0
Waziri Mkuu,Mizengo Pinda.
Kasheshe iliibuka katika zoezi la uandikishaji la wakazi  katika Mtaa wa Mbondole katika Kata ya Msongola  Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam baada ya makarani kuandikisha majina kwenye kituo bubu cha Shule ya Msingi Mbondole.

Tukio hilo lilitokea juzi  asubuhi baada ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) tawi la Mbondole kubaini  mbinu  hiyo kuwa  inaweza kutumika kuandisha  majina watu ambao siyo wakazi, hivyo kuamuru kituo hicho kisitishwe na kuhamia kituo cha Sekondari ya Mbondole.

Wanachama hao wa CUF walikuwa wamejiandaa wakiongozwa na mgombea wao wa nafasi ya uenyekiti wa Mtaa wa Mbondole, Mrisho Jogoo huku wengine wakisikika wakisema kuwa wamezoea kuongeza majina na kuwa siku hiyo pangechimbika.

Baada ya purukushani hizo, Jogoo aliiambia NIPASHE kuwa  baada ya kufika katika kituo hicho alfajiri walikuta majina yameshaandikishwa, hivyo kwa pamoja wafuasi wa CUF na Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikubaliana kuyachoma moto ili zoezi lianze upya.

Jogoo alisema kuwa walikubaliana kuwa bila kufanya hivyo, vurugu zingetokea.

“Hata karani  Mary Sanga tulipoongea naye hakuonyesha kubisha, hilo lilisaidia sana kuepusha shari na kukiri kuwa walifanya kosa kuandikisha kwenye kituo ambacho hakijaruhusiwa kisheria. Pia alituambia kuwa  kilichosababisha ni mawasiliano kutokuwa mazuri,” alisema.

Alisema katika Mtaa wa Mbondole kikako kiliamua kutenga kituo  kimoja cha uandikishaji cha shule ya sekondari.

Afisa Mtendaji  Kata wa Msongola, Omari Ally, alisema pamoja na tukio  la kuchanganya kituo, kilichotokea katika Mtaa wa Mbondole, lakini zoezi la uandikishaji  zinakwenda vizuri.

“Hakuna tatizo kubwa lililotokea kama ni kuchoma majina yalikuwa ni maamuzi ya hekima ili kila upande kuondoe hofu kuwa walioandikishwa hawakuwa wakazi wa Mtaa wa Mbondole,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

 
Top