0

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi

BARAZA Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM, limetaka mchakato wa kumpata mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani, uanze mapema.


Limetaka chama kitenge kanda sita, ambazo waombaji watakwenda kuzungumza na wanachama na wadau mbalimbali, kupima nguvu ya wagombea.

Hayo yalibainishwa jana kwenye Maazimio ya Baraza hilo, kabla ya kufunga kikao chake mjini Dodoma, ambapo pia walitaka kubadilishwa utaratibu wa kura za maoni.

Pia, UVCCM walisema Katiba Iliyopendekezwa ni lazima ipite kwa kishindo kizito katika kura ya maoni itakayoitishwa Aprili mwakani.

Katika maazimio hayo, UVCCM wametaka kuanza mapema mchakato wa kumpata mgombea wa Urais, kwani jambo hilo pia litatoa nafasi kwa wagombea kufahamika kwa umaarufu maradufu zaidi ya kuliko wale wa upinzani.

“Hili likifanyika wagombea wetu watafahamika zaidi na wanachama na Watanzania kwa ujumla na chama kigharimie matangazo ya moja kwa moja kwenye vituo vya Televisheni na redio,” alisema.

Pia, baraza hilo limeazimia kuishauri CCM kuangalia na kubadilisha utaratibu wa kura za maoni kwa kubadilisha taratibu zake ili unapofika wakati wa uchaguzi kwa vikao vya ngazi husika katika maamuzi kuchuja kwanza majina ya wale wote waliogombea nafasi za uongozi na kubakiza majina machache kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni.

Walisema hilo litafanya kuwa na makundi machache na hata kuwaunganisha tena itakuwa rahisi kuliko hivi sasa.

Akifunga mkutano huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliwataka vijana kujihadhari wakati wa kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Rais kikikaribia.

Alisema UVCCM ina kazi kubwa kuhakikisha CCM inapata ushindi katika uchaguzi mkuu ujao ili chama kiendelee kuongoza.

“Kuanzia sasa mjipange vizuri kuhamasisha wanachama pamoja na wananchi wote kuipigia kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa kazi hii inahitaji uongozi wa busara ambao naamini upo ndani ya UVCCM, siku zote CCM ushindi ni lazima,” alisema.

Maazimio mengine Viongozi wa CCM wa ngazi zote na Serikali kufanya ziara za kikazi mara kwa mara na kuacha kukaa maofisini ili kubaini na kutatua kero za wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi, ukosefu wa masoko ya uhakika kwa wakulima, unyanyasaji usio wa lazima unaofanywa na mgambo.

Pia Serikali kuendelea kubuni mpango wa haraka ili kuweza kushughulikia tatizo la ajira kwa kushirikisha watu mbalimbali kama wataalamu waliopo kwenye vyuo, wafanyabiashara na hata wanasiasa makundi ya vijana, viongozi wa dini, wakulima na wavuvi ili waje na mpango wa taifa wa tatizo la ajira na utekelezaji wake kwa kipindi cha muda mrefu na mfupi.

Aidha, vijana wote wa Tanzania wametakiwa kuona na kutambua fursa kwa ajili ya manufaa yao kwa lengo la kujikomboa kiuchumi.

Pia, baraza hilo limelipongeza Bunge Maalumu la Katiba kwa kulipatia Taifa Katiba Inayopendekezwa yenye maslahi kwa makundi yote na kuwataka wananchi kuwa makini wakati wa kuelekea kura za maoni, kwani mijadala mbalimbali isitumike kuwagawa na kuvunja amani ya nchi na kila mtu mwenye dhamana afuate utaratibu na sheria zilizopo.

Pia, baraza hilo liliitaka Serikali kuanzisha mfuko maalumu ambapo asilimia ya fedha zitumike kusaidia ajira kwa vijana na fedha za mikopo kwa vijana na kuwezesha Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) na Vyuo vya Ufundi Stadi Nchini (VETA), kukopesha vijana, kuanzisha utaratibu wa vijana kujiunga katika vikundi wakiwa vyuoni na mfuko huo uratibiwe na Ofisi ya Rais.HABARILEO

Post a Comment

 
Top