Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza bungeni Dodoma jana
Dar/Dodoma.
Moto wa kashfa ya ufisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow unaoendelea
kuwaka bungeni, sasa unaonekana kugeuka gharika inayoweza kuwakumba
vigogo wengi zaidi na kuiweka Serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika
hali ngumu.
Kashfa hiyo
ya uchotaji wa Sh306 bilioni za akaunti ya Escrow, inahofiwa kuwakumba
vigogo zaidi ya 50 ndani ya Serikali wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu,
wabunge, majaji na wakuu wa taasisi za Serikali waliohusika.
Habari
zilizopatikana zinaeleza kuwa kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya
mawaziri na watendaji wa Serikali na mahakama, inatishia anguko la
Serikali.
“Kuna waziri
(anamtaja) ameniambia ameangalia ile orodha ya watu wanaodaiwa kuchukua
fedha hizo ni zaidi ya 52. Hofu yangu hili jambo likiingia bungeni na
kujadiliwa huenda likasababisha kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri kwa mara
nyingine,” alisema mbunge mmoja kutoka Kanda ya Mashariki.
Wabunge wajipanga
Mbunge
mwingine kutoka Zanzibar (CCM), alisema kuwa anasubiri kwa hamu
kuchangia katika mjadala huo ili waondoke wale wote ambao wamekwapua
fedha hizo.
Juzi, Waziri
Mkuu Mizengo Pinda aliitisha kikao cha mawaziri ambacho kilihudhuriwa
na baadhi ya mawaziri na walifikia uamuzi kuwa suala hilo litajadiliwa
ndani ya chama kabla ya kuingia ndani ya Bunge.
“Kinachosubiriwa
ni ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) halafu tutakutana
wabunge wa CCM kabla ya kwenda bungeni,” alisema mmoja wa wajumbe wa
kikao hicho.
Pamoja na
hali hiyo, wabunge katika makundi makundi kwa wiki nzima wamesikika
wakijadili jambo hilo huku wakilihusisha na mbio za urais mwakani.
Mbunge mmoja
(jina tunalo) alisema kuhusishwa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika
sakata hilo kunatokana na mtuhumiwa mmoja ambaye ni kiongozi katika
Wizara ya Nishati na Madini, kuwa mmoja wa meneja wake wa kampeni.
“Hakuna
mahali ambapo Pinda ameguswa moja kwa moja katika ripoti ya CAG
(Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) wala Takukuru (Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), bali wanasema ni kwa sababu ya
kampeni za urais na mhusika mmoja katika sakata hilo anatajwa kuwa kama
Pinda akipata urais, yeye ndiye atakayekuwa Katibu Mkuu Kiongozi,”
alisema mbunge huyo kutoka upinzani.
Jana Mbunge
wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu akizungumza na gazeti hili,
alisema sakata hilo linatakiwa liishe kwa kuwa linaumiza uchumi wa nchi
kwa kuwa mtambo wa IPTL ni matatizo.
“Hili jambo kwa namna yoyote lazima liishe na kwamba mwisho wake ni bora tutaifishe ule mtambo na ufie mbali,” alisema Mangungu.
Alisema
linatakiwa liishe kwa kuwa limekuwa ni jambo la kushutumiana kila upande
kitu ambacho si kizuri, na kwamba Bunge linapaswa kusimama kuonyesha
makali yake.
“Ni mzigo kwa wananchi hivyo lifike mwisho. Ni heri shari yenye heri kuliko heri yenye shari,” alisema Mangungu.
Mbunge wa
Ole (CUF), Rajabu Mohammed Mbarouk alisema sakata hilo limetokea juu na
sasa limefika chini na kukwamisha mambo mengine yasifanyike.
“Bunge
haliwezi kuisha kwa kuwa linagusa masilahi ya watu wengi, pia linagusa
masilahi ya chama. Hili hata lijadiliwe bungeni haliwezi kuisha hivyo,”
alisema Mbarouk.
