WAZIRI
Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa amewataka wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri
Mkuu watambue jukumu walilonalo la kuwahudumia wananchi kutokana na
majukumu ya ofisi hiyo yanayogusa maisha ya kila siku ya Watanzania.
“Ofisi
ya Waziri Mkuu ni kubwa na pana sana na inahusika na shughuli za kila
siku za Watanzania. Kwa hiyo tuna kazi kubwa ya kukidhi matarajio yao,”
alisema Majaliwa. Alitoa kauli hiyo jana mchana wakati akizungumza na
wakuu wa taasisi, wakurugenzi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu
kwenye mkutano uliofanyika ofisini kwake, Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Jana
ndiyo aliripoti kwa mara ya kwanza tangu alipoapishwa Ijumaa iliyopita
kwenye Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma. “Pamoja na kazi nyingine, tunayo
majukumu makubwa ambayo ni udhibiti, usimamizi na ufuatiliaji wa
masuala mbalimbali humu serikalini.
Ninatarajia
kupata mpango kazi kutoka kwa Mkuu wa kila idara na kila taasisi zilizo
chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nitakwenda pia ofisi za Tamisemi ili
kuweka vipaumbele vyetu sawa,” alisema.
Aliwataka
watumishi hao wawe tayari kutekeleza kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ambayo
imekuwa ikisisitizwa na Rais John Magufuli ili kumudu kasi ya utendaji
kazi Serikalini ambayo anahimiza hivi sasa. Alisema ana imani kuwa
watumishi hao watampa ushirikiano kama ambavyo walikuwa wakiutoa kwa
mtangulizi wake, Mizengo Pinda ambaye amestaafu hivi karibuni.
|
Post a Comment