pic 1
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Anna Makinda akiongea na waandishi wa habari kuhusu tamko la kutogombea Uspika Msimu huu hawapo pichani katika mkutano wake  uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
pic 2
Waandishi wa habari wakifatilia kwa makini maelezo anayotoa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Anna Makinda hayupo pichani alipotoa tamko la kutogombea tena Uspika wa Bunge msimu huu.
pic 3
Spika wa bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh. Anna Makinda katikati akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mkutano wake katika ofisi za bunge leo jijini Dar es salaam.(Picha na Ally Daud -Maelezo).
Na Jacquiline Mrisho-MAELEZO-Dar es salaam.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Anne Makinda ametangaza rasmi kutogombea nafasi ya Uspika wa Bunge baada ya kuliongoza Bunge la 10 kwa kipindi cha miaka mitano.
Mhe.Makinda ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam wakati alipokuwa akizingumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam.
 “Kama yalivyo matakwa ya kisheria na demokrasia ya hapa nchini wanasiasa wanatumikia nafasi zao mbalimbali kwa kipindi cha miaka mitano na kisha wanarudi kuomba tena ridhaa kwa wananchi kuongoza”,alisema Mhe.Makinda.
Mheshimiwa Makinda aliongeza kuwa anaona wakati umewadia kwa yeye kuwaachia wengine nao washike wadhifa huo katika  Mhimili huo muhimu wa kusimamia Serikali.
Mbali na hayo Mhe.Makinda aliendelea kusema kuwa ametumikia nafasi mbalimbali katika Siasa kwa kipindi cha miaka 40 ndani ya Bunge, ikiwemo nafasi ya Waziri ,Mwenyekiti wa Bunge,Naibu Spika na Spika  hivyo  kwa sasa ameamua kung’atuka katika masuala ya uongozi.
Hata hivyo Mheshimiwa Spika amewaambia waandishi wa habari kuwa katika kipindi cha uongozi wake, Bunge lilifanyakazi kwa ushirikiano na liliweza kuisimamia Serikali hadi kupelekea baadhi ya Mawaziri kujiuzulu.
Ameongeza kuwa Bunge la 10 lilifanikiwa kubadilisha mfumo wa bajeti kwa kuweka sheria mpya za bajeti ambayo iliongeza nidhamu katika matumizi ya fedha.
Mheshimiwa Makinda amesema kuwa atawakumbuka Waheshimiwa mbalimbali katika bunge aliloliongoza akiwemo Mhe.Tundu Lissu , Mhe.Halima Mdee, Mhe.Felix Mkosamali,Mhe.Moses Machali,Mhe. John Mnyika na wengine ambao alifanya nao kazi kwa kushirikiano