0


Baada ya miezi kadhaa ya mapigano nchini Burundi, huenda nchi hiyo ikakumbwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, hii ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kushughulikia mizozo, ICG lililoko Brussels.
Vikosi vya usalama vyapiga doria mjini Bujumbura
Shirika la ICG limetoa tahadhari hiyo baada ya mapigano ya makundi yenye silaha na kuongezeka kwa mapigano kuwa Burundi inakabiliwa na tisho la mauwaji ya halaiki na mapiganano ya kikabila.
Shirika hilo limesema kuongezeka kwa mapigano,kuwepo kwa misimamo mikali na kuendelea kuwepo kwa wakimbizi karibu elfu 200,000 kunadhihirisha kuwa migawanyiko imeongezeka huku majadiliano ya kitaifa yakionekana kutozaa matunda yoyote. Umoja wa mataifa pia umeonya kuwa Burundi huenda ikarudi kwenye vita kufuatia kuongezeka kwa mauwaji, kukamatwa na kuzuiliwa kwa watu.
Wakazi wametoroka makwao katika mji mkuu wa Burudi Bujumbura hapo jana baada ya kupata miili minne kwenye mitaa ya jiji hilo hii ikiwa ni sehemu ya msururu wa mauwaji yanayohusishwa na kugombea na kuchaguliwa kwa rais Pierre Nkurunziza kwa mhula wa tatu.
Hatari ya kuzuka mapigano Burundi
Wakimbizi wa Burundi katika kambi ya Nyarugusu Tanzania
Kulingana Philippe Bertoux, mratibu wa Ufaransa anayehusika na maswala ya kisiasa katika Umoja wa mataifa ,Ufaransa imetaka kuwepo kwa mkutano wa dharura wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa. Nayo Uingereza ambayo inashikilia uenyekiti wa baraza la Usalama la Umoja wa mataifa imesema mkutano huo utafanyika Jumatatu.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power amesema nchi yake imesikitishwa na muda uliotolewa na serikali ya Burundi wa siku tano siku Jumatatu kwa maafisa wa usalama kusaka silaha na viongozi wa upinzani akisema hatua hiyo huenda ikazua mapigano kuanzia mwishoni mwa wiki hii.
Vifo vya watu wanne ambao maiti zao zimepatikana mitaani kumefikisha 13 idadi ya watu waliouawa tangu Jumatatu wiki hii.Afisa mkuu wa haki za binadamu wa umoja wa mataifa amesema wanakadiria kuwa zaidi ya watu 198 wameuawa nchini Burundi tangu mwisho wa mwezi Aprili wakati Nkurunziza alitangaza kuwania awamu ya tatu hatua ambayo ilipingwa nchini humo na kimataifa.
Wakimbizi waongezeka
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Mkaazi mmoja aliyejitambulisha kama Marriane alisikika akisema"lazima nitoroke" akiashiriana kuwepo kwa maafisa wa usalama".
Kufanikiwa kwa Nkurunziza kuwania awamu ya tatu kuongoza taifa la Burundi kulizua mzozo na maandamano na pia mapinduzi yaliyoshindwa.Zaidi ya watu elfu mia 200 wametoroka taifa hilo lililoko Afrika ya Kati.
Yamkini wafuasi wa Nkurunzisa na wale wa upinzani wanauwana huku maafisa wa usalama wakishukiwa kuwauwa wanachama wa upinzani.Aliyekuwa mkuu wa ujasusi na mwandani wa karibu wa Nkurunziza ni kati ya wahanga wa mzozo huo lakini wengi wa waliouwa wamekuwa raia wa kawaida wa Burundi ambao miili yao imekuwa ikitupwa mbali na wanakoishi.
Rais Barak Obama wa Marekani amesema wiki iliyopita kuwa Burundi haijafanya juhudi za kutosha kuhakikisha sheria nchini humo na huenda ikaondolewa na Marekani kwenye mkataba wa kibiashara na mataifa ya Afrika.DW

Post a Comment

 
Top