0
 KAMUSI YA KISWAHILI SANIFU
        MAENEO YENYE WASEMAJI WA LUGHA YA KISWAHILI
Baada ya kutafakari juu ya matumizi yasiyo sahihi ya lugha yetu ya Kiswahili, hivi karibuni nilishawishika kuandika ili kutoa mchango wangu kuhimiza matumizi ya lugha yetu kila mahali.
Bado kila ninapopata nafasi nafuatilia kwa karibu kuona namna ambavyo wasomi na viongozi wetu na waigizaji wa michezo ya filamu wasivyoienzi lugha yetu.
Katika kituo kimoja cha televisheni hivi karibuni, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), walikuwa wakitoa maelezo ya namna wanavyofanya shughuli zao.
Kilichonivutia ni kwamba miongoni mwa watumishi wa taasisi hiyo ya umma wamo wageni kutoka nchi zilizoendelea. Mmoja kati yao ni Fritz Raifmakers.
Raifmakers alinikosha kwa namna alivyozungumza kwa kutumia lugha yetu kwa ufasaha, ukweli alinifurahisha. Bila kuchanganya na Kiingereza pamoja na yeye binafsi kutoka moja ya nchi za Ulaya. Ukweli si yeye tu, nafahamu wapo wazungu wengine wengi ambao kwa kweli hukizungumza Kiswahili sanifu na kwa ufasaha mkubwa.
Baadaye, ofisa mwingine wa PPRA ambaye ni mswahili mwenzetu, kama kawaida ya wasomi wetu, ilipofika zamu yake hali ilibadilika ghafla, alikipa kisogo Kiswahili.
Tuangalie mfano mwingine. Bila shaka wengi tunafuatilia mfululizo wa tamthilia ya Kichina inayoendelea katika Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC1) inayoitwa Maudodo na wakwe zake. Ukiifuatilia tamthilia hii inafurahisha.
Kwa nini? kwanza hadithi yenyewe, lakini la pili ambalo ndilo ningependa mlizingatie zaidi ni namna lugha yetu inavyotumika vizuri.
Tamthilia ile inakitangaza Kiswahili sanifu vizuri na kwa ufasaha. Ikumbukwe Wachina ni zaidi ya robo ya idadi ya watu wote duniani. Hii ni idadi kubwa mno ikilinganishwa na ya watu wote wanaozungumza lugha ya Kiswahili duniani kote ambayo inakadiriwa kufikia zaidi ya 150 milioni. Wachina wakiwamo.
Hii maana yake nini? Tutafakari kidogo. Tuna uhusiano mzuri na wa karibu na China. Na wao wana mikakati mikubwa na mingi ya kuwekeza nchini kwetu. Hivi tunavyoongea idadi ya Wachina nchini kwa tathimini ya haraka inaweza kuwazidi wageni wengine wote kwa pamoja. Acha wale wazungu wanaokuja nchini kama watalii.
Fikiria zaidi, itakuwaje miaka 20 ijayo kwa Wachina hawa wanaojifunza lugha yetu kwa bidii? Watanzania kwa takwimu ya idadi yetu ya hivi karibuni tunakadiriwa kufikia milioni 45. Idadi ya watu duniani kwa sasa inakadiriwa ni zaidi ya 6 bilioni ambayo, kama nilivyosema hapo awali, zaidi ya robo ni Wachina.
Kwa hesabu za haraka, wanakaribia bilioni 2. Linganisha na idadi yetu! Hii ina maana kwamba si muda mrefu Wachina wanaozungumza lugha yetu kwa ufasaha watakuwa wengi. Sisi tunaendelea kudandia lugha za wenzetu tena bila ya ufasaha wowote.
Faida kwa nchi yetu hapo ni kwamba lugha yetu itakuwa imepata na kuongeza idadi ya wazungumzaji wake. Hiyo ni neema maana itatusaidia kujenga hoja kwenye vyombo vya uamuzi duniani kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa moja ya lugha ya mawasiliano kwenye mikutano yake.
Wasanii ovyo
Wasanii nchini ni moja ya makundi makubwa katika jamii yetu. Ni kundi linalokua kwa kasi, hivyo linahitaji kuelimishwa kuwa lina wajibu mkubwa wa kuzingatia matumizi sahihi na sanifu ya lugha yetu ya Kiswahili.
Waigizaji wengi wetu hawakufanya vizuri shuleni, walishindwa. Ukifuatilia wengi walifanya vibaya kama sio kufeli somo la Kiswahili.
Vijana wetu leo hawajui Kiswahili wala Kiingereza. Matokeo yake, wanaishia kama wasomi wetu wengi hapa nchini, kuchomekachomeka maneno ya Kiingereza ambayo nayo wakati mwingine wala sio mahali pake, achilia mbali neno hilo kuwa sahihi au kukosewa kisarufi.
Hata hivyo, bado yapo matumaini mahali fulani. Nikirejea tena TBC1, kuna mfululizo wa tamthilia inayorushwa na kituo hicho cha Taifa, inaitwa ‘Siri ya mtungi’. Yenyewe bahati nzuri imeigizwa na wasanii wetu hapa nyumbani. Igizo lile limeigiziwa mjini Bagamoyo. Si nia yangu hapa kuilezea tamthilia hiyo, ila lugha iliyotumika ni fasaha, wengine waige.
Kukua kwa Kiswahili
Nafahamu na kukubali kuwa Kiswahili kinakua. Swali la kujiuliza kinakuaje? Kwa mfano, mimi siwezi kukubaliana na wale wanaodai kuwa kutohoa maneno ya Kiswahili kutoka lugha za wenzetu nako ni kukua kwa lugha yetu, si sahihi. Kwa nini tutohoe na maneno mengi tunayo?
Tujadiliane, kukuza lugha ni kufanya nini hasa? Kukua kwa lugha yetu kwa tafsiri sahihi, maana yake ni kupata neno jipya lenye asili ya moja na jamii zetu za Kitanzania na kuliingiza kwenye matumizi ya lugha yetu moja kwa moja. Mifano iko mingi, neno ‘kyenda’ lenye asili ya Uchaga, lina maana ya namba tisa. Ni miongoni mwa maneno yanayoongeza idadi ya maneno tuliyonayo ya Kiswahili. Huku ndio kukuza lugha yetu. Yapo mengi. Lakini kuna yale ya Kiswahili chenyewe ambayo hatuna utamaduni wa kuyatumia kabisa ambayo mara yanapotumika uonekana kama maneno mageni sana, kumbe sivyo.
Wakati Mwalimu Nyerere alipoamua kupumzika, aliwaambia Watanzania ‘nang’atuka’. Wengi wetu tulilisikia kama neno jipya kabisa. La hasha, ni kwamba halikuwa likitumika tu mara nyingi. Nihitimishe kwa kuwaomba Watanzania wenzangu kukitumia Kiswahili vizuri mahali popote wanapozungumza na hadhira yoyote ile ili wale wasiokifahamu sawasawa wapate jukumu la kukitafuta na kujifunza kwa bidii zaidi.

Post a Comment

 
Top