Shukrani
Mheshimiwa Makamu wa Rais;
Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Viongozi wa CCM Mkoa;
Viongozi Wenzangu;
Viongozi wa Dini;
Wazee Wangu;
Wananchi Wenzangu;
Nawashukuru
sana wazee wangu wa Dar es Salaam, kwa kukubali mwaliko wangu na kuja
kuzungumza nami siku ya leo. Natambua kuwa taarifa ilikuwa ya muda
mfupi lakini mmeweza kuja kwa wingi kiasi hiki. Naomba radhi kwamba
ilikuwa tukutane Ijumaa lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu
tukaahirisha mpaka leo. Asanteni sana kwa uvumilivu wenu.
Kama
mjuavyo, kila ninapoomba kukutana nanyi ninalo jambo au mambo muhimu
kitaifa ambayo napenda kuzungumza nanyi, na, kwa kupitia kwenu taifa
zima linapata habari. Leo nina mambo mawili.
Wazee Wangu;
Kwanza
kabisa, nataka kurudia kuwashukuru Watanzania wenzangu kwa moyo wenu wa
upendo mliouonyesha kwangu katika kipindi chote cha matibabu yangu
nikiwa nje na hata baada ya kurejea nchini. Kwa kweli nina deni kubwa
kwenu. Lazima nikiri kuwa, salamu zenu na taarifa kwamba watu
wamekuwa wananiombea uponaji wa haraka na uzima zinanipa faraja kubwa na
kunitia moyo. Nadhani zimechangia sana kuifanya afya yangu kuendelea
kuimarika kila kukicha. Bado sijawa “fit” kabisa lakini naendelea
vizuri. Hali yangu ilivyo sasa sivyo ilivyokuwa wiki iliyopita au siku
niliporejea nchini.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Ndugu Wananchi;
Jambo la
kwanza ninalotaka kulizungumzia leo ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliofanyika Jumapili iliyopita tarehe 14 Desemba, 2014 na jana tarehe 21
Desemba, 2014 katika maeneo ambayo uchaguzi huo uliahirishwa. Bila ya
shaka sote tumesikia taarifa ya awali ya zoezi la upigaji kura
iliyotolewa na Mheshimiwa Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, TAMISEMI tarehe 17 Desemba, 2014. Katika taarifa yake hiyo,
Mheshimiwa Waziri alieleza kwamba kwa jumla zoezi limeenda vizuri kwenye
maeneo mengi nchini. Uchaguzi ulifanyika kwa ukamilifu katika
Halmashauri 141 kati ya 162. Katika Halmashauri 21 uchaguzi wake
uliahirishwa na umefanyika jana tarehe 21 Desemba, 2014.
Kwa jumla,
katika maeneo mengi uchaguzi ulifanyika kwa salama na amani na hivyo
kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowapenda kuongoza vijiji
vyao, vitongoji vyao na mitaa yao. Kufanyika kwa uchaguzi huu ni
uthibitisho mwingine wa kuendelea kukomaa kwa demokrasia nchini. Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa wale wote walioshiriki
katika uchaguzi huu kwa maana ya vyama vya siasa na wagombea. Natoa
pongezi maalum kwa walioshinda. Nawaomba sasa wakae chini kutengeneza
mikakati na mipango ya kuwaongoza wananchi wa maeneo yao katika kupata
ufumbuzi wa changamoto za maendeleo na za maisha, zinazowakabili.
Ndugu wananchi;
Katika
taarifa yake hiyo pia, Waziri Hawa Ghasia alielezea masikitiko yake
kuhusu kasoro za uendeshaji wa zoezi zilizojitokeza katika maeneo
mbalimbali. Aidha, aliahidi kuchukua hatua stahiki za kinidhamu dhidi
ya watendaji na viongozi wa Serikali waliosababisha kasoro hizo.
Alifafanua kuwa miongoni mwa hatua zinazoweza kuchukuliwa ni pamoja na
kufukuzwa kazi, kusimamishwa kazi, kushushwa cheo, kukatwa mshahara au
kupewa onyo.
Napenda
kuelezea kufurahishwa kwangu na msimamo huo wa Waziri wa TAMISEMI na
nampongeza kwa hatua alizochukua. Namuunga mkono na namtaka aendelee na
msimamo huo katika kukabili vitendo vya utovu wa nidhamu wa watumishi
wa umma. Lazima kila mtumishi wa umma ajue kuwa asipotimiza ipasavyo
majukumu yake kuna adhabu inayolingana na kosa alilofanya. Isitoshe,
watu hao ndio watakaoendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwakani
wakiwa mawakala na wasaidizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hivyo basi,
kuwajibishwa wale waliozembea katika uchaguzi, itakuwa fundisho kwao na
kwa wengine katika uchaguzi wa mwaka 2015 na chaguzi nyingine zijazo.
Ndugu wananchi;
Kwa upande
wa ghasia, fujo na ugomvi uliotokea wakati wa zoezi la uchaguzi,
nimezungumza na viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi na kuwataka
kuhakikisha kuwa wale wote waliofanya vitendo vya kuvunja sheria
wanatiwa nguvuni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Nimewataka
wasifanye ajizi na watu wa aina hiyo. Hawa ni watu hatari ambao hawana
budi kuchukuliwa hatua thabiti za kuwadhibiti na kuwaadabisha.
Tusipofanya hivyo tunawakatisha tamaa raia wema na watiifu wa sheria.
Aidha, watu wakikamatwa na kuachiliwa muda mfupi baadae, wakati
mwingine hata bila dhamana ya namna yo yote inawachanganya sana watu
wema. Isitoshe tutakuwa tunalea maradhi ya watu wabaya na kuwafanya
waendelee kusumbua jamii. Nimewakumbusha kuwa wasipokuwa wakali sasa
tunaweka mazingira ya hatari ya kuja kutokea mambo mabaya zaidi mwaka
ujao kwenye uchaguzi mkuu.
