Mara nyingi huwa napata nafasi ya kukutana na vijana wengi ambao ndio
kwanza wanakuwa wamemaliza masomo yao
ya chuo kikuu. Ni nafasi pia ambayo huwa naitumia kutaka kujua ni mipango gani
wamejiwekea baada ya kumaliza masomo yao.
Ni mengi ambayo huwa
ninayapata kutoka kwao, lakini kwa walio wengi kilio chao kikubwa huwa ni suala
la ukosefu wa ajira. Kwa asilimia kubwa wengi wao ninao kutana nao ni lazima
hugusia tatizo la ajira. Hiki ni kitu ambacho huwa kinaniuma sana kwa kusikia taarifa zile zile, tena mara
kwa mara zikijirudia.
Kuna maswali mengi
ambayo hubaki nikijiuliza tatizo ni nini hasa?kweli ni ajira au tatizo pia lipo
kwa wahitimu wenyewe?Huwa nabaki najiuliza maswali yote hayo baada ya kugundua
kwamba tupo kwenye taifa ambalo bado lina fursa nyingi sana kuzitumia.
Kama fursa hizi zote
zipo nafasi ya vijana waliomaliza vyuo mbalimbali ya kujitengenezea ajira iko
wapi?wengi kweli hukata tamaa na kujikuta wakilala na kusahau kuwa zipo fursa nyingi
sana ambazo wangeweza kuzitumia kuwafanikisha bila wao kujua.
Lakini, unapokuja
kuchunguza kwa makini, chanzo cha vijana wengi kukwama kufikia mafanikio
unakuja kubaini wakati mwingine tatizo linaweza lisiwe ajira bali vipo vizuizi
au mambo yanayomzuia kijana huyu kufikia mafanikio makubwa katika maisha yake.
Ni vizuizi au mambo
hayohayo ambayo natamani kila kijana mwenye uchungu na mafanikio yake
ayajue ili aweze kujikwamua hapo alipo na kuwasaidia wengine. Haina
haja ya kukata tamaa, upo uwezo wa kufanikiwa mkubwa ndani mwako ikiwa
utagundua
mambo yanayokukwamisha kufanikiwa.
Sitaki kuona
ukiendelea kuteseka na kuishi maisha magumu bila sababu wakati kila fursa ya
mafanikio ipo katika hii Nchi. Acha kusingizia sana ajira kuwa ndilo tatizo pekee hasa
linalokukwamisha. Bila kupoteza muda, ni vyema ukayajua mambo yanayomkwamisha kijana
wa kitanzania kufikia mafanikio makubwa,
ili uchukue hatua.
1. Kutafuta mafanikio ya haraka.
Fikra nyingi za
vijana wanaomaliza vyuo mbalimbali huwa zimejikita kwenye kutaka mafanikio ya
haraka. Kwa hakika hili limekuwa tatizo kubwa ambalo kwa bahati mbaya wengi
huwa hawalioni kirahisi, lakini limekuwa likipelekea mipango na malengo yao
mengi kukwama. Kutokana na hili hujikuta wakiwaza njia nyingi za mikato za
kupata pesa ikiwemo hata rushwa na
kusahau kutafuta mafaniko hatua kwa hatua.
Unapokutana na kijana
kama huyu awe amesoma au hujasoma na unapokuja kumwambia kuwa maisha ni hatua
na mipango kiukweli hawezi kukuelewa nini unachoongea. Hili ni moja ya tatizo
kubwa sana
linawakabili vijana wengi wa kitanzania na kupelekea kushindwa kupata mafanikio.
2.
Kukosa mipango na malengo imara.
Kutokana na kukosa
mipango na malengo imara hili limekuwa ni tatizo pia linalopelekea vijana wengi
kushindwa kufanikiwa. Vijana wengi wamekuwa wakiishi kwa kuwa na mipango ya muda
mfupi sana au
hakuna kabisa. Kikubwa kinachowapoteza hapa ni kuangalia kwao mambo ya sasa
ikiwemo starehe za muda mfupi.
Ni muhimu sasa kujua
kwamba mafanikio yanahitaji malengo. Kama ajira kweli hakuna ni kitu gani
kinachofanyika cha mbadala ili kupata kitu cha kukuingizia kipato? Vijana wengi
wamekuwa wakiwaza tu ajira ajira na mwisho wa siku wanajikuta wakikosa kitu cha
kufanya kabisa. Kwa hiyo kukosa malengo ni tatatizo linalowakwamisha vijana
wengi kufikia ndoto zao.
3. Kukosa kujiamini.
Kama upo kwenye
safari ya mafanikio halafu hujiamini, elewa kabisa huwezi kufikia mafanikio
hayo. Mafanikio yoyote yale yanahitaji ujiamini wewe kwanza
kuwa unaweza. Vijana wengi wanakosa kujiamini na matokeo yake hujikuta wakishindwa
kuchukua hatua za kubadili maisha yao.
Na kutokana na tatizo
hili la kutokujiamini hupelekea wao kushindwa kuzitumia fursa zilizopo nchini
kama vile biashara ndogondogo za kujiajiri, kilimo cha kisasa na hata ufugaji
wa kisasa pia. Kitu cha kujiuliza je, ni kweli ajira peke yake ndiyo chanzo cha
kipato? Jibu bila shaka ni hapana. Tatizo kubwa linaloonekana hapa kumkwamisha
kijana huyu wa Kitanzania kufanikiwa ni kutokujiamini kwake.
4. Kukosa mtaji.
Mbali na matatizo
mengine binafsi ambayo yamekuwa yakimkwamisha kijana kufikia mafanikio, lakini
swala la kukosa mitaji pia nalo ni tatizo kubwa sana. Vijana wengi wenye elimu
ya juu na kawaida, wote kwa pamoja kilio ni hikihiki kwamba hakuna mtaji. Ni
kweli wanakuwa wanatamani kufanya bishara fulani, lakini hakuna mtaji wa biashara
hiyo.
Na hili ni jambo
ambalo serikali na wadau wengine wanatakiwa kuliangalia kwa jicho la pili ili
kuwasaidia vijana hawa kuweza kutoka walipo na kujenga taifa imara lenye mafanikio. Lakini si hivyo tu
hata vijana wenyewe wanaweza kuungana ili kupata mitaji na kuanza kuwekeza
kwenye miradi ya kuwafanikisha.
Yapo mambo mengi
ambayo yamekuwa kikwazo cha kumzuia kijana wa kitanzania kufanikiwa. Lakini kwa
leo fanyia kazi kwanza mambo hayo machache ili
yawe msaada kwako.
Post a Comment