Kahama. Uwepo wa machimbo mengi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu eneo la Bulyanhulu lenye kata za Luguya, Bulyanhulu na Bugalama wilayani hapa, imedaiwa kuwa moja ya sababu inayochangia watoto wengi kukatisha masomo hasa wasichana.
Imeelezwa kuwa wasichana hao hujikuta wakipata
mimba za utotoni na wavulana kujiingiza kwenye shughuli za uchimbaji wa
madini ya dhahabu.
Akitoa taarifa kwa Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya
ya Kahama, Julius Chagama, Zabron Donge alisema sababu hiyo imechangia
kuongezeka kwa watoto wanaokatisha masomo kila kukicha wilayani humo.
Donge alisema ili kukabiliana na hali hiyo,
Serikali imeweka mikakati mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa elimu
ikiwamo wa Mgodi wa Bulyanhulu ili kuhakikisha watoto wanamaliza shule
na wazazi wanapewa elimu.
Pia, alisema licha ya mikakati iliyowekwa na
halmashauri kwa kushirikiana na Mgodi wa Bulyanhulu, kuna mashirika
yasiyokuwa ya kiserikali yanayojihusisha na ulinzi wa mtoto hufanya kazi
ya kuwarejesha shuleni wasichana waliojifungua katika umri mdogo.
Watoto hao hujiunga na masomo ya Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Walioikosa (Memkwa).
Ofisa Mawasiliano wa Mgodi wa Bulyanhulu, Mary
Lupamba alisema mwaka huu pia wamewalipia ada wanafunzi 40 wanaosoma
kwenye shule sita za sekondari ambao walifanya vizuri katika masomo ya
sayansi na hisabati.
Lupamba alisema ili kuhakikisha watoto wanaoishi
katika mazingira hatarishi wanafaidika na elimu, watumishi wa Kampuni ya
Acacia kutoka ofisi za Kahama na Dar es Salaam wana mpango wa kudumu wa
kuwasomesha masomo ya sekondari.
Alisema wanaonufaika na mpango huo ni wale wanaoishi jirani na mgodi huo. Alisema mpaka sasa umewanufaisha wanafunzi 900.
Naye Kaimu Katibu Tawala, Chagama alisema viongozi
kuanzia ngazi ya kijiji, kata na wilaya wanajukumu la kuishirikisha
jamii katika kusimamia masuala ya elimu kwa watoto wao badala ya
kupuuza.
Alisema kama jamii itaelewa umuhimu wa elimu, suala la kukatisha masomo litatoweka.CHANZO:MWANANCHI
Post a Comment