Sakata la Akaunti ya Tegeta ESCROW
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia si geni masikioni kwenu, nalo ni
sakata la Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Bila ya shaka mtakumbuka kuwa
wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti mwezi Juni, 2014, kulitolewa madai
kuwa fedha zilizokuwemo katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta iliyoko Benki
Kuu zimechotwa kinyemela na mmiliki wa Kampuni ya Pan African Power
Solution (PAP) akishirikiana na Maafisa wa Serikali.
Serikali
iliahidi kufanya mambo mawili. Kwanza, kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa Akaunti hiyo na kwamba
taarifa yake itawasilishwa Bungeni. Na, pili, kumuagiza Mkurugenzi Mkuu
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya
uchunguzi wa mwenendo mzima wa miamala katika Akaunti hiyo na kama kuna
uhalifu wo wote uliopo kwenye mamlaka yake achukue hatua zipasazo kwa
mujibu wa mamlaka na madaraka aliyonayo.
Ndugu Wananchi;
Yote mawili tuliyoahidi tumefanya. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali amefanya ukaguzi wa miamala katika Akaunti ya Escrow ya
Tegeta iliyoko Benki Kuu na taarifa yake ilishawasilishwa Bungeni. Pia
niliagiza taarifa hiyo ichapishwe kwenye magazeti na tovuti ya Serikali
ili watu waweze kuisoma. Agizo hilo nalo limetekelezwa. TAKUKURU
wameendelea na uchunguzi wao na watakapomaliza na kuridhika kuhusu
makosa yaliyofanywa watawafikisha wahusika Mahakamani. Mkurugenzi Mkuu
wa PCCB alifika kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
na kutoa baadhi ya mambo kuhusu suala hili aliyoyaona ni muhimu Kamati
iyajue.
Mambo Manne Makuu
Ndugu Wananchi;
Tarehe 8 Desemba, 2014 nilipoanza kazi baada ya mapumziko ya ugonjwa
nilikabidhiwa taarifa mbalimbali kuhusu sakata hili. Tangu wakati huo
nimekuwa nazisoma pamoja na kuzungumza na watu mbalimbali na kuagiza
nipatiwe ufafanuzi wa mambo mbalimbali kutoka kwa wahusika. Shabaha
yangu ni kuyaelewa vizuri mambo hayo ili niweze kufanya uamuzi ulio
sahihi na wa uhakika. Nimebaini kuwa yapo mambo makuu manne:-
(a) Akaunti ya ESCROW
(b) Miliki ya PAP kwa IPTL
(c) Kodi za Serikali, na
(d) Tuhuma za Rushwa
Akaunti ya ESCROW
Ndugu Wananchi;
Katika Mikataba ya Kununua Umeme (Power Purchase Agreements) ambayo
TANESCO imetiliana sahihi na kampuni binafsi za kuzalisha umeme za IPTL,
SONGAS, SYMBION POWER na AGGRECO, kuna malipo ya namna mbili
yanayofanywa na TANESCO. Kwanza, hulipia umeme ilionunua kutoka kwa
kampuni hizo yaani tozo ya umeme (energy charges). Na, pili hulipia
gharama za uwekezaji uliofanywa na kampuni hizo, yaani tozo ya uwekezaji
(capacity charges). Katika mikataba yote hiyo imekubaliwa kuwa iwapo
kutatokea kutofautiana, au mzozo unaohusu uwekezaji, upo utaratibu wa
usuluhishi. Utaratibu huo unataka kwanza kufanyike mazungumzo,
wakishindwa kuelewana watafute mtu wa kuwashauri na kuwasuluhisha;
wakishindwa kukubaliana wapeleke shauri lao kwenye Kituo (Mahakama) cha
Kimataifa cha Usuluhisi wa Migogoro ya Uwekezaji, (International Centre
for Settlement of Investment Disputes – ICSID) kilichopo London,
Uingereza.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 1998
TANESCO walifikisha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa
Migogoro ya Uwekezaji, London, malalamiko kwamba gharama za uwekezaji za
IPTL ni kubwa mno kuliko kiasi halisi walichowekeza. Mwaka 2001 Kituo
cha Usuluhisi kilifanya uamuzi wa shauri hilo. Madai ya TANESCO
yalikubaliwa kuwa uwekezaji halisi uliofanyika ni Dola za Marekani 127
na siyo Dola milioni 163.17 walizodai IPTL. Kutokana na kupungua huko
kwa gharama za uwekezaji, tozo ya uwekezaji (capacity charges) nayo
ilipunguzwa kutoka Dola za Marekani milioni 3.6 kwa mwezi mpaka Dola za
Marekani milioni 2.6 kwa mwezi. Kituo pia, kilitoa mwongozo kuhusu
ukokotoaji wa tozo hiyo.
Ndugu Wananchi;
Miaka minne
baadaye TANESCO ilianza vuguvugu la kutaka kupata nafuu zaidi. Waliamua
kugomea kulipa tozo ya uwekezaji kwa mkokotoo wa mwaka 2001.
Nimeambiwa kuwa wanasheria wa TANESCO walishauri Shirika hilo lidai
ukokotoaji kiwango cha tozo ya uwekezaji wa IPTL ufanyike kwa kuzingatia
thamani ya hisa walizolipia wawekezaji ambayo ni shilingi 50,000 badala
ya kutumia msingi wa mtaji uliotokana na mkopo wa Dola za Marekani
milioni 38.16 wa wanahisa uliotumiwa na usuluhisho wa kwanza ICSID-1.
