Mwaka jana kuliandaliwa semina kwa njia ya mtandao ambapo
tulitoa elimu ya jinsi ya kutengeneza kipato kwenye mtandao kwa kutumia blog.
Baadae tulitoa kitabu ambacho kiliendelea kutoa elimu hii ya kumwezesha mtu
yeyote kutengeneza biashara yake kupitia mtandao kwa kuw ana blog ambayo inatoa
elimu fulani watu wanayohitaji.
Watu wengi wamejipatia kitabu hiki na wengi wamefungua
blog zao ambazo sasa zimeshaanza kupata wasomaji ambao wanazifuatilia kwa
makini. Unaweza kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu
Ili uweze kutengeneza fedha kwenye mtandao kwa kutumia
blog kwanza itakuhitaji muda wa kuanza kujenga wasomaji wanaokuamini,
itakuhitaji wewe ujifunze sana na ujiweke kama mtaalamu kwenye lile eneo ambalo
umechagua kuandikia na kutoa elimu kwa watu wengine. Pia utahitaji kuwa na
kompyuta ili uiendeshe blog yako kitaalamu zaidi. Sasa mahitaji haya yanaweza
kuwa kikwazo kwa watu wengi ambao wanataka kutengeneza kipato kupitia mtandao.
Leo nakushirikisha njia nyingine ya kutengeneza kipato
kwenye mtandao kwa kutumia mitandao ya kijamii. Wote tunajua kwamba dunia ya
sasa karibu kila mtu yupo kwenye mtandao wa kijamii. Kuna mitandao ya kijamii
ambayo ni maarufu na watu wengi wanaitumia, hata wewe pia unaitumia. Sasa leo
nataka nikupe ujanja wa jinsi unaweza kuitumia mitandao hiyo kutengeneza kipato
ili uweze kubadili hali yako ya kipato.
Ni mitandao ipi
ina watumiaji wengi kwa hapa Tanzania?
Kwa Tanzania kuna baadhi ya mitandao ya kijamii ambayo
ina watumiaji wengi sana. Kwanza kabisa ni mtandao wa kijamii unaoitwa
facebook, huu ndio unaongoza duniani na hata hapa tanzania umejizolea watumiaji
wengi sana. Karibu kila mtu anayetumia mitandao ya kijamii yupo facebook.
Mtandao mwingine wenye watumiaji wengi ni instagram. Huu
ni mtandao ambao umechipukia kwa kasi sana hapa tanzania na umepata umaarufu
mkubwa na watu wengi kuufuatilia. Ni mtandao ambao ni rahisi sana kutumia na
kule watu wanaweka picha tu na maelezo.
Twitter nao pia ni mtandao wa kijamii ambao watanzania
wengi wanatumia, ila waliomiliki sana mtandao huu ni watu maarufu kwenye jamii
kama viongozi au wasanii. Twitter sio mtandao ambao unavutia wengi kuwepo kwa
sababu unahitaji kuweza kutoa ujumbe kwa maneno machache sana na hivyo hii ni
changamoto kwa wengi.
Linkedin pia ni mtandao wa kijamii ambao umekaa kitaaluma
na kitaalamu zaidi. Kupitia linkedin mtu anaweza kuweka wasifu wake na nafasi
anazoweza kufanyia kazi na ikawa rahisi wenye uhitaji kumfikia. Ni mtandao
ambao haujakaa kiumbea umbea kama mingine na hivyo hauna watumiaji wengi kutoka
Tanzania.
Kwa madhumuni ya makala hii nitajadili mitandao miwili
ambayo watanzania wengi wanaitumia ambayo ni facebook na instagram.
Je inawezekana
kutengeneza fedha kwa kupitia mitandao ya kijamii?
