0

Na mwaandishi Wetu 
MILA na desturi za Jando na unyago zinazofundishwa kwa vijana katika mikoa ya Lindi na Mtwara zimetajwa kuwa ni sababu moja wapo ya kuwepo kwa mimba za utotoni pamoja na maambukizi ya ukimwi kwa vijana kwenye mikoa hiyo.
Hayo yalielezwa jana na katibu wa shirika lisilo la kiserikai la maendeleo Masasi (MADA) Bernedetha Jumla alipokuwa akizungumza na kikundi cha vijana cha juhudi kilichopo katika kijiji cha Sululu Halmashauri ya mji Masasi mkoani humo.
Alisema kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali ya GIZ,EVERPLAN,DSW,yalifanya utafiti katika wilaya za mikoa hiyo ikiwemo ya Masasi na kwamba matokea ya utafiti huo yalibaini kuwa  baadhi ya changamoto zilizopo ikiwemo mimba za utotoni pamoja na maabukizi ya ukwimi zinasababishwa na mila na desturi zinazofundishwa kwa vijana katika jando na unyago.
Katibu huyo alisema kufuatia matokea hayo ya utafiti ilipelekea shirika la MADA liliamua kubuni mradi wa afya ya uzazi na jinsia kwa vijana lengo la mradi huo ni kuwafanya vijana wabadili tabia zao ikiwemo ngono uzembe ambazo uchangia mimba za utotoni pamoja na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.
Alisema vijana waliohusishwa katika mradi huo ni wenye umri wa miaka 14 hadi 24 na kwamba mradi huo ni wa miezi sita na unafadhiliwa na mashirika ya DSW,EVERPLAN na GIZ kutoka Ujerumani, hivyo hatua ya kwanza ambayo imefanyika ni mafunzi ya kuwajengea uwezo viongozi wa shirika hilo ili weweze kutekeleza mradi huo kwa ufanisi zaidi.
                        
Jumla alisema pia wamehamasisha vijana juu ya uanzishwaji wa vituo vya klabu za vijana katika Halmashauri mbili ya mji Masasi na Halmshauri ya wilaya ya Masasi na kwa sasa tayari wameshaunda klabu mbili zenye vijana 25 kila moja  katika ngazi ya kata na kijiji kwenye kila Halmashauri.    
Alisema kwa sasa wameanza na vikundi viwili ambapo ni kikundi cha Juhudi kilichopo kijiji cha Sululu Halmashauri mji Masasi na Kazi moja kijiji cha Mihima Halmashauri ya wilaya Masasi,juhudi wanajishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji huku Kazi wao wanajishughulisha na ufugaji wa nyuki,kuku na masuala ya kisanii.
“Tutahamasisha Halmashauri za mji na wilaya ya Masasi ziingize mpango kazi wa elimu ya afya ya uzazi na jinsia kwa vijana na zipangiwe bajeti ili AZISE zitekeleze kila mwaka mipango hiyo,”alisema Jumla
Aliongeza kuwa bado mwamko wa vijana kujitolea kushiriki katika shughuli za kimaendeleo ni mdogo hivyo wanahitaji kuelimishwa zaidi aidha uwelewa wa elimu ya afya ya uzazi na jinsia kwa vijana ikiwemo na uhamasishaji pia unahitajika katika jamii.
Katibu huyo alieleza kwamba pia kuna tatizo la wanawake kutoshirikishwa katika kutoa maamuzi kwenye masuala ya matumizi ya fedha katika kaya zao hali inayochangia kumrudisha nyuma mwanamke katika kujiletea maendeleo.

Post a Comment

 
Top