Wakati
wakisubiri mchakato wa usuluhishi wa mzozo huu mpya kuanza, pande zote
mbili zilikubaliana kuanzisha Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Tarehe 5
Julai, 2006, akaunti hiyo ikaanzishwa kwa mkataba uliyotiwa sahihi na
IPTL upande mmoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa niaba ya TANESCO
upande mwingine. Aidha, Benki Kuu iliteuliwa kuwa wakala wa kutunza
akaunti hiyo nayo ilitia sahihi.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu
wa mkataba huo, Kampuni ya IPTL iliendelea kupeleka madai ya tozo ya
uwekezaji kwa TANESCO ambayo nayo iliwajibika kulipa madai hayo. Malipo
hayo yalitakiwa kupelekwa kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta tofauti na
ilivyokuwa kabla ambapo yalipelekwa IPTL moja kwa moja. Utaratibu huu
mpya ulikubaliwa kutumika hadi pande mbili zitakapofikia mwafaka kuhusu
kiwango cha ukokotoaji. Kwa upande wa malipo ya gharama ya umeme
(energy charges) TANESCO imeendelea kulipa moja kwa moja kwa IPTL bila
kupitia Akaunti ya Tegeta ESCROW maana hizo hazikuwa na mgogoro.
Ndugu Wananchi;
Kwa miaka
saba tangu tarehe 5 Julai, 2006, akaunti hiyo ilipoanzishwa mpaka tarehe
5 Septemba, 2013, wakati Mahakama Kuu ilipokabidhi shughuli zote za
IPTL kwa PAP, hakuna hatua stahiki zilizochukuliwa kutafuta ufumbuzi wa
mzozo wa tozo ya uwekezaji baina ya ITPL na TANESCO. Pande mbili husika
hazikuwahi kukaa kuzungumza na wala hakuna shauri lililofikishwa kwenye
Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Mogogoro ya Uwekezaji kama
ilivyofanyika mwaka 1998.
Wakati wote huo, TANESCO iliendelea kulipa madai ya tozo ya uwekezaji ya
IPTL na kupeleka malipo hayo kwenye Akaunti ya Escrow. Ulipaji
ulisimama katika kipindi kifupi wakati kampuni ya IPTL ilipowekwa kwenye
ufilisi. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, wakati akaunti hiyo inafungwa
tarehe 20 Novemba, 2013, kulikuwa na fedha taslimu shilingi
8,020,522,330.37; Hatifungani zenye thamani ya shilingi 159,231,370,000
na Dola za Marekani 22,198,544. Fedha zote hizo ni sawa na shilingi
bilioni 202.9.
Ndugu Wananchi;
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, kama TANESCO ingelipa tozo ya uwekezaji ipasavyo,
wakati huo Akaunti hii ingekuwa na shilingi bilioni 306.7. Kwa sababu
ya kutolipa fedha zote ipasavyo, wakati Akaunti inafungwa TANESCO
walikuwa wanadaiwa na IPTL shilingi bilioni 103.8. Kwa mujibu wa
Mkataba wa Mauzo ya Umeme (PPA) malipo yaliyocheleweshwa, yanatozwa riba
ya asilimia mbili ya fedha zote ambazo hazikulipwa kwa wakati. Hivyo
basi, riba iliyotokana na TANESCO kuchelewesha malipo ilikuwa Dola za
Marekani milioni 33.6.
Ni matumaini
yangu kuwa ufafanuzi uliotolewa katika Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali unasaidia kuweka kumbukumbu sawa na sahihi
kuhusu kiasi gani kilichokuwepo kwenye Akaunti ya ESCROW siku uamuzi wa
Mahakama ulipofanya akaunti hiyo ifungwe. Kwa kifupi Taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaeleza kuwa Akaunti
hiyo ilikuwa na shilingi bilioni 202.9 na siyo shilingi bilioni 306.7
kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Fedha za Nani
Ndugu Wananchi;
Ni matumaini yangu pia kwamba maelezo haya kwa kiasi fulani yamesaidia
kutoa jibu kwa swali maarufu la fedha za kwenye akaunti hii ni za nani?
Je ni za umma au za IPTL? Pengine nianze kwa kuelezea Akaunti ya ESCROW
ni nini? Akaunti ya ESCROW ni tofauti na akaunti nyingine tunazozijua
katika Benki zetu ambazo mtu anaweka fedha zake. Kama tujuavyo, katika
Benki zipo Akaunti za aina tatu ambazo wengi tunazifahamu na kuzitumia
yaani Akaunti ya Akiba (Savings Account), Akaunti ya Hundi (Current
Account) na Akaunti ya Muda Maalum (Fixed Deposit Account). Akaunti ya
Escrow ni akaunti maalum inayoanzishwa kwa ajili ya kufanya kazi maalum,
kwa masharti maalum na kazi hiyo ikiisha akaunti yenyewe hufungwa.
Akaunti hiyo husimamiwa na wakala aliyeteuliwa kwa makubaliano ya wale
wanaofungua akaunti hiyo. Wakala ndiye mwenye jukumu la kusimamia
akaunti na kumlipa mwenye fedha wakati ukifika. Kwa akaunti ya Escrow
ya Tegeta pande mbili husika zilikubaliana kuwa Benki Kuu ndiyo iwe
Wakala. Ni muhimu kujua kuwa akaunti hiyo ingeweza kufunguliwa kwenye
Benki yoyote siyo lazima BoT.
Akaunti ya
Tegeta ESCROW ilifunguliwa BoT mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha
za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges) zilizokuwa zinalipwa
na TANESCO kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa ambaye ni IPTL. Kabla
ya hapo TANESCO ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa IPTL. Kama
nilivyokwishasema, awali ilifanyika hivyo ili kutoa nafasi kwa pande
hizo mbili husika kumaliza tofauti zao kuhusu kiwango cha tozo ya
uwekezaji ya IPTL.
