Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes', Sredojevic Milutin
‘Micho’, amesema bado ana imani kubwa na timu yake kuibuka na ushindi
dhidi ya Taifa Stars, mchezo utakapoigwa usiku wa leo katika dimba la
Amaan visiwani Zanzibar.
"Kucheza
ugenini sio sawa na unapokuwa nyumbani. Mara nyingi mnakuwa na msukumo
mkubwa sana kutoka kwa timu pinzani kutokana na kuwa na sapoti kubwa
kutoka kwa mashabiki wao hasa ukizingatia wao wapo nyumbani. Lakini yote
kwa yote nina uhakika wachezaji wangu watarudi nyumbani wakiwa na uso
wa bashasha na tabasamu”, Micho, ambaye pia aliing'oa Tanzania katika
hatua kama hii ya kufuzu CHAN alitanabaisha.
Mserbia
huyo amewajumuisha wachezaji watano wenye asili halisi ya ushambuliaji
katika kikosi cha wachezaji 18 ambacho tayari kipo Zanzibar tayari kwa
pambano hilo. Taarifa zilizopo ni kwamba Micho atatumia mfumo wa
kushambulia zaidi huku pande zote akitumia winga wenye asili ya
ushambuliaji wa kati.
Hassan
Wasswa Mawanda, nahodha wa timu hiyo ana uwezekano mkubwa wa
kuchezeshwa kama beki wa kati huku akishirikiana bega kwa bega na ama
Derrick Tekkwo au Kezironi Kizito katika eneo hilo nyeti kabisa.
Mshambulizi
mwandamizi, Robert Sentongo ataongoza safu ya ushambuliaji ya 'The
Cranes' huku nahodha msaidizi, Farouk Miya akisimama kama namba tisa
vilevile Yasser Mugerwa au Muzamiru Mutyaba akisambaza sumu eneo la
kiungo.
Mchezo
wa marudiano kati ya mahasimu hawa wawili utapigwa wiki mbili zijazo
katika dimba la Nelson Mandela, Namboole jijini Kampala
Mshindi
atakayepatikana kati ya timu hizi, atavaana na ama Sudan au Kenya kabla
ya kuelekea nchini Rwanda ambapo michuano hii ya CHAN mwaka huu ndipo
itakapofanyika.
Michauno ya CHAN ni michuano ya mataifa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani za nchi zao.

Post a Comment