0

MBUNGE WA MASASI MARIAM KASEMBE
 Katika ahadi zangu wakati nagombea sijawahi kuahidi mashine za kusaga. Kama wana shida ya mashine za kusaga waseme wasaidiwe.
1. Ernest Wendeleni, Chikunja.
Hakuna zahanati Chikunja, uliahidi utajenga mpaka leo kimya. ?
Jibu: Kwanza niseme kuwa Ernest hajafika Chikunja kwa zaidi ya miaka mitano. Chikunja kuna zahanati inafanya kazi kwa zaidi ya miaka mitano sasa na wananchi wanapata huduma. Hata hivyo tutaendelea kuhakikisha huduma za afya zinakuwepo na zinapatikana kama ilivyopangwa.
2. Hassan Hassan Misinzo, Ndanda.
Uliahidi utahakikisha kuna mashine za kusaga mpaka sasa hakuna. Kwa nini hukutimiza ahadi hiyo?
Jibu; Katika ahadi zangu wakati nagombea sijawahi kuahidi mashine za kusaga. Kama wana shida ya mashine za kusaga waseme wasaidiwe.
3. Hassan Mpalanga. Masasi Mjini.
Hakuna vituo maalumu vya usafiri katika maeneo mengi, lini utabadilisha mandhari ya mji wa Masasi iwe ya kupendeza?
Jibu:Tuna stendi kuu ya mabasi Masasi mjini, ambayo ina kituo kikubwa cha mabasi ya mikoani na ya ndani. Hata hivyo tumeshatengeneza eneo la kujenga stendi kubwa kwa sababu kuna ongezeko kubwa la watu na maendeoe. Eneo hilo lipo karibu na uwanja wa ndege.
4. Prisca Mlaponi, Nagaga.
Hospitali ya Nkomaindo bado inakabiliwa na uhaba wa dawa na vitanda. Uliahidi tatizo hilo litakwisha. Vipi mpaka sasa unatusaidiaje?
Jibu: Ni kweli kulikuwa na uhaba wa vitanda na dawa, nilitafuta wafadhili, nikapeleka vitanda na magodoro. Magodoro ya ‘ICU’ yalinunuliwa ili kusaidia wagonjwa mahututi lakini ieleweke kuwa suala la dawa ni tatizo la nchi nzima. Nimejitahidi kufanya vikao na halmashauri ili kuhakikisha kuwa fedha zinazipatikana zinunue dawa muhimu. Nilimueleza Rais kuhusu tatzo hili, alitoa muongozo kutatua hilo. Sisi viongozi tunalifanyia kazi bado.
5.Deniss Chimwaga, Liwale
Kwa nini umeme mpaka sasa haujafika katika maeneo mengi. Huoni kuwa uchumi wa Masasi utaimarika kama umeme utakuwepo?
Jibu: Nilipoingia madarakani, umeme ulikuwepo katika maeneo ya mijini tu. Lakini kwa kipindi nilichokaa madarakani umeme umeendelea kuwepo katika maeneo mengi kwa kupitia wakala wa umeme vijijini, REA. Hata hivyo umeme utaingia vijijini hatua kwa hatua, umeme utawekwa kama nilivyoahidi. Alipokuja Rais Jakaya Kikwete na Nape Nnaye, nilitoa wazo, kuwepo kwa programu maalumu ya kusambaza umeme vijijini, wananchi watashindwa kuelewa kuwa gesi imewanufaishaje. Niliomba pia katika ilani ya CCM, Masasi ipewe kipaumbele kupata umeme.
6. Christopher Saimon Mtambalike, Chigugu.
Ufaulu ni mdogo sana shule za Masasi, mimba za utotoni zimekithiri na elimu ni duni kwa ujumla. Utaliondoaje tatizo hili?