Kimsingi
basi, fedha hizi ni za IPTL kwani ndiye mlipwaji na ni malipo yanatokana
na madai ya IPTL kwa TANESCO kuhusu tozo ya uwekezaji. Hata hivyo, kwa
mujibu wa CAG, inawezekana katika fedha hizo kuna fedha za umma. Hi ni
kwa namna mbili.
Kwanza, kama
mgogoro baina ya TANESCO na IPTL ungetatuliwa na kiwango cha tozo ya
uwekezaji kupungua kama ilivyofanyika mwaka 2001 katika ICSID-1 na kama
pande mbili husika zingekubaliana au kuagizwa kuwa punguzo hilo lianze
kuhesabiwa tangu tarehe ilipofunguliwa Akaunti hiyo (tarehe 5 Julai,
2006), basi kungekuwepo pesa za kurejeshwa TANESCO. Maadamu hili
halikufanyika mpaka Mahakama ilipofanya uamuzi uliosababisha akaunti
hiyo kufungwa. Katika mazingira hayo fedha zote zinakuwa ni za IPTL
maana hakuna madai ya TANESCO.
Ndugu Wananchi;
Namna ya
pili ni ile ambapo katika fedha hizi kunaweza kuwepo fedha za umma na
iwapo kuna kodi za Serikali ambazo hazijalipwa. Kwa mujibu wa Taarifa
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuthibitishwa na
TRA ni kwamba kulikuwa na kodi ya VAT ambayo haikulipwa. Nimeambiwa
kuwa TANESCO ndiyo ilikuwa na wajibu wa kukata kodi hizo kabla ya kulipa
madai ya IPTL lakini kwa baadhi ya malipo haikufanyika hivyo. Hivi IPTL
inastahili kudaiwa kodi ya Serikali? Kwa mujibu wa tathmini
iliyofanywa, kodi inayotakiwa kulipwa na IPTL ni shilingi bilioni 21.7.
IPTL wameshapelekewa madai na TRA, na IPTL wamekubali kulipa.
Katika
ukaguzi wa Hesabu za TANESCO za mwaka 2012, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali aliwaelekeza TANESCO kuacha kuhesabu fedha zilizopo
kwenye Akaunti ya ESCROW kama ni fedha zao. CAG aliwaambia TANESCO
kwamba fedha hizo si zao.
Maagizo hayo ya CAG yanasomeka kama ifuatavyo:
“As a
result, the deposit balance in Escrow account does not meet the
definition of an asset of the Company and therefore an adjustment has
been made to de-recognize the asset and related liability to the tune of
the amounts available in the Escrow account”
Kwa tafsiri
yake ni kuwa: “Hivyo basi, fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya Escrow
hazina sifa ya kutafsiriwa kama ni mali ya kampuni (TANESCO) hivyo,
marekebisho yamefanywa ili kutotambua mali na madeni yanayohusu fedha
hizo kwa kiasi cha fedha zilizopo kwenye akaunti ya Escrow.”
Kutokana na
maelezo haya ni dhahiri kwamba, fedha zilizokuwa kwenye Escrow siyo za
TANESCO na hazikupaswa kuingizwa kwenye vitabu vya TANESCO kama mali
yake.
Chimbuko la Sakata
Wazee Wangu;
Chimbuko la
kadhia yote hii Bungeni na kwenye jamii ni uamuzi wa tarehe 5 Septemba,
2013, wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kuitambua PAP kuwa mmiliki halali
wa IPTL na kuagiza Mfilisi akabidhi shughuli zote za IPTL kwa PAP.
Katika utekelezaji wa uamuzi huo wa Mahakama Kuu ukazuka mjadala mkali
kuhusu fedha zilizomo kwenye akaunti ya ESCROW kukabidhiwa kwa PAP.
Kwanza kabisa mjadala ulikuwa ndani ya Serikali miongoni mwa viongozi
na watendaji wa Wizara na Taasisi zinazohusika moja kwa moja na akaunti
hiyo. Hizi ni Wizara ya Nishati na Madini, TANESCO na Benki Kuu.
Viongozi na Watendaji husika walikuwa wanajiuliza na kuuliza kama
walipe au wasilipe. Walipotaka ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
wakaelekezwa watekeleze uamuzi wa Mahakama Kuu. Alisema uko sawa na
hauna matatizo. Halikadhalika, Benki Kuu walipoulizia kuhusu kodi za
Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza kuwa hakuna kodi ya
kulipwa.
Kwa
kuzingatia ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, malipo yakafanyika
kwa IPTL tena bila ya kodi kulipwa. Baada ya malipo kufanywa ndipo
mjadala huo ukahamia katika jamii na Bunge na kugeuka kuwa kadhia kubwa
iliyochukua sura ya kashfa yenye dalili za rushwa na wizi.
Uamuzi Unaotiliwa Shaka
Wazee Wangu na Ndugu Wananchi;
Kwa jumla
uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu akaunti ya Escrow, ushauri wa Mwanasheria
Mkuu kwa Serikali wa kuelekeza uamuzi huo utekelezwe na viongozi wa
Serikali kutekeleza ushauri huo vimetiliwa shaka. Umeonekana kuwa
haukuwa uamuzi sahihi na kwamba umeitia hasara nchi. Isitoshe uamuzi
huo umeibua hisia za kuwepo harufu na vitendo vya rushwa. Wapo waliosema
si bure iko namna! Wapo waliotaja majina na watu wanaodai wamepata
mgao wa Escrow tena wengine wamechukua fedha kwa viroba, sandarusi na
rumbesa. Bahati mbaya sana katika mjadala ilijengeka dhana isiyokuwa
sahihi kwamba jambo hili lilianzishwa na Maafisa hao wa Serikali kwa nia
ya kujinufaisha wao binafsi. Ukweli ni kwamba uamuzi ulifanywa na
Mahakama Kuu na kwenye Serikali ilikuwa utekelezaji wa amri hiyo.
