Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akifafanua
jambo mbele ya ujumbe kutoka Wizara ya Uchukuzi pamoja na Mamlaka ya
Bandari jana. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe.
Dar es
Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeitaka
menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kurejesha nyongeza ya
fedha zote za malipo ya safari ilizowalipa watendaji wake tangu mwaka
2011, baada ya kubainika kuwa zililipwa bila kuidhinishwa na Msajili wa
Hazina.
Ukaguzi
maalumu uliofanywa katika mamlaka hiyo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2011/12, unaonyesha kuwa TPA iliomba
nyongeza ya malipo ya safari lakini kabla ya kupewa kibali na Msajili wa
Hazina, ilianza kuwalipa watendaji wake nyongeza hiyo.
Msajili wa
Hazina ametoa kibali cha nyongeza ya malipo hayo ya safari Januari 2,
mwaka huu na kwa takriban miaka minne mamlaka hiyo imefanya malipo bila
kupewa kibali na Serikali.
Mwenyekiti
wa Kamati ya PAC, Zitto Kabwe alisema malipo ya safari kwa wafanyakazi
wa ngazi za chini wa mamlaka hiyo kwa siku, awali ilikuwa Sh94,000 na
sasa ni Sh123,000 na watendaji wa juu awali ilikuwa Sh270,000 na sasa ni
Sh500,000.
Alisema
malipo kwa safari za nje watendaji wa ngazi za chini kwa siku, awali
walikuwa wakilipwa Dola 296 za Marekani na wa ngazi za juu Dola 600 na
kwa sasa wanalipwa Dola 800.
“Tunataka
mrejeshe fedha hizi tangu mlipoanza kuzilipa mwaka 2011 maana mlifanya
makosa kwani mmelipa bila kupewa idhini na Msajili wa Hazina,” alisema
Zitto na kuongeza: “Wote ambao mmewalipa mnatakiwa kuwakata katika
mishahara yao.”
Kamati hiyo ilikutana jana na TPA katika ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam kujadili hesabu za mamlaka hiyo kwa mwaka 2011/12.
Akijibu
suala hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPA, Madeni Kipande alisema
kati ya waliolipwa, wapo waliostaafu, kuacha kazi na kufariki dunia,
huku akisisitiza kuwa ukusanyaji wa fedha hizo utakuwa mgumu kwa watu
hao.
Hata hivyo, Zitto alijibu: “Hayo mtayaeleza katika taarifa yenu mtakayotuletea kuhusu urejeshaji wa fedha hizo.”
Katika hatua
nyingine, kamati hiyo iliibana TPA kutokana na kutokuwa na nyaraka za
uthibitisho wa matumizi ya fedha kutokana na kutokuwa na mfumo wa kisasa
wa kutunza kumbukumbu na kuitaka kuwasilisha taarifa hizo haraka.
“Ripoti
inaonyesha kuwa mmetumia Sh6.4 bilioni kwa ajili ya matangazo,
tuliwabana na mmetuletea uthibitisho ila kuna Sh384 milioni matumizi
yake hayaonekani,” alisema mjumbe wa kamati hiyo, Abdul Marombwa.
Awali,
mamlaka hiyo ilieleza kuwa imetumia Sh9.6 bilioni kwa ajili ya mikutano
na kushindwa kuonyesha mchanganuo wa matumizi na baada ya kubanwa ilitoa
nyaraka huku zikiwa na pungufu ya Sh686 milioni.
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Picha na Salim Shao
Post a Comment