MABINGWA
wa Kandanda Tanzania bara, Young Africans wanatarajia kuanza mazoezi ya
ufukweni mwishoni mwa juma hili ikiwa ni maandalizi ya kombe la Kagame
linalotarajia kuanza Julai 11 mwaka huu jijini Dar es salaam.
Mkuu
wa kitengo cha habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro amesema
kwamba kikosi chao kinaendelea na mazoezi uwanja wa Karume tangu
mwanzoni mwa wiki hii chini ya kocha, Hans van der Pluijm, lakini bado
wachezaji wengi wapo na timu zao za Taifa wakicheza mechi muhimu za
kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika, AFCON 2017.
Hata
hivyo, Muro amezungumzia suala la wachezaji wa Kigeni ambapo
amebainisha kwamba wameshawapata, lakini wanashindwa kuwasainisha
kwasasa kwani bado mapendekezo ya kuongezea idadi ya wachezaji wa kigeni
hayajajibiwa na TFF.
"Wachezaji
wengi tuliozungumza nao wanaonekana kuipenda Yanga na wanatamani kuja
Yanga, tunasubiri majibu ya mapendekezo yaliyotumwa na klabu TFF kuomba
kuongezewa idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka watano mpaka angalau 10. Kwasasa tuna wachezaji watano wa kigeni, tunapata kigugumizi tumuache nani".
Pia Muro amesema safari hii wanaangalia wachezaji kutoka mataifa yaliyopiga hatua kisoka na ikiwezekana watakwenda mpaka ulaya.
"Tumetoa
kipaumbele kwenye mataifa yale ambayo yanaonekana yamekaa vizuri
kisoka, tunaangalia Zimbabwe, Afrika Magharibi, Afrika kaskazini,
ikiwezekana tutaangalia na Ulaya pia kwasababu nia tunayo, sababu tunayo
na uwezo tunao. Hatushindwi kufanya hivyo pale ambapo maelekezo ya
benchi la ufundi yatataka tufanye hivyo".

Post a Comment