0
Siasa kwa maelezo makini na mafupi ni:
“…Itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani, ambao ni msingi wa kuendesha uchumi wake; utamaduni na mwenendo mzima wa maisha ya jamii hiyo; mfumo wa mawazo yaongozayo utawala wa Serikali ya nchi. Pia ni utaratibu wa utekelezaji au uendeshaji wa jambo kwa kutumia busara na hekima ili kufikia lengo tarajiwa sawia.”
Tuliokuwepo enzi hizo, sasa tunayo fursa nzuri ya kulisemea jambo hilo ‘siasa’, hata kuchanganua tofauti zake kwa nyakati husika. Siyo lazima uitwe mwanasiasa ili kuweza kuona tofauti ya jambo lenyewe, bali akili na hekima zako timilifu unayaweza hayo.
Wapo baadhi ya watu katika jamii, wenye kuielezea siasa kama ifuatavyo. Mtu mmoja alisema hivi; “…Siasa za sasa ni za kuchumia tumbo, yaani za kuganga njaa.” Mwingine alisema; “…Ukijua kujikomba au kujipendekeza kwa viongozi wakubwa walioko madarakani, hata kwa jambo lisilo na mashiko ama la kijinga, basi na wewe utakuwa mwanasiasa na utafanikiwa kupanda juu, hata ukiwakejeli watu.”
Naye J.J Kizibo wa Mikwamba Muheza (jina siyo lake) alisema; “siasa za kweli zilikuwepo kabla ya Uhuru wetu na miongo miwili iliyofuatia, ila hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na baadhi ya viongozi aliokuwa nao awali wao wameondoka na ‘siasa’ za kweli”.
Francis Chandima wa Handeni amesema hivi; “...Hapa hakuna siasa bali ni sarakasi za siasa, hivi tumwombe Mungu kwa kiasi gani ili atuondolee huu utoto, ujinga na kejeli za siasa kwa taifa na wananchi wetu kwani matarajio endelevu ya nchi yetu yanatoweka.”
Sarakasi za siasa
Zipo, kwani sarakasi imeelezwa kuwa ni; “…Michezo ya kistadi ya kuonyesha vitendo visivyo vya kawaida na vya ajabu; kama vile tembo kupanda baiskeli, nyoka kacheza muziki wa kwaito; au mtu kawatukana wengine, lakini anaowafurahisha wanasema; “…Kajibu mapigo, hivyo yuko sawa tu.” Siasa hizi za sarakasi ni upuuzi mtupu na wanaozishabikia ni wenye mrengo wa kitoto wenye kutia kichefuchefu.
Baadhi ya viongozi wetu wa siasa wanafanya mambo mengi yaliyo nyeti ‘ndiyo sivyo’ na kutulazimisha ati tuyaone kuwa ni kwa maendeleo yetu. Siyo kila mtu ni punguwani au hamnazo, jinsi wanavyotufikiria wao baada ya kuingia madarakani; bali wao ama wengi wao ndio ‘mwapuza’.
Angalia sarakasi ya ufujaji pesa wa IPTL na Escrow zinazohusishwa na wahisani kutukatia laini kwenye pesa za kuboresha bajeti yetu ya 2014-2015. Hivi inaingia akilini kuwa viongozi wetu wakuu kushindwa kupata hesabu au ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Takukuru mapema tangu lilipotamkwa ‘zengwe’ hili?
Spika alalama
Tumesoma magazetini kwamba Spika akipiga yowe, ‘Hakuna posho za wabunge’. Mbona hapigi yowe kuwa hakuna pesa kwa mahitaji ya kukidhi maisha ya wananchi?
Wanajamii tunaambiwa wabunge wanapostaafu wanaishi maisha duni. Tuwaelewaje wakati nyumba tatu za maspika wawili zinakula mabilioni ya pesa ile ya Anne Makinda na mbili za Samuel Sitta, nao wabunge wanakaa kimyaa! Au ni ngoma ya jirani?
Sarakasi ya tatizo la maji haliishi, mara mitambo mipya inafungwa Ruvu Juu, Ruvu Chini, mara mambomba makubwa yanatandikwa Boko mara Bunju; na mgawo na ukame wa maji uko palepale. Richmond kaondoka mdogo wake Dowans kalamba dume Mahakama ya kitaifa, analipwa mabilioni ya shilingi na ndugu yao Symbion kapata kazi na umeme ni mgawo vilevile; na kutuunguzia vifaa vyetu majumbani. Sababu za utetezi hata hazikidhi. Kweli ‘nyoka kacheza muziki wa kwaito’.
Kwa mfano wa wazi tumeambiwa tulikuwa na tembo 142,000 Serikali hii ilipoingia madarakani, lakini sasa tuna tembo 55,000 na papo hapo viongozi wanajitetea hakuna ujangili mambo yako sawa wameyadhibiti, wanajamii wanajiuliza vipi? Taifa linapata sifa mbaya ya ujangili na rushwa nje ya nchi imeripotiwa na shirika la kimataifa la uchunguzi huo. Pia, Waziri Membe kwa majibu mepesi anatuambia hizo ni taarifa za mpitanjia tu pale Mwenge kwenye mabanda yauzwayo vinyago. Je, na ile orodha ya majina ya wahusika wakuu na vigogo wa ujangili na bosi wao wa Arusha imefanywa nini? Mbona kimya?
Miaka ya nyuma tuliambiwa wakazi wa Mwanza wanakula makapi ya vichwa vya samaki sangara, viongozi walibisha hadi ilipothibitishwa uuzwaji haramu wa samaki hao nje ya nchi.
Aibu tupu! Ni kweli tuko katika sarakasi za siasa na viongozi ni wepesi wa kukana kila jambo na kukashifu hao wapinzani hata kwa matukio ya wazi yaani wanatufanya wanajamii wote vipofu na viziwi. Rai yangu, tuwalipe Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ingawa tumelipana ‘kiinua mgongo’ kwenye Bunge Maalumu la Katiba, ili nao wanajamii maskini wapate dawa.MWANANCHI

Post a Comment

 
Top