Watu ambao wana marafiki au wafuasi wengi kwenye mitandao
hii ya kijamii wamekuwa wanatengeneza fedha kupitia mitandao hii. Watu hawa
hufanya kazi na makampuni yanayohitaji kujitangaza na makampuni hayo kuweka
matangazo kwenye kurasa zao kwenye mitandao hii na hivyo wao kutengeneza
kipato. Na ili kuhakikisha wanaendelea kutengeneza kipato wanatafuta njia bora
za kukutumia wewe.
Wanachotaka ni wewe uwe na hamasa ya kuwafuatilia na
ukifika pale unakutana na matangazo mbalimbali. Watu hawa wenye wafuasi wengi wamekuwa
wakitengeneza ugomvi usio na maana ili tu kuwafanya watu wengi wawafuatilie na
hivyo wao kukuza biashara zao za kuuza matangazo.
Makampuni mengi yamekuwa yakitafuta njia nzuri ya
kutangaza biashara zao kupitia mitandao hii ya kijamii na njia kubwa wanayoiona
ni nzuri ni kutumia watu wenye wafuasi wengi.
Wewe unawezaje kutengeneza kipato kupitia mitandao hii?
Swali zuri sana, na hapa ndio ninataka nikupe maarifa
ambayo yatabadili maisha yako kama utayatumia. Tumeshaona mitandao ya kijamii
inayotumika sana kwa tanzania na pia tumeshaona kwamba inawezekana kutengeneza
fedha kwenye mitandao hii ya kijamii kama ambavyo tayari kuna watu
wanaotengeneza fedha kupitia mitandao hii.
Sasa je wewe unawezaje kutengeneza fedha pia? Kumbuka
labda wewe sio mtu maarufu hivyo una wafuasi au marafiki wachache. Na makampuni
mengi yanayotaka kutangaza kupitia mitandao hii wanataka watu wenye wafuasi
wengi.
Hapa ndio wakati wa kutumia akili yako vizuri na ukiweza
kufanya hivi utatengeneza kipato kikubwa mpaka mwenyewe utashangaa ulikuwa wapi
hukujua hilo mapema. Hivyo twende pamoja na fanyia kazi yale ambayo unajifunza
hapa.
Tuseme wewe ni kijana ambayo huna kazi ila una simu yenye
uwezo wa kuingia kwenye mitandao hii. Kama umeshatumia mitandao hii kwa muda
umeshajijengea marafiki na wafuasi kadhaa kupitia mitandao hii. Lakini siku
zote umekuwa unaingia kwenye mitandao hii na kutoka bila ya kutengeneza kipato
chochote.
Sasa leo nataka uwe na mpango tofauti. Kama tulivyoona
hapo juu ni kwamba makampuni mengi yanakimbilia kutangaza kupitia watu wenye
wafuasi wengi. Makampuni haya yanata fedha nyingi kwa muda mfupi na tangazo lao
linakaa muda mfupi pia. Wewe njoo na mpango wa kuyasaidia makampuni haya
kujenga wafuasi wengi kupitia mitandao hii ya kijamii.
Badala ya makampuni haya kulipa ada kubwa ya matangazo
mara moja, kwa nini yasitengeneze wafuasi wake wenyewe ambao wataendelea
kuwatangazia bure kila siku? Hiki ni kitu ambacho makampuni mengi hayaelewi na
unahitaji kuwaelewesha na kuwapa mpango wako wewe.
Mpango wako unakuwa ni kuyasaidia makampuni kuendesha
kurasa zao kwenye mitandao hii ya kijamii. Unayasaidia makampuni haya kupata
wafuasi wengi, unatoa taarifa muhimu za makampuni hayo, unaendesha mashindano
madogo madogo, vyote hivi vinaisaidia kampuni kupata wafuasi na kuwatangazia,
huku wewe ukitengeneza kipato.
Kwa kifupi
unahitaji kuwa na mpango huu;
1. Kuwa na mpango w akuweza kuisaidia kampuni kuongeza
wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii. Unaweza kuanza na mitandao miwili
yenye watumiaji wengi Tanzania, ambayo ni facebook na instagram.