Wazee Wangu;
Nilipokutana
na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata maoni yake kuhusu
kadhia hii ameendelea kusema alichosema Bungeni kuwa hakukosea katika
ushauri wake na wala Mahakama haikufanya makosa. Hivyo basi, hakuona
sababu ya kwenda Mahakamani kuomba marekebisho ya uamuzi wa Mahakama
kuhusu fedha zilizokuwepo kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta kukabidhiwa
kampuni ya PAP mmiliki wa IPTL. Vilevile haoni kama kuna hasara yo
yote ambayo nchi imepata kwa sababu fedha zile ni za IPTL na imelipwa
IPTL.
Akifafanua,
alisema kuwa akaunti ya Escrow ilianzishwa kwa ajili ya kutunza fedha za
malipo ya tozo ya uwekezaji kwa IPTL yaliyokuwa yanafanywa na TANESCO.
Kabla ya mzozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo na kuanzishwa kwa akaunti
ya Escrow ya Tegeta, TANESCO ilikuwa inalipa tozo ya uwekezaji moja kwa
moja kwa IPTL. Baada ya kutokea mzozo na akaunti kuanzishwa mambo
mawili hayakubadilika. Kwanza kwamba IPTL haikuacha kupeleka madai ya
tozo ya uwekezaji kwa TANESCO. Na, pili, kwamba TANESCO haikuacha
kulipa madai hayo. Mdai na mdaiwa hawakubadilika. Kuwepo kwa akaunti
ya Escrow hakubadili mwenye fedha zake. Akaunti hiyo iliundwa kuhifadhi
fedha za IPTL wakati suluhu inatafutwa kuhusu kiwango cha tozo.
Matumaini ni kwamba kama kiwango kitapunguzwa, TANESCO inaweza kupata
nafuu ya malipo.
Kuhusu
uamuzi wa Mahakama Kuu kuruhusu IPTL ilipwe fedha za akaunti ya Escrow,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema ni uamuzi sahihi na wala taifa
halikupata hasara kwa sababu pesa zimelipwa IPTL na siyo mtu mwingine.
Isitoshe anaona uamuzi wa Mahakama umeisaidia TANESCO kutua mzigo
mkubwa iliyokuwa nao kwa miaka saba.
Kama mjuavyo, akaunti ya Escrow ilianzishwa kuhifadhi pesa za malipo ya
tozo ya uwekezaji ya IPTL. Ilianzishwa kwa matumaini kuwa TANESCO
watapata nafuu ya tozo ya uwekezaji. Lakini, hapakuwahi kufanyika
mazungumzo baina ya TANESCO na IPTL kuhusu jambo hilo na wala suala hilo
halijafikishwa ICSID. Haikuweza kufanyika hivyo kwa sababu washauri wa
kisheria wa TANESCO hawajafanya hivyo. Wapo wanaodai kuwa hawafanyi
hivyo kwa sababu hakuna sababu mpya zinazoweza kupatikana kuifanya ICSID
ibadili uamuzi wake wa 2001 kuhusu kiasi cha tozo na namna ya
ukokotoaji wake.
Matokeo yake ni TANESCO kuwa na akaunti ya Escrow ambayo mwisho wake
haujulikani. TANESCO inaendelea kudaiwa na IPTL tozo ya uwekezaji na
kulazimika kulipa kwenye akaunti hiyo. Kwa masharti ya akaunti ya
Escrow wanaposhindwa kulipa wanatozwa riba. Kwa mujibu wa taarifa ya
CAG mpaka tarehe 20 Novemba, 2013, TANESCO ilikuwa inadaiwa shilingi
bilioni 103.8ambazo hawajalipa kwenye akaunti ya Escrow na riba ya Dola
za Marekani milioni 33. Kwa sababu hiyo basi uamuzi wa kufunga Akaunti
ya Tegeta Escrow unalipatia unafuu TANESCO dhidi ya kulimbikiza madeni
na riba.
Kwa upande wa kodi za Serikali ambazo hazikulipwa, Mheshimiwa Jaji
Werema alisema yeye alitoa ushauri tu. Hata hivyo, kama mamlaka husika
inaona zipo kodi zinazostahili kulipwa izidai. Hakuna kilichopotea kwa
sababu anayedai, yaani TRA yupo, na mdaiwa yupo, IPTL.
Uamuzi wa ICSID II Kuhusu Tozo ya Uwekezaji
Wazee Wangu;
Yalitolewa
mawazo kuwa kama fedha za akaunti ya Tegeta Escrow zingelipwa baada ya
uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji
(ICSID II) kutoa uamuzi wake, TANESCO ingepata nafuu ya kupungua kwa
tozo ya uwekezaji. Kuhusu jambo hilo nimeambiwa kwamba kuna mambo
mawili ya msingi. Kwanza kwamba Mahakama hiyo haikutoa viwango vipya
vya tozo kama ilivyofanya mwaka 2001 kwenye ICSID–I. Haikubadili
mwongozo wa ukokotoaji wa tozo. Imesema madai yanaweza kuzungumzwa na
kusisitiza kuwa katika mazungumzo hayo TANESCO watambue kwamba wanahisa
waliwekeza mtaji wao binafsi wakati wa kununua mtambo na pia walikopa
madeni, na kwamba kiasi cha fedha walichowekeza kilitakiwa kiwe na
kiwango cha juu zaidi cha faida.
