0


Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Conchesta Rwamlaza, amedai kuna  minong’ono kuwa askari wa usalama barabarani  hupangiwa kiwango cha kukusanya na kuwakilishwa kwa viongozi wao na hivyo kuwafanya kujali zaidi fedha kuliko kusimamia sheria za barabarani.
Akiuliza swali bungeni leo, Rwamlaza alihoji serikali inasemaje kuhusiana madai hayo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima, alisema Sheria za Usalama wa Barabarani namba 67 ya mwaka 1973 inatoa mamlaka kwa askari wa barabarani kutoza faini za papo kwa papo kwa makosa mbalimbali ya usalama wa barabarani.
“Hili ni moja ya jukumu la msingi la kikosi cha usalama wa barabarani unaolenga kuimarisha usimamizi wa Sheria za Usalama wa Barabarani,”alisema.
Alisema ukamataji wa makosa ya barabarani na faini ya papo kwa papo hulenga katika kuwatia hofu ya adhabu madereva wakorofi hivyo kuwafanya wafuate sheria na kanuni za usalama barabarani.
 “Hakuna kiwango cha pesa ambacho askari wa usalama wa barabarani amepangiwa kukusanya, askari ameelekezwa kukamata makosa kwa wingi iwezekanavyo hususani makosa hatarishi kama vile mwendo wa kasi, ulevi, ujazaji wa abiria na mizigo, uendeshaji wa hatari na kadhalika,”alisema.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalum , (CUF), Mkiwa Kimwaga, alisema askari wa vitochi barabarani wamekuwa ni kero kubwa kwa madereva.
“Wakati mwingine wanasimamisha magari kama sita na wanakwambia kuwa na wewe umekuwa ukiendesha katika mwendo kasi,”alisema.
Alihoji ni lini serikali itanunua vitochi vya kisasa ambavyo vitatoa na namba badala ya vya sasa ambavyo vinaonyesha mwendo tu kama walivyoahidi katika bajeti iliyopita.
Akijibu swali hilo, Silima alisema wananchi hawatakiwi kuona kero kwa vitochi kwa sababu viko pale kwa ajili ya kuepusha ajali.
“Fikra kwamba vitochi ni kero mziondoe kabisa, tunakerwa ili tusife tunataka maisha yenu yaendelee,”alisema.
Alisema ajali nyingi zinazotokea nchini zinasababishwa na mwendo kasi. Hata hivyo, alisema serikali imeshanunua baadhi ya kamera za kisasa zinazoonyesha namba za gari.Alisema kuwa kamera hizo zinaweza kurekodi namba na mwendo na kesho yake dereva akaelezwa makosa yake.
CHANZO:MWANANCHI

Post a Comment

 
Top