2. Weka ada ndogo kwa kila siku ambayo kampuni unayofanya
nayo kazi itakulipa. Hakikisha ni ada ndogo kiasi kwamba kampuni unayofanya
nayo kazi haioni kama inapoteza fedha.
3. Toa mpango huu kwa makampuni mengi, kila kampuni
unayoijua na ambayo huwa inatangaza kwenye mitandao hii wape mpango wako huo.
Na hata kama kuna kampuni haijajua kutangaza kupitia mitandao hii ni wakati
mzuri wa kuwajulisha hilo. Unapotoa mpango wako kwa makampuni mengi, kuna
machache ambayo yatakubali.
4. Fanya kazi vizuri sana na makampuni haya na hii ndio
itakuwa wasifu wako wakati unaendelea kuomba kufanya kazi hii na makampuni
mengine. Kama utaweza kuonesha kwamba umeyasaidia makampuni mengine kukuza
wafuasi na kutangaza kwa wengi kupitia mitandao hiyo, itakuwa rahisi kwa
makampuni mengi kutaka kufanya kazi na wewe.
Unahitaji kutengeneza mpango bora ambao utatoa thamani
kubwa kwa kampuni yoyote ambayo itakuamini wewe. Mambo hayo manne hapo juu ni
muhimu kuyazingatia.
Mambo
yatakayokuzuia kufanyia kazi hiki ulichojifunza leo;
Kuna baadhi ya mambo ambayo yatakuzuia kufanyia kazi hiki
nilichokushirikisha hapa leo. naomba niyaweke wazi hapa ili unaposhindwa ujue
umeamua mwenyewe.
1. Hupo tayari kufanya kazi kwa bidii na maarifa,
kufikiri zaidi, kuwa mbunifu na kuongeza thamani kwenye biashara za wengine.
2. Unaogopa kutoa mapendekezo kwa kampuni usiyomjua mtu
kwa sababu watakataa. Au utaongea na makampuni machache na yatakataa. Sasa kama
unaogopa kwa sababu yatakataa, mpaka sasa ambapo hujatoa mapendekezo wamekataa,
kwa nini usitumie mbinu nzuri kuwashawishi? Halafu ukiongea na makampuni kumi
yakakataa ni kitu cha kawaida. Nitafute utakapokuwa umeongea na makampuni 100
na yote yakakataa, nitakupa mbinu za tofauti.
3. Uko tayari kushabikia timu nani na timu nani ila hupo
tayari kutumia mitandao hii kwa faida yako na ya wengine. Sijui wewe kuwa
kwenye timu ya mtu ambayo hata haiendi uwanjani unalipwa kiasi gani, unahitaji
kuachana na huu ujinga na ufikirie kutengeneza kipato.
4. Uko tayari kuendelea kuona wivu kwenye maisha ya
kuigiza kuliko kufikiria ni kipi ufanye ili kutengeneza fedha kwenye mitandao
hii ya kijamii. Umekuwa unaona watu wanavaa vizuri kuliko wewe, wanaonekana
kuwa kwenye ofisi nzuri kuliko wewe, wamepiga picha wakiwa wanacheka na
kufurahi, wakiwa wanakula vyakula vizuri, wakiwa wapo kwenye sehemu nzuri za
mapumziko. Na huenda kwa kuona wengine kwenye picha hizi unaona wewe ndio
hujielewi. Sasa achana na mambo hayo ya kuonea wivu kwa sababu sehemu kubwa ya
mambo unayoona kwenye mitandao ya kijamii ni maigizo. Au angalau watu
hawakuoneshi wakiwa wanapitia matatizo yao binafsi, wakiwa wanakazana kupata
fedha, wakiwa wanapambana na ugumu wa maisha. Wewe fikiria jinsi ya kuweza kuongeza
thamani kwa wengine kupitia mitandao hii.

Post a Comment