0
        
Moshi. Rais Jakaya Kikwete, amesema tatizo la upungufu wa madaktari nchini ni kubwa lakini akasema Serikali imejipanga na kuweka mikakati kabambe ya kulitatua.
Rais alitoa kauli hiyo leo wakati akizindua jengo la chumba cha upasuaji la hospitali ya Rufaa ya Mawenzi na kuweka jiwe la msingi jengo la wodi ya mama na mtoto.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kwa sasa daktari mmoja anahudumia wagonjwa 30,000 na muuguzi akihudumia wagonjwa 23,000, idadi aliyosema ni kubwa.
Alisema kwa Ulaya, daktari mmoja huhudumia wagonjwa 5,000 na kwamba ili nchi iweze kuondokana na tatizo hilo, ni kuzalisha madaktari wengi watakaofanya kazi nchini.
Kuhusu mapambano dhidi ya maradhi mbalimbali, Rais Kikwete alisema kwa sasa serikali inajenga uwezo wa ndani wa kupambana na magonjwa ukiwamo ugonjwa wa malaria.
Hata hivyo Rais Kikwete alisema ipo changamoto ya baadhi ya wananchi kutumia vyandarua wanavyopewa, kwa ajili ya kufugia kuku na kuweka kwenye bustani za mbogamboga.
Rais Kikwete alitumia uzinduzi huo kumwaga takwimu za Afya nchini, ambapo alisema pamoja na jitihada za Serikali, bado asilimia 49 ya wajawazito wanajifungulia nyumbani.
Alisema takwimu zinaonyesha vifo vya wajawazito vimepungua kutoka 126 hadi 119 kutoka kwa kila akina mama 100,000 na kuagiza kila zahanati kuwa na wodi ya kujifungulia akina mama wajawazito.
Akizungumzia hali ya lishe nchini, Rais Kikwete alisema hali sio nzuri na kubainisha kuwa asilimia 42 ya watoto nchini wana shida ya udumavu huku mkoa wa Kilimanjaro ukiwa na udumavu wa asilimia 28.
Alisema asilimia tano ya watoto wana ukondefu, asilimia 16 wana uzito mdogo huku upungufu wa madini joto ukiwa ni asilimia 35 na kwamba tatizo hilo ni kubwa nchini.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, upungufu wa madini joto mwilini husababisha magonjwa mbalimbali ukiwamo ugonjwa wa Goita.
Baada ya hafla hiyo, Rais Kikwete alikwenda kufungua jengo la kitega uchumi la Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF) ambalo ndilo jengo kubwa la kibiashara mkoani Kilimanjaro.SOURCE:MWANANCHI

Post a Comment

 
Top