0
BILIONEA Moise Katumbi leo atatarajia marejesho fulani ya uwekezaji wake mkubwa katika klabu ya Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakati michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakapofikia kilele chake.
Mazembe wanaikaribisha USM Alger kuanzia Saa 9.30 kwa Saa za DRC sawa na Saa 10:30 kwa Saa za Afrika Afrika Mashariki na mchezo huo utaonyeshwa katika chaneli ya SuperSport9.
Mtoto huyo mzaliwa wa mama Mkongo na baba Myahudi, mwanasiasa na mfanyaiashara ‘mwenye pesha’ za kuonekana kutokana na biashara ya madini ya shaba mjini Lubumbashi ametengeneza kikosi cha ‘Nyota wa Afrika’.
Mazembe ilishinda 2-1 nyumbani kwa USM Alger, Algeria Jumapili iliyopita katika fainali ya kwanza na kwenye kikosi chake cha kwanza kulikuwa kuna Wamali watatu na wachezaji wawili wawili kutoka kila nchi, DRC, Ghana, Tanzania na Zambia.
"Nyota wa Afrika" Kikosi cha TP Mazembe chenye wachezaji kutoka mataifa tofauti

“Lengo letu ni kuwapa nafasi wachezaji wenye vipaji vikubwa Afrika," anasema baba wa umri wa miaka 50, Katumbi kuelekea mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Mazembe wenye kumeza watu 18,000.
“Lengo kubwa la klabu mwaka huu lilikuwa kushinda taji la Ligi ya Mabingwa kwa mara ya tano. Nina furaha sana Lubumbashi, kwa sababu tunachukuliwa kifalme,"anasema kiungo Mghana, Daniel Nii Adjei, ambaye alitokea benchi kwenye mchezo wa kwanza mjini Algiers.
Baada ya ushindi mzuri wa ugenini mjini Algiers, ‘The Ravens’ yaani Kunguru wanatarajiwa kutwaa taji kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010, walipoifunga Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 6-1. 
Mazembe pia ilitwaa taji hilo kubwa Afrika mwaka uliotangulia na inakuwa klabu ya kwanza ya ukanda wa Sahara kufikia mafanikio hayo tangu mwaka 2004.
Timu za Afrika Kaskazini zimekuwa zikitawala katika Ligi ya Mabingwa Afrika zikitwaa mataji nane kati ya 10 yaliyopita yakienda Misri au Tunisia. 
Lakini Mazembe imeendelea kuwa mshindani mzuri kwa kuweza kufika Nusu Fainali mara mbili tangu watwae taji la mwisho.
Hakuna mwenye ‘njaa’ ya mafaniko hayo leo kumzidi kocha Mfaransa, Patrice Carteron, baada ya kuyakosakosa mataji kadhaa ya Afrika. 
Baada ya kujiuzulu ukocha wa Mali, aliambulia Medali ya Fedha za ushindi wa pili wa michuano ya Kombe la Shirikisho la CAF mbele ya CS Sfaxien mwaka 2013 baada ya kuruhusu bao la dakika ya mwisho katika mchezo wa marudiano DRC.
Mwaka jana, Mazembe ilitarajiwa kuipiku Entente Setif ya Algeria katika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa, lakini makosa ya kipa mkongwe, Muteba Kidiaba yaliigharimu timu.
“USM ni hatari kwa sababu hawana cha kupoteza,” ameonya kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 na beki wa zamani wa Lyon na Saint-Etienne, Carteron.
“Kushinda nchini Algeria yalikuwa mafanikio mazuri. Timu iliandaliwa vizuri kisaikolojia na walionyesha nia na dhamira. Lazima tutumie nguvu zetu za kushambulia kupata ushindi mwingine. Ni namna pekee tunayojua kuicheza,”amesema.
Mazembe imekuwa na rekodi nzuri nyumbani hivi karibuni ikizitandika Moghreb Tetouan ya Morocco 5-0 kwenda Nusu Fainali kisha kuibamiza El Merreikh ya Sudan 3-0 kufika Fainali. Mabao manne katika mechi hizo yamefungwa na ‘Mfalme’ wa Tanzania na Lubumbashi kwa sasa, Mbwana Ally Samatta, ambaye anahitaji mawili zaidi kumpiku Bakry 'Al Medina' Babiker wa Merreikh anayeongoza.
USM wanaoingia fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza inatarajia kupata ushindi wa ugenini wa 2-1 Lubumbashi kama ilivyofanya kwa El Hilal ya Sudan katika Nusu Fainali ili bingwa wa Afrika mwaka huu akapatikane kwa mikwaju ya penalti.
Lakini kipa Mohamed Zemmamouche, ambaye uhodari wake uliinusuru timu hiyo kufungwa mabao zaidi mjini Algiers, anakubali kwamba “Mambo ni magumu”.
Viungo Rainford Kalaba wa Mazembe na Hocine El Orfi wa USM, wote walitolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo wa kwanza, hivyo wataukosa mchezo wa leo sawa na Nahodha wa USM, Nacereddine Khoualed anayetumikia adhabu pia.
Ikumbukwe bingwa wa taji hilo atazawadiwa dola za Kimarekani Milioni 1.5, mshindi wa pili dola Milioni 1, wakati timu zote zilizoishia Nusu Fainali zinapata dola 700,000 kila moja.
