JESHI la
Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema ajali za barabara
zimepungua hadi 7,570 kwa kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka huu
ikilinganishwa na ajali 13,466 zilizotokea kwa kipindi kama hicho mwaka
jana.
Kamanda
wa kikosi hicho, Mohamed Mpinga aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati
akikabidhi gari kwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jackson
Kapongo aliyejinyakulia gari aina ya Toyota surf lenye thamani ya zaidi
ya Sh milioni 24 katika shindano lililochezeshwa na Kampuni ya kuuza
magari ya Enhance Auto.
Alisema
katika ajali hizo, vifo vilipungua kutoka 3,437 mwaka jana hadi kufikia
vifo 3,195 mwaka huu huku majeruhi wakipungua kutoka 13,495 mwaka jana
hadi 8,566 mwaka huu.
Kamanda
Mpinga alisema ajali hizo zimepungua kutokana na elimu ya usalama
barabarani inayoendelea kutolewa kwa wananchi ambapo kwa wastani wa
ajali za kila mwezi zimepungua kutoka zaidi ya 1,000 kwa mwaka jana na
chini ya 1,000 kwa mwaka huu.
Alisema
mara nyingi kipindi cha kuelekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ajali
nyingi zaidi hutokea na kusababisha vifo na majeruhi na kuwataka
wananchi kuyatumia magari yao vizuri na kuzingatia sheria za usalama
barabarani ili kuepukana na ajali hizo.
“Tatizo
kubwa la ajali za barabarani ni mwendokasi, magari mabovu, ulevi na
kupita gari la mbele bila tahadhari hivyo tufuate sheria za usalama
barabarani ili tuepukane na ajali hizi,” alisema.
Akizungumza
kampuni hiyo, Mpinga alisema imekuwa ikichezesha shindano hilo kila
mwaka na kushirikisha nchi mbalimbali Afrika ambapo kwa mwaka jana
mshindi alipatikana kutoka Zambia, lakini kwa mwaka huu ameshinda
Mtanzania hivyo ni jambo la kujivunia.
Alisema
mbali na kutoa zawadi, lakini kampuni hizo za magari zina jukumu kubwa
la kutoa mchango kwa usalama barabarani kwa kutoa elimu sambamba na
kuuza magari yenye viwango vinavyokubalika ili kuepusha ajali zisizo za
lazima.
“Natoa
mwito kwa kampuni zingine kuwekeza katika usalama barabarani na
wasifikirie tu kuuza magari bali wahakikishe magari yanakuwa salama na
wanaoendesha wanakuwa salama... tuagize magari yenye viwango maana ajali
nyingi pia zinasababishwa na ubovu wa magari,” alisema.
Mapema
Mkurugenzi wa Enhance Auto, Aatif Farooq Butt alisema mshiriki alitakiwa
kushiriki kwa kuchagua mitandao yao ya kijamii kwa wingi zaidi na
lilishirikisha nchi ambazo wanafanya nao biashara ikiwemo Botswana,
Burundi, Jamhuri ya Congo, Malawi, Msumbiji, Sudan Kusini, Uganda,
Zambia, Zimbabwe na Tanzania.
Post a Comment