Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa
habari kuhusu mkutano wa umoja huo uliomalizika jana. Kulia ni Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, wa pili kulia ni
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NLD, Dk
Emmanuel Makaidi.Picha na Mwinyi Sadallah.
Zanzibar. Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesema kila chama ndani ya umoja huo kiko
huru kutoa fomu na kuandaa wanachama wake watakaoshindanishwa katika
mchakato wa kuwapata wagombea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Tamko hilo lilitolewa na viongozi wakuu wa Ukawa baada ya kumalizika kwa
kikao cha siku mbili kilichofanyika Shangani, Zanzibar kujadili hali ya
kisiasa na utaratibu wa kuwapata wagombea wa nafasi za udiwani,
uwakilishi, ubunge na urais.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema wagombea wa umoja huo
watapatikana kwa kuzingatia sifa na uwezo wa kila mmoja na nia ya kweli
ya kuleta mabadiliko katika nchi.
“Hakuna chama kinachozuiwa kutoa fomu kutafuta wagombea katika mchakato
wa ndani wa chama kabla ya Ukawa kufanya uteuzi wa mwisho,” alisema
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema.
Kuhusu mvutano
Kauli ya Mbowe inakuja wakati kukiwa na wasiwasi miongoni mwa wanachama
na wajumbe wa kamati ya ufundi ya Ukawa kutokana na mvutano wa kila
chama kutaka majimbo fulani ambako kila kimoja kinadhani kinakubalika.
Hata hivyo, Mbowe alisema Ukawa inaendelea kuimarika tangu kuasisiwa kwake na hakuna mpasuko kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
“Hakuna mushkeli, uhusiano wetu Ukawa unaendelea kuimarika na
tutahakikisha tunasimamisha mgombea mwenye sifa na uwezo wa kutuletea
ushindi, hatutagubikwa na masilahi ya vyama, tunataka masilahi ya Ukawa
kwanza vyama baadaye.
“Ni ndoto Ukawa kumeguka kwa sababu tumetambua umoja ni nguvu na wenzetu
wanasubiri kuona tunameguka,” alisema Mbowe katika mkutano huo
uliohudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif
Sharif Hamad.
Gharama za uchaguzi
Alipoulizwa kuhusu gharama za uchaguzi ndani ya Ukawa, Mbowe alisema ni
mapema kueleza hilo lakini hawatarajii kumwaga fedha kama wanavyofanya
baadhi ya wagombea wa chama tawala katika kutafuta nafasi mbalimbali za
uongozi ikiwamo urais wa Muungano... “Ukawa tunajiamini, tuna uwezo wa
kushinda dola.”
Awali, Mwenyekiti wa CUF ambaye pia mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa
Ibrahim Lipumba alisema kikao hicho kimepata mafanikio makubwa na
kusisitiza kuwa wagombea wa Ukawa watatangazwa baada ya kukamilika
mchakato ndani wa vyama.
Alisema kwa mwelekeo wa kisiasa baada ya kufanya tathmini, Ukawa ina
nafasi kubwa ya kuingia Ikulu ya Muungano na Zanzibar mwaka huu kutokana
na CCM kushindwa kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.
Alisema lengo kubwa la Ukawa ni kuwa na Tanzania mpya yenye maendeleo na
sera ya maisha bora kwa Watanzania wote na kuwataka wananchi kuwa
tayari kuyapokea mabadiliko ya kiutawala baada ya Uchaguzi Mkuu.
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema chama chake si
msindikizaji katika Ukawa na nia yake ni kuona mabadiliko ya kiutawala
yanatokea. Aliwataka Watanzania kuwa tayari kufanya uamuzi mgumu.
“Tayari nimeota ndoto Ukawa wanakamata madaraka ya nchi mwaka huu,” alisema Makaidi.
Katiba mpya
Akizungumzia Kura ya Maoni ya Katiba inayopendekezwa, Mbowe alisema Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), haiwezi kufanya mambo mawili kwa wakati
mmoja na kutaka Kura ya Maoni isitishwe kwa sababu muda wa maandalizi ni
mdogo na imeshindwa kuandikisha wapiga kura kutokana na ukosefu wa
vifaa.
Alisema Serikali kuendelea kulazimisha Kura ya Maoni wakati matayarisho ni mabovu kutasababisha vurugu.
Mwananchi
Post a Comment