Jambo la
pili ni kwamba, shauri hili la pili la ICSIDI II halikuihusisha kampuni
ya IPTL mwenye Mkataba wa Kuuza Umeme na TANESCO na siyo Benki ya
Standard Charterd. IPTL wameweka pingamizi la utekelezaji wa uamuzi wa
shauri hilo hapa nchini, hivyo inakuwa vigumu kwa TANESCO kufanya
mazungumzo kwa msingi wa shauri hilo.
Kinga Dhidi ya Madai
Wakati wa
kufunga akaunti ya Escrow, upande wa Serikali ulielezea hofu yake ya
uwezekano wa siku za usoni mtu kudai tena kulipwa fedha hizi hizi
ilizolipwa PAP. Nimeambiwa kuwa suala hilo haliwezi kutokea kwani
limetengenezewa wigo imara wa kimkataba kuzuia. PAP imetiliana sahihi
na Serikali kwamba iwapo kutatokea mdai yo yote PAP itawajibika kulipa.
Mashaka ya Miliki ya PAP kwa IPTL
Ndugu Wananchi;
Hofu nyingine kuhusu uwezekano wa Serikali kupata hasara ni yale madai
kuwa huenda miliki ya PAP kwa asilimia 70 za hisa za IPTL zilizokuwa za
kampuni ya Mechmar Berhard ya Malaysia siyo halali. Pale mwanzoni
ilidaiwa kuwa kampuni ya Mechmar ilipouza hisa zake kwa kampuni ya Piper
Link ya British Virgin Islands ilikuwa chini ya mchakato wa ufilisi
kule Malaysia. Kama ingekuwa hivyo, kisheria mtu hawezi kuuza hisa zake
akiwa kwenye mazingira hayo. Katika uchunguzi wa CAG alieleza kuwa
amethibitisha kwamba madai hayo si kweli, Mechmar walipouza hisa zao
tarehe 9 Septemba, 2010 kampuni haikuwa kwenye ufilisi. Iliingia kwenye
mchakato wa ufilisi mwaka 2012.
Lakini kwa upande wa kampuni ya Piper Link ya Uingereza inasemekana
iliuza hisa hizo baada ya kuwa wamepokea amri ya Mahakama ya Malkia ya
BVI kuizuia isiuze hisa hizo. Je ni kweli? Imefanyika hivyo? Kama ni
kweli je PAP waliponunua hisa hizo walijua kama kuna zuio au hapana?
Kama walijua basi na wao ni sehemu ya njama za kufanya udanganyifu.
Kama hawakuwa wamejua basi wametapeliwa. Nimeagiza uchunguzi wa kina
ufanyike kupata ukweli. Natambua hivi sasa Mahakamani zipo kesi
zinazohoji uhalali wa PAP kumiliki asilimia 70 za hisa za Mechmar
Berhad. Uchunguzi wetu hautaingilia mchakato huo lakini unaipa Serikali
fursa nzuri ya kuchukua hatua zipasazo kuhusu suala hili lenye mjadala
mkubwa.
Jambo lingine muhimu ambalo limeleta matatizo kwa Mahakama zetu nchini
na BRELA ni uuzaji wa hisa za IPTL au kuwekwa rehani hisa hizo bila ya
uamuzi huo kusajiliwa BRELA na kwenye Mahakama zetu. Sheria zetu
ambazo ndizo za nchi ya Jumuiya ya Madola kama ilivyo kwa Hong Kong,
Malaysia, na BVI, inaitaka kampuni ya Piper Link ya BVI iliponunua hisa
za Mechmar katika IPTL kusajili BRELA ununuzi huo. Hali kadhalika,
inaitaka SCB ya Hong Kong na kupata amri ya Mahakama kuzuia deni la
Mechmar na kuwekwa dhamana ya hisa za Mechmar katika IPTL. Piper Link
isiuze hisa 70 za Mechmar katika IPTL. Walitakiwa wasajili na BRELA na
Mahakama yetu. Kutokufanya hivyo ndiko kunazua maneno mengi na mzozo
kuhusu uuzaji wa hisa hizo kwa PAP. Kwa SCB wanapata usumbufu wa kudai
madeni yao IPTL kwa sababu hiyo hiyo. Uchunguzi utakaofanyika utapata
ukweli wa yote kwa uhakika.
Ndugu Wananchi;
Taarifa niliyopewa wakati najiandaa kuzungumza nanyi ni kuwa katika
Mahakama zetu nchini kuna mashauri yahusuyo miliki ya PAP ya hisa 70
zilizokuwa za Mechmar katika IPTL na yapo mashauri yahusuyo PAP kupewa
fedha za akaunti ya Escrow. Zipo pia nyingine za masuala mbalimbali
yakiwemo mashauri yaliyofunguliwa na PAP dhidi ya watu, na makampuni
binafsi na vyombo vya Serikali. Naamini uamuzi wa Mahakama zetu utatoa
majibu kwa masuala yote hayo.
Pamoja na hayo yatakayokuwa yanaendelea Mahakamani, Serikali itaendelea
kufanya uchunguzi wake na kuamua namna ya kushughulikia taarifa
zitakazopatikana ili nayo iweze kwenda Mahakamani itakapolazimu kufanya
hivyo.
Jambo lingine muhimu nataka uchunguzi wa kina ufanyike ni kujua nani ni
nani katika uuzaji na ununuzi wa hisa za Mechmar. Hususan nataka tujue
kwa ukweli na uhakika hisa hizo zimeuzwa kwa bei gani. Je, ni kweli
gharama zinazosemwa ndizo zenyewe? Nataka kuthibitisha ukweli huo ili
tujue kodi yetu ya ongezeko la mtaji (Capital Gains Tax) inayostahili
kulipwa Tanzania ni kiasi gani? Je kiasi gani kimelipwa na kipi
hakijalipwa ili kidaiwe?
