0

Selemani Jafo,Naibu waziri Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Picha ya Maktaba).
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa nchini kuandaa utaratibu wa kuwapeleka Wenyeviti na Mameya kupata mafunzo ya uongozi katika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kilichopo mkoani Dodoma.
Akizungumza mara baada ya ziara yake ya kukitembelea chuo hicho, mhe Jafo alisema kwa kuwa uchaguzi mkuu umepita na Madiwani wameshachaguliwa wanatakiwa wapewe mafunzo maalumu ya muda mfupi juu ya namna ya kusimamia na kuendesha halmashauri zao.
“Ninawaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuwasiliana na Ofisi ya Rais Tamisemi ili kujua namna ya kuwawezesha nauli Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Halmashauri na Mameya na Manaibu Meya kuja Chuoni Hombolo kwa siku tatu au tano kupata mafunzo juu ya uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa”.alisema.
Naibu Waziri huyo alisema ni vyema mafunzo hayo yakaanza na Wenyeviti wa Halmashauri, Makamu Wenyeviti, Mameya na Manaibu Meya ili kuwajengea uwezo Viongozi hao wa mamlaka za Serikali za Mitaa na kwamba ikiwa katika halmashauri 185 Madiwani wake wakiwezeshwa watakuwa na uelewa mpana wa masuala yanayohusu mikataba na malipo katika halmashauri zao.
Alisisitiza kuwa gharama wanazotakiwa kuwezeshwa katika halmashauri zao ni nauli tu kwani na kwamba Wakurugenzi hawatakiwi kuwalipa posho Wenyeviti hao wa halmashauri kwa kuwa kila kitu kinachohusu mafunzo hayo kitasimamiwa na Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo.
Aidha alisema baada ya mafunzo hayo Madiwani wengine watapata mafunzo hayo katika maeneo yao au kupitia Kanda zao kulingana na utaratibu wa Chuo kitakavyopanga.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Emanuel Gibai alisema Uongozi wa Chuo upo tayari kutoa mafunzo hayo kwa kuwa Wana watumishi wanaolipwa na Serikali kwa ajili ya mafunzo yanayohusu Serikali za Mitaa.
Alisema Chuo kina mabweni na madarasa ya kutosha kuwapokewa Madiwani hao wa Halmashauri watakaokuja wakati huu ili kuwajengea uwezo wa kuyahudumia maeneo yao.
Alisema kwa kipindi hiki ambapo Wanafunzi wamefunga chuo wanatarajia mafunzo hayo ya Wenyeviti na Makamu wenyeviti pamoja na Mameya na Manaibu meya yafanyike kati ya tarehe 10 na 20 januari ya mwaka 2016 katika Chuo hicho
Alisema Chuo kina wataalamu waliobobea katika uongozi wa Serikali za Mitaa na wapo tayari kuwafundisha madiwani wote pamoja na Viongozi wengine wa Serikali kwa utaratibu utakaopangwa na Wizara.

Post a Comment

 
Top