Misikiti minne iliofungwa na maafisa wa polisi wiki iliopita baada ya
kuchukuliwa na vijana wenye itikadi kali za kiislamu hatimaye
imefunguliwa.
Hatua ya kuifungua misikiti hiyo ya Minaa,Sakina,Musa na Swafaa inajiri
baada ya siku mbili za mazungumzo kati ya viongozi wakuu wa
kiislamu,wataalam na uongozi wa kaunti ya Mombasa.
Maelezo ya mazungumzo hayo yalioandaliwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho na kaunti kamishna Nelson Marwa yamefanywa kuwa siri.
Kabla ya misikiti hiyo kufunguliwa ,viongozi wa kiislamu pamoja na
wataalam walilazimika kuajiri kiongozi wa dini wa kila msikiti na kubuni
kamati maalum ya kusimamia misikiti hiyo ya kisauni na majengo mjini
Mombasa.
''Hatutaki wajisikie kana kwamba serikali ina wakandamiza.Tumewapa mda
wa kuzungumza na kuamua kuhusu kamati za misikii hiyo na viongozi w dini
ambao watakuwa wakisimamia ibada.Watatupatia majina na kufikia
kesho{leo} misikiti hiyo itafunguliwa'',alisema bwana Marwa ambaye ndio
mwenyekiti wa kamati ya usalama kaunti ya Mombasa.
Duru zinaarifu kuwa miongoni mwa wale walioalikwa katika mazungumzo hayo
ni viongozi wakuu wa kiislamu wakiwemo wawakilishi kutoka baraza kuu la
waislamu nchini Kenya SUPKEM,barasa kuu la ushauri wa maswala ya
kiislamu na baraza la maimamu na wahubiri nchini Kenya CIPK.
Misikiti hiyo ilifungwa wiki iliopita na maafisa wa usalama baada ya
uvamizi katika Msikiti wa Musa pamoja na msako wa kuwanasa zaidi ya watu
250 ambao baadaye walishtakiwa kwa kuwa wanachama wa makundi ya
kigaidi.
Maafisa wa polisi pia walionyesha baadhi ya silaha na nakala ambazo wanasema zilipatikana katika msikiti huo.
Muda mchache baada ya kukamatwa kwao,magenge ya vijana walizua ghasia na
kuanza kuwashambulia raia wasio kuwa na hatia katika vituo vitatu vya
mabasi pamoja na makaazi katika eneo la kisauni.
Wakati wa ghasia hizo watu watatu walidungwa visu na kufariki huku wengine saba wakijeruhiwa vibaya.
Viongozi wa kiislamu mjini Mombasa na maeneo mengine ya nchi wamekuwa
wakitaka kufunguliwa kwa misikiti hiyo ambayo imekuwa katikati ya utata
kuhusu madai kwamba ilikuwa inatumiwa kuwafunza vijana itikadi kali
mbali na kuhifadhi silaha kinyume na sheria.
Post a Comment