0
 
Meneja Mradi wa Kamati ya Uangalizi wa Chaguzi Tanzania (TEMCO), Dk Benson Bana
Dar es Salaam. Zaidi ya Sh720 bilioni zitatumika kuanika ‘uozo’ wakati wa mchakato wa uandikishaji wapiga kura, kura ya maoni na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Akitoa taarifa hiyo jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mradi wa Kamati ya Uangalizi wa Chaguzi Tanzania (TEMCO), Dk Benson Bana, alisema kuwa fedha hizo zimetolewa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kuwezesha mpango huo kufanikiwa.
Alisema kuwa kwa mara ya kwanza kamati hiyo, pia itaangalia mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya vyama vya siasa, utakaojumuisha wagombea urais, ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Udiwani.
Baada ya kumalizika kwa hatua hiyo, TEMCO itaandika ripoti ikatakayoweka wazi mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wanasiasa kuteua na kushinda nafasi wanazogombea ikiwamo kununua kura.
“Watazamaji wa uchaguzi watakuwa makini kuangalia mifumo ya kisheria na kitaasisi, uteuzi wa wagombea ndani ya vyama vya siasa, uthabiti wa tume za uchaguzi, utekelezaji wa Sheria ya gharama za Uchaguzi na uteuzi wa wagombea unafanywa na tume za uchaguzi,” alisema Dk Bana.
Aliongeza: “Tunafuatilia ili wananchi wa kawaida wawe na imani na mfumo wa uchaguzi katika nchi yao. Uchaguzi wa mwaka 2000 watu wengine walikuwa wanaogopa kusema sisi tulitokea tukasema hakukuwa na uchaguzi bali uchafuzi na tulifikiri wangetufukuza hawakufanya hivyo.”
Vile vile, TEMCO itaangalia upigaji kampeni, masuala ya jinsia, utendaji wa vyombo vya habari na matukio yatakayojitokeza wakati wa kupiga kura ikiwamo kuhesabu kura, kukusanya na kutangaza matokeo.
Dk Bana alisema zoezi hilo lililofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), litasimamiwa na watazamaji wa muda mrefu 180 watakao angalia zoezi la uandikishaji wapiga kura litakaloanza Februari mwaka huu.
Watazamaji wa muda mfupi 6,400 wanatarajiwa kuangalia shughuli za kila siku ya kupiga kura ya maoni, Uchaguzi Mkuu utaangaliwa na watazamaji wa muda mrefu 118 na 7,000 wa muda mfupi watakaopangwa katika vituo mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika uamuzi huo ni mzuri lakini wamechelewa kwa sababu hawapaswi kusubiri mpaka wakati wa uchaguzi wa ndani walitakiwa kuanza sasa wakati wa zoezi la kuandikisha wapiga kura.
“Haipaswi kuwa TEMCO pekee, waangalizi wa ndani wanapaswa kuwa wa kamati na taasisi mbalimbali ili kuwe na ulinganishi isije ikawa kamati moja inatumika vibaya,” alisema Mnyika.source:mwananchi

Post a Comment

 
Top