Mkamuzi yalikuwa siyo ya kitoto kama unavyoona kwenye picha
Watu wakiserebuka mwanzo mwisho
Leo Mkanyia Ang'aa katika Tamasha la DoaDoa
Baada ya ziara ya mafanikio katika jiji la maraha la Nairobi, kundi zima
la Swahili Blues Band chini ya uongozi wa Leo Mkanyia walielekea mjini
Jinja Uganda kushiriki katika Tamasha la muziki la DoaDoa.
Tamasha la DoaDoa ni maalumu kwa wanamuziki kutoka Afrika ya Mashariki
kushiriki na kutambulishwa kwenye jukwaa la kimataifa. DoaDoa wanatoa
fursa mahsusi kwa wasanii hao kuonyesha kazi zao kwa wadau mbalimbali wa
kimataifa wa muziki pamoja na wapenzi kutoka nchi husika.
Baadhi wa wadau wakimataifa walioshiriki ni pamoja na wawakilishi kutoka
Songlines Magazine(UK), Sheer Publishing(Ethiopia), Visa for
Music(Morocco), Selam festival(Ethiopia/Senegal), Sarakasi
Trust(Uholanzi), Sound Diplomacy(UK) na ONGEA(Australia/Kenya).
Vikundi vilivyo shiriki vilijumuisha pamoja na Leo Mkanyia and Swahili
Blues Band, Nandujja(Uganda), Abeneko(Tanzania), Octave Band(Kenya),
Strong Voice Band(Rwanda), Jemimah Sanyu(Uganda), Idi Masaba(Uganda),
H_Art the Band(Kenya), Moutcho(Burundi) na Makadem(Kenya).
Tamasha hilo lilifanyika kati ya tarehe 6 hadi 9 May 2015 na Swahili
Blues Band walipanda jukwaani siku ya Ijumaa ya tarehe 8 majira ya saa
nne kamili usiku.
Walirusha karata yao ya kwanza kabisa kupitia kibao chao maarufu
kinachojulikana kama "Afrika". Afrika inayopigwa katika mirindimo
mahsusi ya Blues, ina mashairi yaliyojaa dhana ya kizalendo na
kimapinduzi. Katika wimbo huu Leo aliyepiga gitaa na kuongoza uimbaji,
alihamasisha hadhara yote kuwa bara la Afrika siyo bara la migongano na
migogoro wala vita bali ni bara la amani lililoshereheshwa na ngoma
pamoja na muziki. Wadau waliohudhuria walikunwa vilivyo pale Leo
alipowahamasisha wadau kusema Hapana kwa Boko Haram na Al Shabaab.
Baada ya wimbo huo uliomithiri ya hotuba kutoka kwa mwanadiplomasia
aliyebobea, Leo aliamua kuwarudisha wapenzi wote katika vitongoji vya
Jiji la Dar es Salaam pale aliposhusha kibao chao cha Mdundiko. Ndani ya
kibao hicho, bendi haikuhitaji steji shoo kwani kadamnasi ilivamia
jukwaa na kunengua mdundiko vilivyo.
Kibao cha tatu kilitii kiu ya wadau wanaozungumza lugha ya kifaransa
waliohudhuria kama vile vile kutoka nchi za Ufaransa, Burundi, Algeria
na Senegal. Kibao hicho kinaitwa "Mon Ami".
Baada ya Mon Ami, wapenzi wa rhumba la asili lililojaa mirindimo ya
ngoma za asili kutoka makabila ya Kitanzania walipewa ladha hiyo kupitia
kibao kinachoitwa Moro Moro.
Moro Moro ilipoisha, ukawa muda mwingine wakupata Blues pale bendi
ilipongurumisha kibao kingine maarufu kinachoitwa "Wazazi Wangu". Katika
kibao hiki Leo na baba yake mzazi Henry Mkanyia walibishana vilivyo
katika magitaa pale kila mmoja wao alipocheza solo kwa kupishana.
Wapenzi walidataje?
Ngoma iliyomaliza shoo siku hiyo iliwarudisha wapenzi kwenye viunga vya
kizaramo pale "Shikandwambwe" ilipotupwa hewani. Jukwaa halikutosha
maana wadau mbalimbali walijialika ili kuonyesha vimbwanga vyao vya
kucheza mirindimo hiyo kutoka kabila maarufu la Wazaramo. Leo aling'aa
kwa mara nyingine pale alipoweka gitaa pembeni na kuchukua kinanda cha
mdomoni "harmonica" na kuwakumbusha wadau jinsi mwanamuziki mkongwe
Stevie Wonder alipoanza maisha yake marefu ya muziki.
Mwandishi wa habari hizi alifanikiwa kuongea na meneja wa Leo Mkanyia
ofisi ya Ulaya na America bwana Samia X na kumuuliza ni nini mipango yao
baada ya Tamasha hili. Akiongea katika kiswahili fasaha na
kilichonyooka Samia X alijibu; Baada ya Tamasha la DoaDoa, bendi itarudi
katika uwanja wa nyumbani wa Hoteli ya nyota tano ya Serena Dar es
Salaam. Na mipango thabiti inaendelea ili kuratibu ziara ya bendi katika
bara la Ulaya kwenye kipindi kijacho cha majira ya joto. Alimalizia
Samia X.
Post a Comment