Washindi wa tatu katika makundi wanapata dola 500,000 wakati wanaoshika mkia kwenye makundi wanapata dola 400,000.
Taji la Ligi ya Mabingwa Afrika limeachwa wazi na ES Setif ya Algeria ambayo ililitwaa mwaka jana kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya sare ya jumla ya 3-3 na AS Vita ya Kinshasa, DRC, ikitoa sare ya 1-1 nyumbani na 2-2 Uwanja wa Tata Raphael mjini Kinshasa.
Je, Mazembe itawalipia kisasi mahasimu wao, Vita kwa kuwaadhibu tena Waalgeria na kubakiza mwali wa Ligi ya Mabingwa DRC? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona. 
HADI sasa, Mbwana Ally Samatta na Mtanzania mwenzake anayecheza naye TP Mazembe wanajivunia rekodi mpya waliyoweka, kuwa Watanzania wa kwanza kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Na Samatta anajivunia pia rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao katika Ligi ya Mabingwa Afrika- baada ya kufunga bao la pili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya USM Alger katika fainali ya kwanza Jumapili iliyopita mjini Algiers.
Awali, Samatta na Ulimwengu walivbunja rekodi mbili zilizowekwa na klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam mwaka 1974 na 1993.
1974 Simba SC iliweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, walipotolewa na Mehalla El Kubra ya Misri kwa penalti 3-0 baada ya sare ya jumla ya 1-1, kufuatia kila timu kushinda 1-0 nyumbani kwake.
Ni mechi ambayo Simba SC walirejea na malalamiko kwamba kipa wao, Athumani Mambosasa (sasa marehemu) alifanyiwa fujo, wakati wa upigwaji wa penalti ikiwemo kutishiwa bastola.
Mwaka 1993 Simba SC iliweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza fainali ya Kikombe cha kwa Afrika kwa ujumla na Kombe la CAF, ambalo sasa limekuwa Kombe la Shirikisho baada ya kuunganishwa na lililokuwa Kombe la Washindi.  
Simba SC ilianza vizuri kwa kulazimisha sare ya 0-0 mjini Abidjan, Ivory Coast Novemba 12 dhidi ya Stella kabla ya kufungwa 2-0 mjini Dar es Salaam Novemba 26 mwaka huo.
Samatta na Ulimwengu mwaka 2013 walivunja rekodi ya Simba SC kucheza fainali ya Kombe la CAF walipoichezea Mazembe katika fainali ya Kombe hilo, wakifungwa 2-0 Novemba 23 na CS Sfaxien nchini Tunisia kabla ya kushinda 2-1 Novemba 30 mjini Lubumbashi, Samatta akifunga bao la pili dakika ya 24.
Na msimu huo, Samatta akawa mfungaji bora baada ya kufungana kwa mabao na raia wa Ibvory Coast, Vincent Die Foneye aliyekuwa anachezea ENPPI ya Misri, kila mmoja akifunga mabao sita.
Mwaka jana, 2014; Samatta na Ulimwengu wakavunja rekodi ya Simba SC kucheza Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichezea Mazembe katika hatua hiyo mechi ya kwanza wakifungwa 2-1 Septemba 20 na ES Setif nchini Algeria na marudiano wakashinda 3-2 hivyo Setif kutwaa taji kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya sare ya jumla ya 4-4.
Jumapili iliyopita Samatta na Ulimwengu wakaandika rekodi mpya ya kuwa Watanzania wa kwanza kucheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa, huku Mbwana pia akiweka rekodi binafsi ya kufunga bao katika mechi hiyo Algiers.
Leo, Mazembe wakiikaribisha USM Alger na mtaji wao wa ushindi wa 2-1 ugenini, Samatta na Ulimwengu wanawania kuwa Watanzania wa kwanza kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Lakini pia Mbwana anawania kuwa Mtanzania wa pili kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo, baada ya Mrisho Ngassa aliyekuwa Yanga SC mwaka jana, kabla ya kuhamia Free State Stars ya mwaka huu. 
Ngassa alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa kufunga mabao sita akifungana na El Hedi Belameiri wa Setif, Haythem Jouini wa Esperance na Ndombe Mubele aliyekuwa AS Vita ya DRC, sasa Al Ahly.
Hadi sasa Samatta ana mabao sita, akizidiwa moja na Sudan Bakri Al-Madina wa El-Merreikh ya Sudan. Samatta analingana na Morocco Mouhcine Iajour wa Moghreb Tetouan ya Morocco, wakati Muivory Coast wa Mazembe pia, Roger Assale mwenye mabao matano hatacheza leo, akitumikia adhabu ya kazi nyekundu aliyopewa Algiers.
Je, Mbwana Ally Samatta atavunja rekodi ya Ngassa leo? Bila shaka hizo ndizo dua za Watanzania kwa vijana wao hao leo.

Post a Comment

 
Top