PROFESA Ibrahim
Haruna Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf) siyo
mtu wa kutiliwa shaka kuhusu ‘madini’ aliyonayo kichwani. Ni msomi
aliyebobea kwenye masuala ya uchumi duniani.
Amezaliwa
Juni 6, 1952, katika kijiji cha Ilolangulu mkoani Tabora. Safari ya
elimu iliyompa uprofesa aliianza mwaka 1959, akisoma elimu ya awali na
msingi katika shule ya Sikonge.
Baadaye
akajiunga na Sekondari ya Tabora Boys, akaenda Pugu Sekondari, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam na kisha kupaa ng’ambo chuo cha Stanford nchini
Marekani alikotunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya uchumi.
Safari ya
elimu ya Profesa Lipumba ni ndefu lakini ni yenye mafanikio makubwa.
Sina shaka ni kutokana na uwezo wa kimasomo aliokuwa nao mhusika na
mvuto miongoni mwa wanafunzi wenzake ambapo aliukwaa uongozi karibu kila
awamu ya masomo aliyojiunga nayo.
Akiwa
shule ya msingi alikuwa kiranja, Tabora Boys akachaguliwa kuwa Mweka
Hazina wa Umoja wa Vijana. Pugu Sekondari alikuwa mjumbe wa Kamati ya
Umoja wa Vijana, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akachaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana, akahitimisha safari yake ya kimasomo wa
kuwa Rais wa Kwanza wa Umoja wa Vijana wa chuo cha Stanford.
Kwa
mtiririko huu wa uongozi, Profesa Lipumba ana nyota ya uongozi hivyo
haliwezi kuwa jambo la kutilia shaka unaposikia kuwa chama chake
kimemteua kuwa mgombea urais anayetafuta tiketi ya uwakilishi wa
muungano ya vyama za kisiasa vya upinzani nchini (Ukawa).
SIFA ZA KUWAKILISHA UKAWA KWENYE URAIS 2015 ANAZO?
Wafuasi
wake ndani na nje ya chama wanamuona anafaa. Hata mwenyewe amejinasibu
mara nyingi kuwa ni mtu asiyejitilia shaka katika kubeba dhima ya
uongozi wa nchi.
Pengine
ni kwa sababu amekuwa kiongozi mzuri katika maisha yake. Maana mbali na
maisha ya shule niliyoeleza, Profesa Lipumba amewahi kuwa msaidizi wa
rais wa masuala ya uchumi nchini kati ya mwaka 1991-1993, wakati huo
Rais wa Jamhuri alikuwa Ali Hassan Mwinyi.
Mbali na
kazi hiyo ambayo ameifanya ikulu, ana hazina ya elimu ya uchumi ambayo
ndiyo msingi wa matatizo ya nchini hivi sasa. Lulu ya elimu yake siyo tu
imetambulika Tanzania kama nchi maskini inayohaha kujikwamua kiuchumi,
la hasha! Hata taasisi na mashirika makubwa duniani yamepata kutumia
ufahamu wake katika kujiendesha.
Profesa
Lipumba amewahi kuwa mmoja wa washauri wa masuala ya uchumi wa Benki ya
Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la
Maendeleo na Ushirikiano la Norway (NORAD), Shirika la Maendeleo la
Kimataifa la Denmark (DANIDA), Shirika la Maendeleo na Ushirikiano wa
Kimataifa la Sweden (SIDA), Dawati la Uchumi Mambo ya Nchi za Nje nchini
Finland na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Hayo ni
kwa uchache, lakini kiongozi huyu amepata pia kushiriki katika utafiti
wa kibiashara wa nchi za Kusini mwa Afrika, amepata kuwasilisha mada
Shirika la Fedha la Dunia (IFM) kuhusu namna ya kuzisaidia nchi maskini
ikiwemo Tanzania na kisha kutayarisha vigezo kuhusu utambuzi wa nchi
maskini zaidi duniani.
Naibu
Mkurugenzi wa Mipango na Bunge wa Cuf wakati akimtangaza Profesa Lipumba
kuwa ni mgombea wao wa urais kupitia Ukawa alisema hawana shaka juu ya
sifa za mwenyekiti huyo kupeperusha bendera ya upinzani kuwania urais na
akasisitiza kuwa vigezo vikitazamwa hakuna wa kumlinganisha naye.
