Kwenye toleo letu la jana, ukurasa wa tatu tulikuwa na habari iliyokuwa na kichwa kisemacho “Repoa: Takukuru ilikithiri kwa kupokea rushwa 2014” iliyotokana na matokeo ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Afrobarometr ya Dar es Salaam.
Katika utafiti huo, imeonekana kuwa Takukuru,
ambayo inahusika na kuzuia na kupambana na rushwa, ilikuwa moja ya
taasisi 10 zilizoongoza kwa vitendo vya rushwa. Baadhi ya taasisi hizo
ni Jeshi la Polisi, ambalo lilishika namba moja, Mamlaka ya Mapato
nchini (TRA), majaji na mahakimu, maofisa wa serikali za mtaa na kwa
kiasi fulani Ikulu.
Kutajwa kwa taasisi hizo kunatia shaka jitihada
ambazo Serikali imekuwa ikisema inazifanya kupambana na rushwa kama ni
za dhati. Kama rushwa ndani ya Jeshi la Polisi haionekani kupungua kwa
kiwango kikubwa, wananchi wategemee nini?
Kama rushwa inazidi kujichimbia kwenye taasisi
kama TRA, kuna uwezekano wa wananchi kuwa na maisha bora ambayo
yaliahidiwa na Serikali ya Awamu ya Nne? TRA kuhusishwa maana yake ni
fedha nyingi ambazo zingeingia serikalini, zinakwenda kwa watumishi hao.
Serikali itapata wapi nguvu za kuwapa wananchi wake huduma muhimu kama
fedha ambazo zingelipwa kodi, zinaingia mifukoni mwa wafanyakazi wa TRA?
Kama majaji na mahakimu wametajwa, wananchi watapata wapi haki ?
Japokuwa imekuwa ni kawaida polisi kutajwa kwenye
tafiti mbalimbali kuwa inaongoza kwa vitendo hivyo vya rushwa, lakini
matokeo haya ya Afrobarometer yanastua kwamba rushwa inazidi kutapakaa
kwenye sehemu zote muhimu kwenye nchi ambayo raia wake bado wanaishi kwa
kipato kilicho chini ya Dola moja (Sh1,830) kwa viwango vya kimataifa.
Kutajwa kwa Takukuru kuwa miongoni mwa taasisi
zinazoongoza kwa rushwa, kunakatisha tamaa zaidi kwa kuwa ndiyo
inaonyesha ni kwa kiasi gani vita vya kupunguza tatizo hilo, ambalo ni
kero kubwa kwa wananchi, haiwezi kufanikiwa.
Kama rushwa imeingia hadi Takukuru, kuna haja gani
ya kusikiliza kilio chao kwamba taasisi hiyo ipewe meno ili iweze
kushughulikia watu inaowakamata kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya
rushwa?
Kwa maana nyingine, kama Takukuru itapewa meno
hayo, kuna uwezekano mkubwa kwamba watu wengi wakabambikiziwa kesi za
rushwa kwa lengo la kuwatisha watoe fedha ili wasipelekwe mahakamani.
Au kwa maana nyingine, hata wananchi raia wema
ambao wangetaka kutoa ushirikiano kwa Takukuru katika kubaini vitendo
vya rushwa vinavyohusu watu wenye fedha, maisha yao yatakuwa hatarini
kwa kuwa ni vigumu kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo kumsikiliza maskini
mzalendo anayetoa taarifa za tajiri mtoa rushwa.
Pia, ina maana kwamba kila kitu kinachotakiwa
kifanywe kwa kufuata sheria na taratibu, kinaweza kukiukwa kwa sababu tu
hakuna chombo madhubuti cha kupambana na rushwa, na matokeo yake ni
nchi kuelekea kusikofikirika.
Taasisi kama Takukuru ambayo imepewa jukumu la
kuzuia na kupambana na rushwa, haitakiwi iwe na hata chembe ya harufu ya
rushwa ili kujenga imani kwa wananchi, ambao wanashindwa kupata huduma
bora za hospitali, maji, elimu na nyingine kutokana na kukithiri kwa
rushwa.Rai yetu ni kwa wahusika kuisoma ripoti hiyo na kuifanyia kazi kubaini
ni wapi hasa taasisi hii imepotea ili pafanyiwe kazi na pili kusaka wote
ambao wameifanya taasisi hiyo iingie doa na kuwshughulikia kwa mujibu
wa sheria ili iwe onyo kwa wengine wanaojaribu kujiingiza kwenye rushwa.{source:mwananchi}
Post a Comment