Tuhuma za Kuwepo kwa Harufu ya Rushwa
Wazee Wangu;
Kumekuwepo na tuhuma za vitendo vya rushwa katika mchakato mzima wa
kufunga akaunti ya Escrow na kukabidhi fedha hizo kwa kampuni ya PAP.
Halikadhalika, kumekuwepo na hisia hizo hizo kwa upande wa jinsi kampuni
ya VIP Engineering and Marketing ilivyotumia pesa zake zilizoko kwenye
Benki ya Mkombozi. Yamesemwa mengi sana na mmeyasikia na kuyasoma.
Rushwa ni kosa la kijinai ambalo kwa Serikali yetu ni kosa ambalo ni
vigumu kulivumilia wala kulifumbia macho. Mara baada ya kupata fununu
za uwezekano wa vitendo hivyo kufuatia taarifa ya awali ya CAG ya
kwenda kukagua miamala, niliagiza taarifa husika zifikishwe kwenye
Taasisi ya Kupamba na Kuzuia Rushwa (PCCB) kwa uchunguzi zaidi.
Naambiwa taarifa hizo zimefika na kazi ya uchunguzi inaendelea. Tayari
watu kadhaa wamehojiwa na wengine wanaendelea kuhojiwa. Wakati
nawasihi wananchi kuvuta subira ili tuwape nafasi PCCB wakamilishe kwa
ufanisi wa hali ya juu kazi yao waliyokwishaianza, nawaomba PCCB
waongeze kasi ya uchunguzi. Napenda kufafanua kwamba kwa upande wa
miamala iliyotoka katika akaunti ya kampuni ya VIP Engineering and
Marketing ya Ndugu James Rugemalila, Serikali inashughulika na watumishi
wa umma kwa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma, maana
suala lao ni la kimaadili. Hatuwahoji wasiokuwa watumishi wa umma.
Maazimio ya Bunge
Ndugu Viongozi;
Wazee Wangu;
Ndugu Wananchi;
Niliona nianze kwa kutoa maelezo hayo ya utangulizi kabla ya
kuyazungumzia maazimio ya Bunge. Serikali imepokea maazimio hayo ya
Bunge na kuyafanyia kazi kwa ajili ya utekelezaji wake. Nawapongeza
Wabunge wetu kwa moyo waliouonesha wa kuchukia maovu na kutaka
yashughulikiwe ipasavyo. Napenda kuwahakikishia kuwa niko pamoja nao.
Nampongeza Mheshimiwa Anna Makinda, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job
Ndugai, Naibu Spika na Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Mussa Zungu kwa
uongozi wao mahiri. Hakika haikuwa kazi rahisi, lakini chini ya uongozi
wao mambo yameisha salama na tumepata maazimio nane yanayozungumzika na
kutekelezeka. Nawashukuru na kuwapongeza sana Wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya uongozi wa
Mheshimiwa Zitto Kabwe na Mheshimiwa Deo Filikunjombe na pia Wajumbe
waliounda Kamati ya Mapendekezo kwa kufikia mwafaka wa mapendekezo haya 8
ambayo yaliazimiwa na Bunge.
Mwisho
lakini si ya mwisho kwa umuhimu, nawapongeza Wabunge wote kwa michango
yao mizuri. Jambo lililonifurahisha sana ni ushirikiano wa Wabunge wa
kambi zote katika kutafuta ufumbuzi wa suala hili muhimu,. Hivi ndivyo
inavyotakiwa Bunge liwe. Kwa kweli lazima nieleze mshangao wangu
niliposikia kambi ya upinzani ikijaribu kufanya maamuzi yale ni yao wao
na wenzao hawamo. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ina
Wajumbe19wa CCM na wa Upinzani 5. Bunge lina Wabunge wa CCM asilimia 74
na wa upinzani asilimia 26. Hivi kama ni yao wao pekee na wa upande wa
CCM wangepinga yangekuwa? Yasingefika po pote, yangefia kwenye Kamati.
Huku ni kutafuta umaarufu kwa mgongo wa wengine. Na, Wabunge wengi wa
CCM na nyie semeni msikike kwa uamuzi mliyofanya wote.
Napenda kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini hatuna upungufu
wa dhamira ya kutekeleza yale maazimio yanayoangukia katika dhamana
yetu. Napenda kuainisha mtazamo na mwelekeo wa Serikali katika
utekelezaji wa maazimio hayo manane kama ifuatavyo:-
Azimio la kwanza:
Serikali iangalie uwezekano wa kuchukua mitambo ya kufua umeme ya IPTL
na kuimilikisha kwa TANESCO kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Pendekezo
tumelipokea, ni jambo linalowezekana kufanya. Hata hivyo, tunapopima
ujumbe tunaoupeleka kwa jumuiya ya wawekezaji tunachelea kuwa inaweza
kuleta hofu na kuwatisha wawekezaji waliopo na wajao. Nalisema hivyo
kwa sababu sisi tuna historia ya kutaifisha mali za kamapuni binafsi.
Hofu hiyo bado ipo. Tukichukua mitambo hii tunaweza kurudisha hofu za
kurudi tulikokuwa na kukimbiza mitaji tunayohitaji kwa uchumi kukua na
nchi kupata maendeleo. Nashauri tuendelee kuyapatia ufumbuzi matatizo
ya IPTL kila tunapoyabaini. Aidha, Mahakama imetusaidia sana kwa
kuamuru mitambo ya IPTL ibadilishwe ili itumie gesi asilia na kutoza bei
ya umeme isiyozidi senti nane za Marekani. Tuyafuatiliye haya kwanza.
Azimio la Pili: Azimio
hilo linazungumzia kuhusu uwazi wa Mikataba linasomeka ifuatavyo:
“Bunge limeazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge
mapema iwezekavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Bunge la
Bajeti. Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya
mikataba ya umeme”.
