MBUNGE wa Jimbo la Ndanda wilayani Masasi kwa tiketi ya Chadema, Cesil Mwambe amesema atahakikisha halmashauri ya wilaya ya Masasi inakuwa bora inayotumikia wananchi kwa kutekeleza mambo mbalimbali yaliyoahidiwa wakati wa kampeni.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwambe alisema, si lazima kupiga kura ya hapana kwa kiongozi ambaye ana uwezo wa kuongoza kwa misingi ya mazoea. Alisema ana imani na uwezo wa mwenyekiti wa halmashauri aliyechaguliwa na ndiyo maana hakuona sababu ya kupiga kura ya hapana kwa mtu mwenye uwezo wa kutetea maslahi ya wananchi wa wilaya ya Masasi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Masasi aliyechaguliwa ni Juma Satma, ambaye ni Diwani wa kata ya Chiungutwa. Mbunge Mwambe alisema jukumu la madiwani ni kumsimamia mwenyekiti wa halmashauri.
“Naamini uwezo wa mwenyekiti wa halmashauri aliyechaguliwa na ndio maana nimempa kura yangu ya ndio,” alisema. Hata hivyo alitoa angalizo, “Lakini haina maana kwamba kila atakachokifanya nitakubaliana naye isipokuwa kwa imani yangu kwake niliona ni bora nikampa kura ya ndio ili nimwelekeze ninachotaka akifanye.”
“Katika kundi la wagombea kuna baadhi ya watu nilikuwa siwaamini na laiti wangepewa nafasi katika jambo hili muhimu mimi ningekataa mara moja na kamwe nisingewapigia kura ya ndio,” alisema.
Alisema jimbo la Ndanda ni jipya na kwamba linahitaji mtu mwenye uwezo atakayewaunganisha wananchi pamoja na halmashauri yao na kwamba maendeleo ya haraka yanahitajika ili liweze kufanana kama majimbo mengine ya zamani.
Aidha alitoa angalizo kwa madiwani wote wa halmashauri hiyo wakumbuke kuwa walitoa ahadi kwa wapiga kura wao wakati wa kampeni za uchaguzi na kwamba kwa sasa jukumu lao ni kutimiza kikamilifu ahadi zao walizozitoa.
Alisema yuko tayari kutoa ushirikiano kwa madiwani wote bila kujali vyama vyao katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye maeneo yao ikiwemo elimu, afya, maji, bei za mazao pamoja na miundo mbinu ya barabara.
Post a Comment