Bendera ya Kenya na Tanzania zikiwa pamoja
Tangu Desemba 22 mwaka jana, kumekuwa na taarifa kwamba Serikali ya Kenya imezuia magari ya Tanzania, maarufu ‘shuttle’, yanayofanya safari za kupeleka wageni na watalii kati ya jijini Arusha na Moshi mkoani Kilimanjaro kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyata uliopo Nairobi nchini Kenya.
Amri hiyo ya Serikali ya Kenya iliwalazimu
mawaziri wawili, Lazaro Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii wa
Tanzania na Phyllis Kandie, Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki,
Biashara na Utalii wa Kenya kukutana kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.
Taarifa walizozisambaza kwenye vyombo vya habari
zilieleza amri hiyo imesimama na wamepeana wiki tatu kulitafutia
ufumbuzi. Hata hivyo baada ya wiki tatu kumalizika Waziri Kandie
alitangaza kurejesha tena amri hiyo.
Mgogoro ulioibuka hauna tofauti na ule wa Rwanda
na Tanzania ambapo, Serikali ya Rwanda ilipandisha ushuru wa barabara
(Road Toll) kwa magari ya mizigo yenye namba za usajili za Tanzania
kutoka Dola za Marekani 150 hadi Dola 500, kama ilivyo kwa Tanzania
waliokuwa wakitoza Dola 500.
Hata hivyo, tatizo hilo lilipatiwa ufumbuzi baada
ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kulazimika kupunguza hadi Dola 150
ili kulingana na Rwanda.
Ni wazi hata hili la sasa la magari yenye namba za
usajili wa Tanzania kuzuiwa kuingia uwanja wa Jomo Kenyatta, halitakuwa
jambo kubwa hadi kufika ngazi ya viongozi wa nchi kuingilia kati.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa
Tanzania, Dk Harrison Mwakyembe ameonyesha mwanzo mzuri katika wizara
hiyo kwa kuzungumza mambo ya msingi manne, ambayo kama yatazingatiwa
basi mgogoro huu hautafika mbali.
Dk Mwakyembe akizungumzia mgogoro huo wa magari ya
Tanzania kuzuiwa kuingia Jomo Kenyatta, alisema Tanzania itaendelea
kuwa sehemu ya mlango wa kuingia na kutokea kwenda kokote ikiwamo ndani
ya jumuiya na kwamba Serikali haitayazuia magari ya Kenya kuleta watalii
au kuwachukua katika viwanja vya ndege vya Tanzania.
Jambo la pili ambalo Dk Mwakyembe kwenye
mazungumzo yake na waandishi wa habari alilitamka, ni kwamba Tanzania
itaheshimu na kuzingatia amri hiyo ya Kenya ili kulinda undugu na
urafiki uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 tangu uhuru.
Kwa mantiki hiyo magari yenye namba za usajili za
Tanzania hayatasafirisha wala kupokea watalii kutoka au kwenda kwenye
Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta.
Jambo la tatu ni kwamba Tanzania itawahamasisha
watalii na wageni wote wenye nia ya kutembelea kwa ajili ya kujionea
vivutio vya kitalii, watumie viwanja vingine vya ndege ili kuondoa
usumbufu na gharama zisizo la lazima.
Hata hivyo, jambo kubwa ni pande zote kukaa meza
moja na kuujadili mkataba wa mwaka 1985 kati ya Tanzania na Kenya
uliolenga kutoa mwongozo wa ushirikiano katika Sekta ya utalii.
Makubaliano hayo yalielekeza maeneo mwafaka kwa ajili ya
kubadilishana watalii kwa lengo la kuwaondolea bugudha. Kama
ilivyofanyika kwenye mgogoro wa ushuru wa barabara, Kenya na Tanzania
bado zina fursa ya kulimaliza jambo hilo.
Tanzania na Kenya ni waasisi wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki ambao kimsingi wanatakiwa kuwa mfano wa kutatua matatizo
madogo kama hayo. Hivyo ni imani yetu jambo hilo litamalizwa ndani ya
muda mfupi na bila kuathiri wananchi.
Post a Comment