Azimio hili
tumelipokea na tunaangalia namna bora ya kulitekeleza ili kuweza kuua
ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza, kuitikia kilio cha muda mrefu
kuhusu uwazi katika mikataba ambayo Serikali inaingia na wawekezaji; na
pili kuhakikisha usiri wa mikataba hiyo ambayo ni haki ya wawekezaji hao
dhidi ya washindani wao inazingatiwa. Serikali na Bunge tutakaa chini
hivi punde kutafuta namna bora ya kisheria na tutafanya hivyo kwa
kujifunza pia kutokana na uzoefu wa nchi ambazo zina utaratibu wa aina
hii.
Azimio la Tatu:
Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba TAKUKURU, Jeshi la Polisi na
vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahili kwa
mujibu wa sheria za nchi yetu dhidi ya watu waliotajwa kwenye taarifa
maalum ya Kamati husika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na
miamala ya Akaunti ya ESCROW, na watu wengine watakaogundulika kufuatia
uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusu kuhusika kwao katika vitendo
hivyo vya jinai”
Vyombo husika vimekwishaagizwa kufanya hivyo na kazi imeanza na
inaendelea. Ikiwa wapo watu wenye makosa hatua zitachukuliwa kwa mujibu
wa sheria.
Azimio la nne:
Linasomeka, “Kamati za Bunge kuwavua nyadhifa zao wenyeviti wa Kamati
za Bunge waliotajwa kupewa fedha na kampuni ya VIP Engineering kabla ya
kikao kijacho cha Bunge”
Azimio hilo liko chini ya mamlaka ya Bunge lenyewe. Nawaachia wao waamue.
Azimio la Tano:
Linasomeka; “Bunge linaazimia kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza utovu wa maadili
dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa
Mahakama Kuu ya Tanzania”
Azimio hili nimelipokea, tumelijadili hata hivyo, itabidi tufuate
utaratibu wa kikatiba na kisheria wa kushughulikia masuala ya namna
hiyo. Inatakiwa suala kama hili lianzie kwenye Mhimili wa Mahakama
yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge. Tume ya Mahakama ndiyo yenye mamlaka
ya kumtaka Rais aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji yeyote
pale inaporidhika kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo.
Nashauri suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie
atakavyoona inafaa.
Azimio la Sita: “Bunge
linaazimia kwamba mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja
Stanbic Bank Ltd. na benki yeyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa
mamlaka ya uchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa
katika akaunti ya ESCROW kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa
fedha haramu (Institutions of money laundering concerns).
Pendekezo la Bunge ni zuri kwamba mamlaka husika na udhibiti wa vitendo
vya utakatishaji fedha vifanye uchunguzi kwa mujibu wa Sheria. Serikali
imelipokea na mamlaka husika yaani Financial Intelligence Units
kulishughulikia. Naamini wameshaaza, tuwape muda watimize wajibu wao
kwa mujibu wa sheria.
Azimio la Saba:
“Bunge liliazimia kwamba Serikali iandae, na kuwasilisha Muswada wa
Marekebisho ya Sheria iliyounda TAKUKURU kwa lengo la kuanzishwa Taasisi
mahsusi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa
kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi,
kijamii na kisiasa.
Kazi ya kufanya mageuzi katika TAKUKURU inaendelea. Tayari Sheria
mbalimbali zimetungwa ikiwa ni pamoja na Sheria Mpya ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa ya mwaka 2008, Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Fedha
Haramu ya mwaka 1991 ambazo zote zinaweka utaratibu wa kushughulikia
vitendo vya rushwa. Tutaendelea kuziboresha sheria hizo kwa kadri
itakavyohitajika. Kazi iliyopo mbele yetu ni kuimarisha usimamizi wa
sheria hizo. Jambo hilo nalo litazingatiwa katika maboresho hayo. Ni
dhamira yangu na ya Serikali ninayoiongoza kupambana na kushinda vita
dhidi ya rushwa. Kwa hiyo tuko tayari kulifanyia kazi pendekezo lolote
linaloimarisha dhamira yetu hii njema.
Azimio la nane:
“Bunge linaazimia kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi
na Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya
TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi
wao.
Azimio hili ndilo Azimio ambalo limevuta hisia za watu wengi, na pengine
ndilo ambalo utekelezaji wake unasubiriwa kwa hamu. Utekeelzaji wake
umeanza. Kwanza, ni kuhusu Bodi ya TANESCO, tumeanza mchakato wa
kuunda Bodi mpya kwani iliyopo imemaliza muda wake. Kuhusu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini, kwa vile ni mtumishi wa umma
anatawaliwa na Sheria na Kanuni za Utumishi wa umma, hivyo
nimeshaelekeza Mamlaka kuchunguza tuhuma zake na hatimaye ikibainika ana
makosa hatua za kinidhamu zitachukuliwa. Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ameshajiuzulu. Tumelitafakari suala la Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi la kupokea fedha kutoka VIP Engineering and
Marketing ambazo kwa maelezo yake ni kwa ajili ya shule anayoimiliki na
kuiendesha. Mwenyewe ameeleza wazi kupitia vyombo vya habari. Pamoja na
hayo yapo mambo ya msingi kimaadili ambayo hayakuzingatiwa, hivyo
tumemwomba atupishe tuteue mwingine. Kuhusu Prof. Muhongo nimemuweka
kiporo, kuna uchunguzi niliagiza ufanywe na vyombo vyetu bado nasubiri
taarifa hiyo ili nifanye uamuzi ndani ya siku chache zijazo.
Hitimisho
Wazee Wangu;
Nawashukuruni kwa kunisikiliza.
Post a Comment