Jibu; Ni kweli kabisa. Sababu ya elimu duni ni kwanza changamoto kutoka kwa wazazi kutowaandaa watoto kielimu. wapo tayari kuwasomesha watoto hadi darasa la saba tu, baaada ya hapo hawataki. Kuna shule za kata maeneo mengine kuna shule mbili lakini wazazi wanakataa kuwapeleka watoto. hawafanyi mandalizi mazuri kwa watoto. Lakini pia kuna upungufu wa walimu suala ambalo nimelipeleka wizarani na wananisaidia. Kuna upungufu wa madarasa lakini fedha za mfuko wa jimbo zimesaidia. Wazazi wapo tayari kuchangia harusi, unyago wa kifahari lakini kupeleka watoto shule wanakuwa wagumu. Viongozi wanahamasisha na kujenga shule za sekondari, msingi na vyuo lakini bado kuna tatizo kwa wazazi.
7. Alfred Mitande, Liwale.
Wanafunzi wengi wanatumikishwa kazi wakiwa shuleni hali inayosababisha washindwe kufanya vizuri kwenye masomo. Je, utatusaidaje kuondoa tatizo hili.
Jibu; Hata sisi zamani tulikuwa tunafanya kazi shuleni na elimu ilikuwa juu. wazazi wa sasa hawataki watoto wafanye kazi. leo hii ni shule chache zenye mashamba. Zamani ilikuwa tunalima shamba la shule halafu tunapata chakula shuleni hapo hapo. Ninatembelea shule na kufanya vikao hilo ni tatizo ni dogo sana. lakini kwa sasa wazazi hawataki hilo, wamebadilika hivi kweli mwalimu atashindwa kumtuma mwanafunzi ndoo ya maji. Kazi nyingine ni sehemu ya wajibu wao.
8. Anna Martin, Chikunja.
Uliahidi visima katika vijiji vyote vya masasi na kuwa tatizo la maji litapungua. Vipi mpaka leo hakuna matokeo chanya.
Jibu; Nilipoingia madarakani kulikuwa na shida ya maji kuanzia mijini hadi vijijini. Ndoa zilikuwa mashakani, lakini hilo tatizo limepungua kwa kiasi kikubwa. Nina mradi wa maji Liwale ukikamilka utasaidia vijiji vitatu ambavyo ni Lilala, Muungano na Nanyindwa. Kuna mradi upo tayari kijiji cha Mtakuja wananchi wanapata maji. Kuna mradi Nambawala Nanganga, Ndanda, Chipute na Nkwera kote miradi inaendelea kuwasaidia wananchi wapate maji. Mradi ukikamilka utahudumia vijiji hivyo. Kuna miradi ya mabwawa huko Muungano na Chiwale. Hizo zote ni jitihada kuhakikisha jimbo langu linapata maji.
9.Happiness Namulimuka, Liwale.
Usafiri wa bodaboda unatumika kufanya matukio mengi ya uhalifu wilayani Masasi, je, utaliutatuaje hili?
JIBU; Bodaboda zinawasaidia wananchi kuanzia mjini na vijijini, kama zinatumika katika uhalifu, hilo suala ni la kiusalama zaidi. Sijawahi kupokea malalamiko hayo kwangu na kama wanapeleka malalamiko polisi basi wanapeleka sehemu sahihi. Hata hivyo nitazungumza na mkuu wa mkoa na kupata ukweli, kama ni kwli zitafanyika jitihda za kuondoa tatizo.
10.Victor Kasembe, Masasi Mjini.
Hatukusikii mara kwa mara bungeni ukiwatetea wananchi wako kama wabunge wengine. Je, tutakupaje kura kwa msimu huu?
Jibu; Nafikiri Victor husikilizi kipindi wala hufuatilii. Ninayo orodha ya maswali ninayouliza bungeni. Zipo rejea za maswali na michango yangu na nina orodha ya kila kitu ninachofanya bungeni. Sikurupuki kuzungumza mambo ambayo si ya msingi. Maendeleo haya yote nimeyapata kupitia michango yangu na maswali ninayoyatoa bungeni. Victor nakuomba unipe kura yako ili niendelee kuzishughulikia kero nyingine zilizopo Masasi.
 

Post a Comment

 
Top