Alisema ni
jambo la ajabu kama alivyosema Zitto kwamba halikufaa kufanyika kwenye
nchi ambayo ina dola, bali lingefanyika kwenye nchi ambazo hazina
mhimili wa dola kama Somalia.
“Haya mambo yanaweza kumwangusha Waziri Mkuu na wengine, hivyo ni jambo zito,” alisema Mbarouk.
Mbunge wa
Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali akiwasilisha maoni ya kambi
ya upinzani kuridhia Itifaki ya Uzuiaji wa Vitendo Haramu dhidi ya
Miundombinu jana, alisema viongozi kama wabunge na mawaziri wametajwa
kupiga dili katika akaunti ya Tegeta Escrow kwa kuwa viongozi wa
Serikali hawaonyeshi dhamira njema katika kuheshimu misingi ya utawala
bora na ndiyo maana wezi na mafisadi wanaotakatisha fedha kiharamu
wameendelea kuachwa.
Alisema
katika uchotwaji wa fedha hizo, Serikali imedhihirisha wazi kwamba
ufisadi ni sehemu ya maisha ya baadhi ya mawaziri na watendaji wa
Serikali.
“Ni aibu na
majanga kwa Waziri Mkuu na mawaziri wengine kusema kwamba suala la
Escrow haliwezi kuzungumzwa bungeni kwa sababu eti liko mahakamani,
jambo linaloashiria Waziri Mkuu anakusudia kuwalinda wale wanaotajwa
kuchota fedha hizo,” Machali alisema na kuongeza:
“Mbaya zaidi
ni pale inapoonekana wazi mhimili wa Bunge unaingiliwa na mhimili
mwingine unaotajwa kuliandikia Bunge barua likitaka kutojadiliwa sakata
la Escrow jambo ambalo ni dharau kwa Bunge.”
Kwa upande
wake, Zitto ambaye kamati yake inapitia ripoti hiyo hakutaka kuzungumzia
chochote kuhusu sakata hilo lakini juzi aliwataka wabunge wajiandae
kupambana na taarifa atakazoziwasilisha mezani mara tu ripoti hiyo
itakapokabidhiwa bungeni kwa ajili ya majadiliano.
Escrow yavuka mipaka ya nchi
Sakata la
utoroshwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow ambalo linawaandama baadhi
ya watendaji wakuu wa Serikali limejitokeza kwa sehemu kubwa katika
baadhi ya magazeti ya nchi za Magharibi yaliyohoji jinsi Serikali
inavyoingiwa na kigugumizi cha kulipatia ufumbuzi sakata hilo.
Magazeti
hayo likiwamo DailyMail la Uingereza ambalo lililowahi kufichua kuwapo
kwa vitendo vya ufisadi katika uwindaji wa wanyamapori
kulikolisababishia taifa hasara kubwa, lilisema kuwa Tanzania inaendelea
kuandamwa na jinamizi la ufujaji wa mali ya umma.
DailyMail
limesema wabunge wameibana Serikali wakitaka kujadiliwa kwa ripoti ya
Escrow ili kuliokoa taifa ambalo tayari limeanza kuonja machungu ya
kusitishiwa misaada kutoka kwa wafadhili wa kigeni.
Katika
ripoti yake hiyo ambayo imelinukuu Shirika la Habari la Reuters,
DailyMail ilisema rushwa ni ugonjwa unaoendelea kuiandama Tanzania na
kwamba vitendo hivyo sasa vimevuka mipaka na kuwakwaza wawekezaji wa
kigeni.
Limesema
kuwa Tanzania ambayo hivi karibuni ilitangaza kugundua hifadhi kubwa ya
gesi iko katika njiapanda na bado haieleweki hatima yake hasa baada ya
Serikali kuonyesha kuwa haiko tayari kuruhusu ripoti hiyo ijadiliwe
hadharani.
Chanzo - Mwananchi
Post a Comment