0


Kesho ni tarehe moja ya mwezi wa kumi na mbili kwa mwaka huu 2015. Hii ina maana kwamba tumebakiza mwezi mmoja tu, yaani siku 31 kumaliza mwaka huu 2015. Kwanza kabisa nikupe hongera kwa miezi hii kumi na moja ya mwaka huu 2015. Hongera hii ni muhimu kwako kwa kuwepo kwa kipindi chote hiki, iwe umekamilisha malengo yako au la.

Sasa leo nataka nikushirikishe kitu muhimu sana wewe kukifanya kabla mwaka huu 2015 haujaisha. Pia kitu hiki kitakuwezesha kuwa na mwaka bora sana ifikapo 2016. Ni kitu muhimu ambacho watu wengi wamekuwa wakikisahau na hivyo kushindwa kufikia kile wanachokitaka.

Lakini kabla hatujaenda kushirikishana kitu hiki muhimu hebu tutafakari kidogo mwaka huu 2015 ulikwendaje.

Najua hujawahi kupata muda wa kutosha kukaa chini nakutafakari kwa kina mwaka huu umekwendaje kwako. Ni mambo gani ambayo ulipanga kuyafanya, ni yapi ambayo umefanikiwa kuyafanya, yapi yamekushinda na pia ni yapi yamejitokeza ambayo hayakuwa kwenye mipango yako.

Leo hii tenga angalau nusu saa, na tafakari sana maisha yako kwa mwaka huu wa 2015. Fikiria kila kilichotokea kwenye maisha yako, iwe ulipanga au hukupanga, iwe kilileta majibu mazuri au majibu ambayo sio mazuri.

Wakati unafanya tafakari hii, kuwa karibu na kitabu chako cha malengo na andika mambo yote hayo.

Na ukishamaliza kuandika yote hayo malizia ni orodha hii muhimu sana kwako, andika mambo 10 mapya uliyojifunza kwa mwaka huu 2015. Mambo hayo yatokane na yale yote uliyopitia na kukutana nayo kwa mwaka huu 2015. Kumbuka haya yote unaandika kwa matumizi yako binafsi na hivyo andika chochote bila ya kujali ni kikubwa au kidogo, muhimu kiwe kitu ambacho umejifunza na unahitaji kuendelea kukitumia.

Umeshamaliza kutafakari mwaka wako na kuandika yale uliyojifunza? Usiseme utafanya hivyo baadae, fanya hivyo sasa, au andika mahali ambapo utakumbuka kufanya hivyo baadae. Sitaki uikose fursa hii muhimu sana kwako. Kwa sababu usipofanya hivi, ni bora hata usijisumbue kuweka malengo ya 2016, kwa sababu utakuwa unapoteza muda wako bure.
Mambo mawili ya kushangaza;

Jambo la kwanza; 
Sasa tupo kwenye mwezi wa mwisho kabisa wa mwaka huu.
Na kwenye mwezi huu wa mwisho, kuna jambo la ajabu sana ambalo huwa linatokea, karibu asilimia 90 ya watu hawaweki tena juhudi. Yaani ni sawa na mpira umekaribia dakika a 90 na hivyo wachezaji wa timu zote wameshachoka na wanasubiri tu filimbi ilie kwamba mpira umeisha.
Kwa wale ambao wamefanikisha malengo yao, wanapunguza kasi sana kwa sababu kile walichopanga wameweza kufikia na wanasubiri kwa hamu sana ifike tena 2016 wapange malengo mengine na wayafanyie kazi.

Kwa wale ambao wameshindwa kufikia malengo yao nao wanapunguza kasi kwa kuona kwamba mwaka huu haukuwa wao na hivyo kusubiri tu uishe na waone kama mwaka ujao 2016 unaweza kuwaendea vizuri.

Iwe wewe upo kwenye waliofanikisha malengo au ambao wameshindwa, nina ujumbe muhimu sana kwako leo hii, na kupitia ujumbe huu utakwenda kuboresha zaidi maisha yako.

Jambo la pili la kushangaza; 
Itakapofika tarehe moja mwezi wa kwanza mwaka 2016, kila mtu anakuwa kama amezinduka. Ndipo sasa kila mtu anaanza kuzungumzia malengo, wengine wanaweka malengo vizuri, wengine wanadakia tu malengo. Kila mtu anakuwa anaweka juhudi na kila kitu kinaonekana kwenda kwa kasi sana.

Angalia tofauti hizi mbili, mwezi wa kumi na mbili kila mtu amepunguza kasi, na mwezi wa kwanza wote wanaanza kwa kasi.
Sasa hapa kwa sisi ambao tunaelewa vizuri zaidi ndio tunataka kupatumia vizuri kuhakikisha mambo yetu yanakwenda kama tunavyopanga.

Jambo muhimu sana la kuzingatia. 
Leo hii nataka nikushirikishe jambo moja muhimu la kuzingatia ili kujihakikishia malengo yako ya 2015 yanakamilika vizuri na yale ya 2016 yanaanza vizuri pia.

Jambo hili muhimu ni kwamba mchezo ndio kwanza umeanza.
Ndiyo, wakati wengine wanapunguza kasi sasa, na kusubiri tarehe moja ianze ndio na wao waanze, sisi tunaendelea kuweka juhudi. Wakati wengine wanakata tamaa na kuona kwa siku hizi chache hakuna kikubwa wanaweza kufanya, sisi tunajua ni muda wa kutosha kwetu kufanya mambo makubwa.

