Tunawaunga mkono wabunge waliojitokeza kupinga kuwasilishwa kwa hati ya dharura muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa mwaka 2015.
Wakizungumza bungeni juzi, baadhi ya wabunge
waliihoji Serikali sababu ya kuharakisha kuwasilisha muswada huo kwa
ajili ya kupitishwa kama sheria.
Si wabunge pekee, wadau wa sekta ya habari
wanajiuliza kuhusu uharaka wa muswada huo ambao kimsingi si suala la
jana au juzi. Ni suala la muda mrefu ambalo wadau wa habari wamekuwa
wakilipigania.
Ikiwa muswada huu utawasilishwa kwa njia ya hati
ya dharura, ina maana utasomwa kwa mara ya kwanza na kupitishwa
vipengele vyote kwa siku moja. Hii ina maana kuwa si wadau wa habari
wala watunga sheria wetu, watakaopata muda wa kutosha wa kuupitia
muswada na kujiridhisha kuwa una kila sababu ya kuwa sheria kwa
maendeleo ya sekta ya habari na wanahabari.
Aidha, wadau wa habari kama wataalamu wa sekta
hiyo, watakosa fursa ya kuwaelewesha wabunge masuala mbalimbali yaliyomo
katika muswada, ili hata wanapoupitia wawe na weledi wa kutosha wa kitu
wanachotaka kukipitisha kuwa sheria rasmi.
Mchakato mzima wa suala hili umegubikwa na usiri
ambao sisi tukiwa wadau wa habari, unatupa wasiwasi na hata kujiuliza
una maana gani? Nini kimejificha nyuma ya usiri huu?
Tumesema hapo awali hili si suala la jana wala
juzi, tumekuwa tukilipigania kwa muda mrefu. Kwa nini taratibu za
kawaida za uwasilishaji wa miswada zisifuatwe ili wadau wote
wajiridhishe kuwa sheria itakayotungwa itakuwa na tija na maendeleo kwa
sekta yenyewe, wanahabari na Taifa kwa jumla?
Kinachotokea sasa kuhusu haraka na usiri
ulioligubika suala hili, wadau wa habari hasa wanahabari wanaweza
kusukumwa kuamini kuwa kuna dhamira isiyo njema kwao.
Hofu hii ya wanahabari imeshaanza kujidhihirisha
katika mjadala bungeni, baada ya baadhi ya wabunge kufikia hatua ya
kuinyooshea kidole Serikali kuwa pengine ina dhamira ya kutaka
kuvikandamiza vyombo vya habari kupitia muswada huo.
Hatutaki kuamini kuwa Serikali yetu sikivu na
inayoongoza kwa misingi ya kidemokrasia, inaweza kutunga kwa makusudi
sheria inayolenga kuvibana vyombo vya habari. Na kama itakuwa hivyo,
tunauliza ni kwa masilahi ya nani?
Tunawakumbusha viongozi na watendaji serikalini
kuwa Tanzania ni nchi yetu sote, hakuna mtu mwenye haki ya kujiona yeye
ni Mtanzania zaidi kuliko wengine au mzalendo kuliko wengine.
Tunatoa tanbihi hii kwa kuwa umejengeka utamaduni
wa viongozi serikalini na hata wanasiasa kufikiri kuwa wao ni weledi wa
kila kitu kuhusu maendeleo na ustawi wa Taifa hili.
Watu hawa wachache siku zote wanalazimisha maoni, mitazamo na
fikra zao vitamalaki hata katika mazingira ambayo umma mpana unaona siyo
sahihi tena kwa kuegemea katika hoja zenye mashiko.
Matokeo ya utamaduni huu wa wachache kujiona ndiyo
wenye uwezo wa kufikiria kwa niaba ya wengine, tuliyaona wakati wa
mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba wakati wanasiasa walinyofoa mambo
mengi yaliyopendekezwa na wananchi, wakapendekeza wanayoyataka wao.
Mwishowe mchakato huo umegawanya nchi.
Na ndio maana tunasema muswada huu hauna udharura
wowote, kwanini uwe siri? Urudishwe kwa wadau wauone ili kuzuia
mgawanyiko mwingine.
Post a Comment