
Dar es Salaam. Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany amemwomba Rais Jakaya Kikwete kusaini hukumu ya kunyongwa hadi kufa inayowakabili watu wanne waliopatikana na hatia ya kumuua mtu mwenye ulemavu wa ngozi.
Mahakama Kuu, mwishoni mwa wiki iliwahukumu kifo watuhumiwa hao baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Zawadi Magindu (32).
Akizungumza na Mwananchi, Barwany alisema imekuwa
ni jambo la kawaida kwa adhabu hizo kutolewa, lakini utekelezaji wake
umekuwa mgumu.
“Ningemwomba Rais kabla hajamaliza muda wake,
achukue hatua ambayo itamfanya akumbukwe siku zote. Katika jambo kubwa
kama hili, ni vyema akaweka saini ili hukumu hii itekelezwe,” alisema
Barwany.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu
anayewawakilisha watu wenye ulemavu wa ngozi bungeni, Al-Shaymaa Kwegir
alisema adhabu hiyo ni sahihi kwa kuwa wahusika walionyesha kukusudia
kuua.
Alisema amefarijika na adhabu hiyo kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kufanya uhalifu kama huo.
“Kwa upande wangu, naona adhabu iliyotolewa inastahili kabisa, mtu aliyeua kwanini naye asiuawe,” alihoji Kwegyir.
Alisisitiza kuwa kama adhabu hiyo itaendelea kutolewa, vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi vitakwisha nchini.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu LHRC Kijo Bisimba alisema licha ya kuwa adhabu hiyo inalenga
kukomesha vitendo hivyo, lakini inakiuka haki za binadamu.
Alisema kuna haja ya kuangaliwa upya kifungu cha adhabu ya kifo na kuondolewa kwenye sheria na kitumike kifungo cha maisha.
“Kwa kosa walilofanya wanastahili adhabu kubwa
ambayo binafsi naona kifungo cha maisha kingewafaa zaidi siyo
kunyongwa,” alisema.
Akitoa maoni yake kuhusu adhabu hiyo, Mwenyekiti
wa Chama Albino (Tas), Ernest Kimaya alisema majaji wameonyesha
kuzingatia sheria na kusisitiza utekelezaji ufanyike haraka.
Kuhusu kuzichapa Ikulu
Katika hatua nyingine Kimaya amezungumzia vurugu
zilizoibuka juzi kwenye Viwanja vya Ikulu baada ya watu wenye ulemavu wa
ngozi kumtuhumu kuonana kinyemela na Rais Jakaya Kikwete.
Kimaya alisema vurugu hizo zilisababishwa na
baadhi yao ambao hawakuelewa utaratibu. “Ule haukuwa mkutano wa hadhara,
Rais alitaka kukutana na viongozi wa chama Taifa, lakini tulishangaa
kuibuka kundi kubwa,” alisema.CHANZO:MWANANCHI
Post a Comment