambi kwa kutumia gari kisha wapiganaji wakaingia.
“Tulichukua udhibiti wa kambi baada ya saa moja ya mapigano makali,” amesema.
“Tulihesabu miili 63 ya Wakenya ndani ya kambi hiyo. Wanajeshi hao wengine wa Kenya walitorokea msituni na tunawawinda.”
Alisema wapiganaji hao watachukua magari 28 ya kijeshi kati ya 31 yaliyokuwa kwenye kambi hiyo pamoja na silaha zote.
 
Kambi mbili za kijeshi, moja ya Majeshi ya Kitaifa ya Somalia (SNA) na nyingine ya AU, zinapatikana eneo moja viungani mwa mji wa el-Ade, ambao unapatikana katika jimbo la Gedo, kilomita 380 magharibi mwa mji wa Mogadishu.
Al-Shabab walifurushwa kutoka mji mkuu Mogadishu, Agosti 2011, lakini bado wana nguvu baadhi ya maeneo ya Somalia na hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara nchini humo.

Post a Comment

 
Top