WATU wenye ulemavu wa ngozi, ambao ni wanachama wa Chama cha Maalbino
Mkoa wa Mwanza, wakiwa na wanaharakati wengine, mwishoni mwa wiki
iliyopita walitembea kwa miguu kutoka jijini humo hadi Butiama, liliko
kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na kuangua kilio cha
nguvu, wakilalamika kutotendewa haki ndani ya nchi aliyoiacha
salama.Akizungumza na gazeti hili kiongozi wa wanaharakati hao, Nkwenge
Mutash alisema safari yao ilianza Machi 13- 18, 2015 na walitumia siku
tano ili kufikisha ujumbe wao wa kupinga mauaji ya Albino na alitoa
shukrani kwa wanavijiji waliowaunga mkono wakiwa njiani kwa kuwapa maji,
chakula na mahitaji mengine muhimu.
Wakiwa njiani, wanaharakati ambao wengine walikuwa ni pamoja na
Khalid Seremani, Michael Athanas na Erick Mutta, walitembelea kituo cha
kulelea watoto wenye ulemavu wa ngozi kinachomlea Zakaria Mayala ambaye
aliondolewa nyumbani kwao Simiyu ili kumuepusha na hatari ya kuuawa.
Mwenyekiti wa chama hicho, Afred Kapole alisema waliamua kwenda
Butiama kwa hayati Baba wa Taifa ili kufikisha kilio chao kwa kulia
kaburini mwa muasisi wa taifa ili awasaidie kwani enzi za uhai wake
alipenda haki, usawa, upendo na amani, kwa vile hivi sasa wanaona
hawatendewi haki katika nchi iliyoachwa ikiwa na misingi ya upendo na
amani,” alisema Kapole.
Chifu wa kabila la Wazanaki, Japhet Wanzagi Nyerere aliyewapokea huko
Butiama, alisema wageni hao walikuja na kwenda kulia kaburini kwa
Nyerere, kiasi kwamba yeye kama binadamu amepata simanzi kubwa hasa
walipolalamikia kuhusu kunyanyaswa katika nchi yao na hivyo akatoa wito
kwa serikali kufanya kitu ili kurudisha imani ya watu hao mioyoni mwao.
Aidha chama hicho kimeomba kama amani kwao imeshindikana nchini Tanzania, basi wanaomba wahamishiwe katika nchi nyingine.
Post a Comment