Mwaka wenye miezi 13. 
Nakukaribisha kwenye mwaka wenye miezi kumi na tatu, najua wote tunajua ya kwamba mwaka kwa kawaida una miezi 12, lakini sisi wanamafanikio tunaweza kupanga mwaka wetu tutakavyo. Kwa sababu hata hii miezi na miaka tunayohesabu sasa, ni watu kama sisi walipanga kulingana na walivyoona itakuwa bora kwa wote.
Sasa sisi, namaanisha mimi na wewe ambaye umekubali, tunaanza kuhesabu mwaka wetu wa mafanikio kuanzia tarehe 01/12/2015 yaani kesho. Hivyo kesho tunahesabu kwamba tumeanza mwaka wetu mpya 2016.

Tunafanya nini sasa kwa kipindi hiki? 
Kwanza kabisa chukua yale malengo ya mwaka 2015 ambayo hukuweza kuyafikia, haya unayavusha kwenye mwaka wetu huu mpya unaoanza kesho. Halafu sasa weka malengo mengine kwa ajili ya mwaka huu 2016.

Hivyo kwa siku chache za mwezi wa 12 uwe umekamilisha kuweka malengo yako na uanze kuyafanyia kazi. Kwa njia hii utapata nafasi kubwa sana ya kuweza kuyafanyia kazi malengo ambayo ni halisi kwako na sio yale ya kuiga.

Kwa nini ni muhimu sana kufanya hivi? 
Ni muhimu sana wewe ufanye hivi, uanze mwaka wako 2016 mapema na uwe na mwaka wenye miezi 13 kwa sababu zifuatazo.

1. Unapata nafasi nzuri ya kuanza kutekeleza malengo yako.
Sasa hivi lengo lolote unalotaka kulifanyia kazi, kuna watu wachache sana ambao wanalifanyia kazi. Kama unataka kuongeza wateja kwenye biashara yako, wengine wengi kwa sasa wameshaanza kukaa kisikukuu sikukuu. Kama unataka kuongeza juhudi na thamani kwenye kazi yako, una uwanja mkubwa sana, maana wengine kwa sasa hawajisukumi, wameshaanza kufikiria sikukuu.

2. Unaepuka kelele na fujo za mwanzo wa mwaka.
Mwanzo wa mwaka kila mtu anakuwa bize kutekeleza malengo yake, wengine ni malengo ya ukweli na wengine ni malengo hewa, hivyo kunakuwa na kelele nyingi sana ambazo zinaweza kufanya uone mambo ni magumu. Hivyo unavyoanza mapema, wakati wengine ndio wanazinduka, wewe unakuwa umeshashika kasi.

3. Unaanza kujiweka tofauti na wengine. 
Nafikiri unakumbuka vyema sana ya kwamba hatua ya kwanza ya kufikia mafanikio makubwa, ni kuanza kuwa tofauti na kundi kubwa la watu. Sasa huwezi kuwa tofauti kama bado unasubiri tarehe moja ya mwezi wa kwanza ambapo kila mtu anaweka malengo na wewe ndio uweke malengo.
Kwenye wakati huo ni rahisi kujikuta unashawishika kuweka malengo ambayo hata sio muhimu kwako kwa sababu tu kila mtu anaweka malengo ya aina hiyo.
SOMA; Mambo 7 Yanayokufanya Ushindwe Kutimiza Ndoto Zako.

Je umeukubali mwaka huu mpya wenye miezi 13? 
Kama umekubali mwaka huu mpya wenye miezi kumi na tatu na upo tayari kuanza kuufanyia kazi, tafadhali niandikie email kwenye amakirita@gmail.com niandikie taarifa zako kamili, majina na namba za simu na kwa wiki hii ya kwanza ya mwezi wa 12 nitakufuatilia kujua kama unaweka malengo kweli na unayawekaje.

Semina ya mwaka 2016. 
Katika kuanza mwaka wetu 2016, ambao sisi wana mafanikio tunauanza kesho, tutakuwa na semina yetu ya kwanza kabisa kwa mwaka huo kwa njia ya mtandao. Semina hii italenga kutuandaa vyema ili kuweza kufikia malengo yetu makubwa ambayo tutakuwa tumeshayaweka tayari umeyaweka.
Katika semina hii utajifunza na kupata maarifa ambayo yataufanya mwaka 2016 kuwa tofauti sana kwako. Zile changamoto zote ambazo zimekuwa zinakuzuia wewe kufikia malengo yako utazipatia ufumbuzi.

Semina hii itaanza wiki ya kwanza ya mwezi wa kwanza, taarifa zaidi zitakuja siku sio nyingi. Usipange kuikosa semina hii nzuri, kwa sababu inaweza kuwa ndio kitu pekee kinachokuzuia mpaka sasa, kukosa maarifa sahihi ya jinsi ya kuyaendea malengo yako.

Nakukumbusha kama unakwenda kuanza mwaka wetu wa miezi 13 tuwasiliane.
Vinginevyo nikutakie kila la kheri katika shughuli zako, na nakusihi tuendelee kuwa pamoja. Maana mchezo ndio kwanza umeanza, na kwa elimu yetu hii hakuna siku ambayo utahitimu, kwa sababu kila siku kuna kitu kipya cha kujifunza.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani

Post a Comment

 
Top