0
Uchunguzi wa kina kuhusu ajali ya ndege unaendeshwa na Urusi
Wachunguzi wa ile ndege ya Urusi iliyoanguka nchini Misri, wanasema kuwa watatumia kila mbinu ili kubaini kilichosababisha kuanguka kwa ndege hiyo juma lililopita katika rasi ya Sinai.
Kwa sasa wanachunguza kwa kina sauti ya ndege iliyonaswa na kifaa cha kurekodi sauti, katika sekunde ya mwisho mwisho ya ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu 224.
Lakini kiongozi mkuu wa kundi la wachunguzi, Ayman el Mokadem, amesema kuwa, kikosi chake bado hakijabaini aina ya sauti hiyo au kilichosababisha ajali hiyo.
Amethibitisha kuwa yamkini ndege hiyo ilipasuka msamba ikiwa bado angani.
 
Ayman el Mokadem, amesema kuwa, kikosi chake bado hakijabaini aina ya sauti hiyo au kilichosababisha ajali hiyo
Aidha inadaiwa kuwa data za ndege zinaonyesha kuwa gia ya ndege ilikuwa bado mahali pake hadi ilipoanguka - hii ikiashiria kuwa marubani walikuwa hawajapata tahadhari yoyote kwamba kulikuwa na matatizo yoyote ya injini.
Wakati huohuo Uingereza imetuma ndege tano Misri kuwaondosha raia wake nchini humo.
Taarifa zake za kijasusi zilidai kuwa ndege hiyo ya urusi ilidunguliwa na bomu, lakini kiongozi mkuu wa uchunguzi huko Misri anasema kwamba uchunguzi unaendelea.
Maafisa mjini Moscow, wanasema kuwa itachukua majuma kadhaa kuwahamisha hadi nyumbani zaidi ya watalii themanini wa Urusi kutoka, katika mgahawa wa Sharm-el-Sheikh nchini Misri, mahali ambapo ndege hiyo iliyoanguka ilianzia safari yake.

Post a Comment

 
Top