0


Bidii yako ya kuendelea kutimiza malengo yako bado ipo au umevunjika moyo, baada ya kuona mipango yako haiendi kama ulivyo panga. Nikukumbushe kwamba kufikia kilele cha mafanikio, sio rahisi kama ulivyoambiwa au ulivyofikiri.

Lazima ukaze mwendo pale unapojisikia kuchoka, lazima uwe na moyo wa ujasiri kukabiliana na vikwazo mbalimbali unavyokutana navyo njiani.

Mapambano ya kufikia kile unachokitamani sio maneno, ingekuwa maneno yanatimiza kile tunachokihitaji. Kila mtu angekuwa na mafanikio makubwa, kuchukua hatua kwa vitendo, ni njema zaidi kuliko kuongea. Japo ule ukiri wa ulimi, huumba kile ulichokitamka. Ukikiri kufanikiwa halafu ukaongeza bidii kwa kile ulichokiri bila kukata tamaa, utafanikiwa.

Ukikiri kushindwa, na ile taswira ya kushindwa ikaendelea kukaa ndani yako. Hata kama utafanya vizuri, hutaona huo uzuri, zaidi utajiona wewe huwezi baada ya kukumbuka kile unachokiamini ndani yako.

Baada ya salamu, nikualike katika kujifunza faida za mtu anayejisimamia maamuzi yake. Kila mmoja wetu aliumbwa na uwezo wa kuweza kujiendesha yeye mwenyewe, yaani wewe ulivyo upo uwezo wako wa kuamua ufanye hili na usifanye hili.

Ikiwa unazo fahamu za kutambua jema na baya, upo uwezo binafsi wa maamuzi yako.
Unaweza ukachukua maamuzi ambayo kila mmoja atakushangaa. Lakini kama moyoni mwako una amani na hicho ulichoamua kukifanya au kukifuata, kitakuwa sahihi kwako.

Simaanishi kila maamuzi ni sahihi, ila usahihi na kusiko sahihi, kuna letwa na mtazamo wa mtu. Jinsi walivyowahi kuona jambo hilo likifanywa, ndio itawafanya washindwe kumwelewa mtu pale anapoamua kwenda kinyume na matarajio yao.

Ukiachana na sheria za nchi, ukiachana na kanuni za kuishi kiroho zilizowekwa ili umpendeze Mungu. Upo uwezo uliowekwa na Mungu ndani yako, tunapoona na kusikia, hayo yote hutengeneza taswira ya namna ya kuishi.

Mitazamo ya mtu inaweza ikawa jinsi alivyofundishwa na familia ama jamii inayomzunguka. Pamoja na mitazamo hiyo, inaweza isimsaidie kuwa na maamuzi yake binafsi.

Usishangae mtu mzima, mwenye familia na watoto wakubwa. Hawezi kuchukua maamuzi magumu ya kuokoa familia yake au maisha yake, mpaka asikie mtu fulani anasemaje.
Hii imesababisha wengi wetu tumeshindwa kuwa huru katika kujiendesha wenyewe.

Nikukumbushe kwamba, ulipokuwa mtoto, kila kitu kilitegemea mzazi au mlezi wako. Ulipotaka kufanya kitu ulimwangalia baba, mama, kaka, dada, babu, bibi, uone kama upo sahihi ama la! vivyo hivyo ulivyokuwa mwanafunzi ulitegemea usahihi wako wa kufanya vitu utoke kwa mwalimu wako.
Mwalimu anapotoa alama ya vema, alimaanisha umepatia na alipotoa alama ya mkasi, alimaanisha umekosa. Tumeenda na mtindo huu katika maisha, tumejikuta yale mazingira yametutengeneza jinsi yalivyotaka yenyewe.

Lakini tulipokuwa tunapita huko kote, tuliitwa watoto, tukaje utu uzima. Maana yake uwezo wa kufikiri jema na baya unakuwepo sasa.

Huko nyuma ilikuwa lazima tujazwe vitu vingi ili inapofika hatua ya kuitwa mtu mzima, tuwe na uamuzi wetu binafsi. Yaani uwe na uwezo wa kuamua hili nitafanya, na hili sitafanya, wakati zamani ukiwa mtoto ulikuwa huwezi kufanya hivyo.

Sasa ule mfumo wa kuamuliwa tuishi vipi, umetuingia kwenye fahamu zetu. Umetufanya akili zetu asilimia kubwa zimekuwa na mitizamo hasi.

Wakati sasa tulipaswa kuwa na maamuzi ya kufanya kile chenye manufaa kwetu. Tunashindwa kutokana na msongo wa mazingira, unajua kabisa hapa nilipo sio sahihi ila unaogopa kuchukua hatua ya kutoka. Ili kulinda heshima ya wazazi au walezi.

Hii imepelekea wengi wetu kuishi kwenye vifungo vya nafsi. Unajua kabisa upo kwenye mahusiano ya uchumba yasiyo sahihi. Lakini unaendelea kung'ang'ania, kisa umeambiwa na mzazi wako huyo anakufaa. Unajua unachosoma hakipo kabisa ndani ya moyo wako, lakini unaogopa kukataa kwa sababu anayekusomesha anataka usome anavyotaka yeye.

Tufanye nini sasa ili tuwe na uwezo wa kuchukua maamuzi yetu binafsi?
Lazima utafute kujijua wewe ni nani, una thamani gani, je unapenda kuwa ulivyo ama mazingira yanakulazimisha uwe hivyo ulivyo.

Ukishaanza kufikia hatua hii, ya kujiuliza maswali ya namna hii, maana yake umeanza kujitambua wewe ni nani. Baada ya hapo anza kutafuta kweli ya kile unachokitaka, haijalishi uliambiwa hii usijifunze. Jiulize kwa nini, hata pasipo kutumia nguvu ya wewe kutaka kujua utashangaa unapata ufumbuzi.

Kingine unachotakiwa kufanya ni kusoma na  kusikiliza sana mawazo ya wengine. Hapa kama ni mchanga wa kumeza vitu, nakushauri utafute kwanza wale unaowaamini. Mwanzoni utapata maumivu makali sana ya kuambiwa ukweli na kuusikia. Lakini baada ya muda fulani, utakuwa umekomaa na kutoka kwenye utumwa wa fikra.

Hapo ndipo utakuwa na ujasiri wa kuchukua maamuzi yako binafsi. Usifikiri wale waliochukua maamuzi yao, watu wakawashangaa na kuwasema vibaya kuwa wamekosea. Lakini wao hawakujali, baada ya muda fulani watu hao hao waliowasema vibaya wanaanza kuwapongeza kwa uamuzi wao.
Unafikiri ni kwa nini? kile kilicho ndani yako, na kinachokuletea msukumo wa kufanya kitu sahihi cha kuleta furaha ya maisha yako, halafu kikawa hakimkosei Mungu, ndicho unachotakiwa kukifanya pasipo kuangalia idadi ya watu wanaokuunga mkono.

Post a Comment

 
Top