Saikolojia ya kawaida inatufundisha kwamba ukiona mtu anaandamwa kwa kiwango kikubwa, wakati mwingine ujue ni kwa sababu amegeuka tishio kwa uhai, vyeo na madaraka ya wasiompenda.
Yesu Kristo aliandamwa na uongozi wa Kiyahudi siyo
kwa sababu alikuwa gaidi au jambazi, bali kwa sababu alikuwa ni tishio
kwa mamlaka na vyeo vyao.
Sitaki kumlinganisha Dk Slaa na Yesu, lakini kama
mwanadamu mwenzetu kuna yanayofanana na watu wengine duniani
waliofanyiwa, hila kama hizo kwa sababu tu walikuwa tishio kwa watawala.
Dk Slaa kwa sasa siyo padri kama wanasiasa wengi
wanavyodanganya umma wa Watanzania kwa sababu aliomba kibali cha
kuondolewa mamlaka ya kipadri na alikubaliwa.
Kuendelea kumwita padri ni porojo za kisiasa na
alama wazi ya hofu ya wapinzani wake kuelekea uchaguzi ujao na
kuwapotosha wananchi wasiojua nini kinaendelea katika nchi yetu.
Ni dhahiri Dk Slaa kwa sasa ni mwiba kwa CCM na
vyama vyenye mrengo wa CCM vinavyoamini katika siasa zisizo na faida.
Kama kiongozi wa chama cha upinzani (Chadema) Dk Slaa ana mvuto wa pekee
kwa Watanzania bila kujali dini, itikadi, kabila, vyeo wala tabaka la
watu.
Dk Slaa amejizolea sifa nyingi katika utendaji
wake pamoja na kurushiwa madongo mengi kwa lengo la kumchafua, lakini
mbinu zote chafu zimeshindikana.
Waswahili hutumia neno ‘jembe’ wakimaanisha mtu
makini na mtendaji na ndilo jina analositahili Dk Slaa, ni mjenga hoja
mzuri. Mtu wa namna hii hata kama utamfanyia fitina, chuki, mizengwe,
hujuma ni kama kupoteza muda tu kwa sababu anajifahamu. Kwa mantiki hii,
Dk Slaa ni kiongozi mwenye msimamo thabiti na anatetea kile anachokijua
kwa nguvu na uwezo wake wote.
DK Slaa aliwahi kudai kuwa katika uchaguzi wa
mwaka 2010, aliporwa ushindi. Kulikuwa na madai kuwa baadhi ya viongozi
wa dini walikwenda kumwona ili kumtuliza asiitishe maandamano ya kudai
ushindi kama alivyofanya Raila Odinga nchini Kenya mwaka 2007.
Swali, kwa nini Dk Slaa alirudia tamko hilo mbele
ya wageni mbalimbali wakiwa mabalozi wa nchi za nje? Alitaka kufikisha
ujumbe gani? Watu makini hawakurupuki bali wanapangilia mambo yao.
Kama ni sifa za uongozi, basi Dk Slaa hababaishi.
Ni kiongozi mwenye muono, yaani ile hali ya kuweza kuona anakwenda wapi
na wengine kumfuata.
Tanzania ya leo imepoteza mwelekeo kiasi cha kulinganisha na meli isiyo na nahodha.
Tanzania ya sasa tunahitaji kiongozi atakayerudisha imani ya wananchi.
Leo Watanzania wengi wamechoka na Utanzania kwa
sababu ya mateso, hujuma, unyanyasaji, vitisho, na maovu yanaendelea
kutokea kila kukicha.
Tanzania ya leo inahitaji “Nyerere mpya” au
“Mandela mpya” kiongozi mzalendo mwenye kuwapenda Watanzania kwa moyo
wote, mwenye kulinda amani na utulivu siyo kwa kutumia bunduki, risasi
wala mizinga bali kwa kutumia utawala bora, demokrasia na matumizi bora
ya sheria za nchi katika kutenda haki sawa. Wizi wa mali ya umma,
wakiwamo tembo na wanyamapori wengine ni lazima walindwe kwa nguvu na
uwezo wote.
Je, kiongozi kama huyu atapatikana kweli? Mungu si
athumani basi ametuletea Dk Slaa ili aweze kuongoza ukombozi wa pili
kwa Watanzania wanaoteseka.
Watanzania mmeshuhudia sasa namna watawala
walivyoshindwa kuwaletea Katiba mpya inayotokana na mawazo ya wengi.
Wameamua kuchakachua mawazo ya wengi kuwaletea katiba yao.
Hii ni alama wazi ya dharau kwa wananchi na ubabe
uliopitiliza na hivi dawa yake ni kuungana na kuipumzisha ili kuwapa
nafasi viongozi na chama kitakachoweza kutuletea Katiba Bora.
Mungu wabariki Watanzania. Tutaonane wiki ijayo panapo majaliwa katika tafakari mpya.Source:mwananchi
Post a Comment