Naam,
hata mimi na wengineo tunapotazama rekodi, elimu na uzoefu wa Profesa
Lipumba hatuna cha kubisha zaidi ya kusema anafaa sana kuwa rais wa
awamu ya tano.
USOMI NA REKODI VITAMSAIDIA LIPUMBA KUWA RAIS 2015?
Weee!
Sitarajii jibu likawa ndiyo kwa sababu Lipumba ameshaonja joto la jiwe
la uchaguzi mkuu wa rais kwa miaka 20, akaangukia pua!
Mwaka
1995, alipojitosa mara ya kwanza katika kinyang’anyiro cha uchaguzi
Profesa Lipumba alipigwa mwereka na Benjamin Mkapa ambaye hakuwa na
kiwango kikubwa cha elimu.
Nambuka
alishika nafasi ya tatu nyuma ya Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi (wakati huo)
Augustino Mrema, ambaye moto wake wa siasa za upinzani ulikuwa mkali.
Mwaka
2000 Lipumba alirudi tena kwenye kinyang’anyiro dhidi ya Mkapa,
akajitutumua mno na kushika nafasi ya pili. Wengi na hasa wafuasi wake
waliamini kuwa kasi aliyokuwa nayo huenda ingekiwezesha chama chake
kushika dola kwenye uchaguzi wa mwaka 2005. Haikuwezekana!
Alitimiza
mwaka wa 20 kwa kurudi tena kwenye uchaguzi mkuu kuwania urais, mkononi
mwake akiwa na usomi, rekodi na uzoefu wa masuala ya uchaguzi; hapo pia
nyota haikuwaka! 2010, aliyeshinda akawa rais wa sasa, Jakaya Kikwete,
akifuatiwa na Dk. Wilbroard Slaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) na yeye akiambulia nafasi ya tatu. Waliomtangulia hawakuwa na
sifa kama zake.
PROFESA LIPUMBA ATAWEZA KUKATA KIU YA URAIS 2015?
‘Maradhi
ya kisiasa’ yaliyomdhoofisha kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama
vingi bado hayajatibika. Uzoefu wa ushindi katika nchi hii unategemea,
pamoja na mambo mengine, nguvu ya chama cha mgombea.
Mwaka
1995, chama cha Cuf hakikuwa maarufu ukilinganisha na NCCR-Mageuzi cha
Mrema. Matokeo hayakuleta miujiza, ushindi ulipangwa kulingana na nguvu
ya vyama. Bila chama imara hujaeleweka bado; tatizo hilo halijatafutiwa
tiba na Cuf.
Binafsi
sijaona mapinduzi ya umaarufu; Cuf iliyokuwa chama kikuu cha upinzani
imebaki kuwa mshiriki wa tatu. Nachelea kuamini kuwa ndoto za Lipumba
kuingia ikulu zinaweza kutimia 2015, ingawa kwa sehemu fulani malengo ya
Ukawa kuunganisha nguvu yakitimia yanaweza kubadilisha matokeo.
Hata
hivyo, hiyo inabaki kuwa imani kwa sababu Chadema ambao ni washirika
wakubwa wa Cuf nao wanatumaini la kumweka mgombea wao wakiamini umaarufu
wa chama chao waliotoka nao kwenye uchaguzi uliopita wakiingia nao
mwaka huu wataumalizia mkia wa CCM walioubakiza 2010 na hivyo kuingia
ikulu.
Ikiwa ni
hivyo, sioni uchu wa urais wa Lipumba aliodumu nao kwa miaka 20 kama
unapata ‘nyama’ ya kutafuna mwaka huu! Pengine miujiza itokee maana
wakati mwingine upepo wa siasa hugeuka.
Hapa
ndipo ninapoona Ukawa wanafuata ‘mkono’ wa CCM unaoning’inia wakiamini
huenda utaanguka wapate kitoweo; hii ni falsafa ya fisi kufuata mkono wa
binadamu akiamini utaanguka autafune.
Kwa mbali
naona Ukawa wanasubiri chama tawala wavurugane, wateue asiyefaa ili wao
wapate kura za hasira za wafuasi wa CCM ambao hawataridhika na uteuzi
wa mgombea waliyemtarajia kuwaletea mabadiliko.
Aisee, hili ni suala la kusubiri na kuona!
Post a Comment