Yaya Toure ndiye mshindi wa Tuzo ya BBC ya Mwanasoka Bora wa Afrika wa Mwaka 2015.
Mashabiki walimpigia Toure, anayechezea Manchester City, kura nyingi kushinda Yacine Brahimi, Pierre-Emerick Aubameyang, Andre Ayew na Sadio Mane.
Alishinda tuzo hiyo mara ya kwanza 2013.
Brahimi kutoka Algeria amewahi kushinda tuzo hiyo 2014 naye Mghana Ayew aliishinda 2011. Aubameyang kutoka Gabon alikuwa akishindania tuzo hiyo kwa mwaka wa tatu mtawalia, huku Mane, kutoka Senegal, akishindania kwa mara ya kwanza.
Toure ameteuliwa kushinda tuzo hii mara sita na ushindi wake mara hii unahakikisha anafunga mwaka akiwa na tuzo kuu, sawa na alivyouanza kwa kuongoza Ivory Coast kushinda Kombe la Taifa Bingwa Afrika mwezi Februari.
Alikuwa nahodha wa timu hiyo Equatorial Guinea na alianza kufunga bao katika nusufainali na kuwezesha timu yake kulaza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 3-1.
Toure alitekeleza mchango mkubwa katika kusaidia taifa lake kufikisha kikomo muda wa miaka 23 wa kusubiri kushinda taji la pili la ubingwa Afrika, kwa kushinda Ghana kupitia mikwaju ya penalti.
Kilikuwa kikombe cha kwanza kwa Toure kushinda akiwa na timu ya taifa katika michuano ya sita ya dimba la Kombe la Taifa Bingwa Afrika, na walishinda baada ya kupoteza mara mbili kwenye fainali, mwaka 2006 na 2012.
Toure pia hakufana sana akiwa katika klabu yake ya Ligi Kuu ya Uingereza, ambayo ilishindwa kutetea taji la ligi waliloshinda 2014, kwa kumaliza wa pili nyuma ya Chelsea.
Lakini Toure amesalia kuwa nguzo katika safu ya kati na amechangia katika ufungaji wa mabao saba kwa klabu yake mwaka huu.
Vera Kwakofi, mhariri wa habari wa BBC Africa amesema: "Uongozi wa Yaya Toure kwa taifa na klabu ni mfano bora kwa wachezaji wengi chipukizi wanaotaka kuiga ufanisi wake.
“Tuna furaha kwamba kama BBC tuko hapa kusherehekea na kujivunia wakati huu na mashabiki wake kote duniani.
Washindi wa zamani wa Tuzo ya BBC ya Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka:
2014: Yacine Brahimi (Porto & Algeria)
2013: Yaya Toure (Manchester City & Ivory Coast)
2012: Chris Katongo (Henan Construction & Zambia)
2011: Andre Ayew (Marseille & Ghana)
2010: Asamoah Gyan (Sunderland & Ghana)
2009: Didier Drogba (Chelsea & Ivory Coast)
2008: Mohamed Aboutrika (Al Ahly & Egypt)
2007: Emmanuel Adebayor (Arsenal & Togo)
2006: Michael Essien (Chelsea & Ghana)
2005: Mohamed Barakat (Al Ahly & Egypt)
2004: Jay-Jay Okocha (Bolton & Nigeria)
2003: Jay-Jay Okocha (Bolton & Nigeria)
2002: El Hadji Diouf (Liverpool & Senegal)
2001: Sammy Kuffour (Bayern Munich & Ghana)
2000: Patrick Mboma (Parma & Cameroon)
Post a Comment